Ninawezaje Kuendelea Kumtumaini Mungu Wakati Na Pambana Na Gharama Za Maisha?

Ukweli ni kwamba, gharama zinapoongezeka huku kipato kikiwa hakitoshi, sio rahisi kuendelea kuwa na imani na utulivu moyoni.

Unaomba, unapanga, unafanya kazi kwa bidii, lakini bado mambo ya kifedha hayaendi kama ulivyotarajia. Kama umewahi kujiuliza, “Mungu yuko wapi katika hali hii?” ujue hauko peke yako. Changamoto za kifedha mara nyingi huibua maswali ya kiroho yanayoweza kuitikisa hata imani ya mtu mwenye msimamo imara.

Katika makala haya, tutachunguza jinsi Neno la Mungu linavyozungumzia moja kwa moja changamoto za kifedha, na namna ambavyo imani inaweza kutupa nguvu ya kuendelea hata katikati ya hali ngumu.

Utajifunza:

Hebu tupitie hekima ya kudumu ya kibiblia inayotoa tumaini hata wakati wa changamoto za gharama za maisha.

Unapokuwa na kidogo sana au huna chochote: jinsi wahusika wa Biblia walivyopata nguvu

Biblia imejaa watu waliopitia changamoto za kifedha na ukosefu wa mahitaji.

Ayubu alipoteza mali zake zote, watoto wake, na hata afya yake. Mjane wa Sarepta alibaki na unga kidogo na mafuta machache tu wakati wa njaa kali. Waisraeli nao walitembea jangwani kwa muda mrefu bila uhakika wa chakula, kipato, au makazi ya kudumu.

Lakini katika kila hali, walijifunza jambo kubwa sana: Mungu anaweza kutunza na kutoa mahitaji ya watu wake hata pale ambapo kwa macho ya kibinadamu inaonekana haiwezekani.

Hadithi hizi zinatukumbusha kwamba changamoto za kifedha hazimaanishi Mungu amekuacha au hayupo pamoja nawe. Mara nyingi, ni katika nyakati hizo ngumu ndipo Mungu huonyesha uaminifu wake.

Maandiko yanasema:

“Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu” (Wafilipi 4:19 SUV).

Kumtegemea Mungu kwa mahitaji yako ya kifedha huanza kwa kukumbuka Yeye ni nani—Baba anayekuona, anayejali, na anayejua jinsi ya kukupa mahitaji yako.

Kwa hiyo, ikiwa mifano ya Biblia inatuonyesha kwamba Mungu anaaminika, tunaushikiliaje ukweli huo wakati hofu na wasiwasi vinajaribu kututawala?

Kulinda moyo wako dhidi ya hofu na mashaka

A man reading Bible promises to strengthens his faith as he waits for God to come through for him in his financial struggles.

Photo by Oladimeji Ajegbile

Kuhangaika na wasiwasi kunaweza kuhisi kama kazi ya muda wote wakati matumizi ni makubwa na kipato ni kidogo. Unaweza kujikuta ukijaribiwa kuuliza, “Kwa nini Mungu hanisaidii?” au “Nikishindwa kumaliza mwezi huu nitaishije?”

Hata hivyo, Mungu hataki tuishi na hofu. Anatuita kuishi maisha yasiyo na wasiwasi, yanayoegemea katika maombi badala ya hofu na paniki.
Yesu alihamasisha kuwa na imani katika upatano wa Mungu:

“Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:31-33, SUV).

Kulinda moyo wako kunamaanisha kuchagua imani badala ya hofu, tumaini badala ya kukata tamaa, na shukrani badala ya kunung’unika. Kunamaanisha kumwendea Mungu mara kwa mara kwa maombi, kuomba msaada na hekima, na kukumbuka kwamba Yeye ndiye mwenye mamlaka na udhibiti wa mwisho wa kila kitu.

Jizoeze kutoa shukrani hata katika nyakati ngumu, kwa sababu moyo wa shukrani ni moyo wenye amani.

Hata hivyo, kulinda moyo wako sio jambo la kukaa tu bila kufanya chochote. Kunamaanisha kuchukua hatua—sio tu kihisia na kiroho, bali pia kwa vitendo katika maisha ya kila siku.

Ukweli unaotia moyo kuhusu utoaji wa Mungu na wakati wake unaofaa

Wakati mwingine, msaada wa Mungu huja kupitia njia zisizotarajiwa: ukarimu wa rafiki, nafasi mpya ya kazi, au hata kurejeshewa fedha kwa wakati unaofaa.

Kumwamini Mungu kunamaanisha kumtambua Yeye kama mmiliki halali wa vyote tulivyonavyo, na kuamini kwamba atatupatia mahitaji yetu kwa wakati unaofaa tunapoyahitaji.

Maandiko yanatukumbusha:

“Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA,…” (Zaburi 24:1, SUV).

Sisi ni mawakili, sio wamiliki. Hii inamaanisha kwamba tunasimamia yale ambayo Mungu ametukabidhi.

Mungu anataka tuishi kwa amani, sio kwa hofu au wasiwasi. Hata hivyo, pia hutumia hali mbalimbali kutujenga na kuimarisha imani yetu. Mara nyingi, hutufundisha nidhamu, uvumilivu na kumtegemea Yeye zaidi kabla ya kufungua njia za baraka na uhuru wa kifedha katika maisha yetu.

Hivyo basi, usichukulie kuchelewa kwa majibu ya Mungu kuwa ni kukataliwa. Huenda muda wa kusubiri ukawa mrefu, lakini baraka inayokuja huwa na thamani kubwa. Mungu hawaachi watoto wake, hasa wanapokuwa katika wakati mgumu wa mahitaji.

Tunapokuwa tukisubiri Mungu atutimizie mahitaji yetu, tunaweza kuchukua hatua gani za busara na za uaminifu ili kusimamia vizuri hali yetu ya kifedha?

Tabia zinazoongozwa na imani ambazo huleta amani katikati ya misukosuko ya kifedha

A person drafting a budget as part of their step to understand their financial obligations.

Photo by Jakub Żerdzicki on Unsplash

Imani bila matendo ni imani isiyo kamili.

Wakati unamtegemea Yesu kuhusu fedha zako, pia jitahidi kuwa wakili mwema wa kile ulichopewa. Anza kwa kupanga bajeti yako. Andika kipato chako, matumizi yako, na madeni uliyo nayo. Kisha tengeneza mpango unaolingana na maadili yako na vipaumbele vyako katika matumizi ya fedha.

Mpe Mungu malimbuko ya kipato chako kupitia zaka na ukarimu. Hilo linaweza kuonekana kama hatari wakati fedha ni chache, lakini ni tamko la kumtegemea Mungu. Unakuwa unatangaza, “Bwana, naamini utatoa na kunitosheleza.”

Epuka tabia zisizo za busara za matumizi ya fedha ambazo zilisababisha makosa au matatizo ya kifedha hapo awali. Mwombe Mungu msamaha kwa makosa yako ya kifedha na nguvu ya kujenga tabia bora zaidi. Chagua kuridhika badala ya kujilinganisha na wengine, na jizoeze ukarimu hata katika mambo madogo madogo.

Kumbuka: amani ya kifedha haitegemei kuwa na pesa nyingi zaidi, bali inategemea kumweka Mungu mbele katika kila jambo la maisha yako. Na kwa njia ya kushangaza, unapompa Mungu nafasi ya kwanza, ndipo unapoanza kuwa na mwelekeo sahihi na udhibiti wa hekima juu ya fedha zako.

Ukweli ni kwamba hauko peke yako katika hali hii. Unaweza kutegemea Maandiko Matakatifu, maombi, na mfano wa watu wengine waliowahi kupitia njia hii kabla yako.

Mungu bado ndiye anayekutimizia mahitaji yako

Changamoto za kifedha ni za kweli, lakini Mungu wako pia ni wa kweli.

Unapomtegemea Mungu katika mahitaji yako, kuishi kwa kufuata kanuni zake, na kuweka ufalme Wake mbele, unapata amani ya kina na ya kudumu zaidi. Moyo wako ushikilie ukweli huu: Mungu ni mwaminifu, na hatawaacha watoto Wake.

Kwa hiyo, tulia kidogo, mwendee Mungu kwa maombi, tumaini, panga kwa hekima, na utoe shukrani. Kisha endelea kufanya hivyo kila siku.

Je, ungependa kujifunza zaidi mafundisho ya Biblia yanayogusa changamoto unazopitia?

Tembelea sehemu za Imani na Fedha za Hope for Africa ili upate mafundisho ya vitendo yanayoongozwa na Roho wa Mungu kuhusu jinsi ya kukabiliana na maisha kwa hekima, utulivu, na amani.

Hapa kuna makala chache zenye mafundisho yenye nguvu ya kuanzia:

Pakua na usome makala haya, na acha Maandiko yarejeshe tumaini lako, yabadilishe mtazamo wako, na yakukumbushe: haujasahaulika. Mungu bado anaendelea kufanya kazi, hata sasa.

Pin It on Pinterest

Share This