Nifanye Nini Ninaposhindwa Kuwaamini Watu?

Mahusiano yenye afya hujengwa juu ya msingi wa kuaminiana. Lakini kwa watu wengi, kuwaamini wengine sio jambo linalokuja kwa urahisi.

Huenda uliwahi kuumizwa na mtu uliyempenda au kuvunjwa moyo na mtu uliyekuwa unamheshimu na kumwamini. Labda ulisalitiwa na mwenzi wako wa maisha, au unaendelea kuumizwa na mwana familia anayekukatisha tamaa mara kwa mara.

Ikiwa umewahi kupitia hali kama hizi, basi unafahamu jinsi imani inapovunjika inavyoweza kuacha majeraha makubwa moyoni, kiasi kwamba huwa vigumu sana kufungua moyo wako na kuwaamini watu tena.

Habari njema ni kwamba, hata kama imani yako imewahi kuvunjwa, sio lazima uendelee kuishi ukiwaogopa au ukiwashuku watu. Biblia inatambua kwamba wanadamu hukoseana, lakini pia inatufundisha jinsi ya kujenga tena imani, kuweka mipaka yenye afya, na kupata usalama katika upendo wa Mungu usiobadilika. Badala ya kuficha maumivu ya zamani, kujifunza kuufungua moyo tena hutuwezesha kupona.

Ili kukusaidia kuelewa nini cha kufanya unapopata ugumu wa kuwaamini watu, tutajifunza:

Tuanze kwa kuelewa kwa nini sio rahisi kuwaamini watu.

Kwa nini kuwaamini watu kunaweza kuwa jambo gumu

Kuamini kunahitaji kuwa tayari kufungua moyo wako na kuonyesha udhaifu wako. Na hilo sio jambo rahisi.

Kila tunapomwamini mtu mwingine, tunajiweka katika hali ya kuhatarisha jambo fulani—iwe ni kukatishwa tamaa, kukataliwa, au hata kusalitiwa.

Watu wengi wanaopata ugumu wa kuwaamini wengine mara nyingi huwa wamepitia historia ya kudanganywa, kuchanganyikiwa, kutelekezwa, na kuvunjiwa ahadi. Uzoefu wa aina hii unaweza kumwacha mtu akiwa na majeraha ya ndani na hisia nzito zinazomuumiza.

Cha kusikitisha ni kwamba, kutowaamini wengine kunaweza pia kuathiri mahusiano yetu, kwa kuwa maumivu yasiyoponywa mara nyingi husababisha maumivu zaidi.

Changamoto ya kuwaamini wengine mara nyingi hujidhihirisha kupitia tabia au dalili mbalimbali. Unaweza kujitambua kwa mambo kama haya:

  • Kuamini kwamba watu watakuumiza au watakukatisha tamaa
  • Kushindwa kufungua moyo wako na kuwaeleza wengine mambo yako binafsi
  • Kuogopa kujiachia kwenye mahusiano kwa hofu ya kuumizwa au kukataliwa
  • Kutilia shaka kila jambo na kuhoji nia ya watu wanaokuzunguka
  • Kutaka kudhibiti kila hali ili usije ukaumizwa tena
  • Kuepuka kabisa kujenga mahusiano ya karibu na wengine

Ingawa tabia hizi zinaweza kuwa njia ya kujilinda dhidi ya kuumizwa, mara nyingi hujenga kuta za kihisia zinazotuzuia kufurahia mahusiano ya karibu na yenye maana tunayoyatamani.

Lakini changamoto hizi za kuwaamini wengine huanzia wapi?

Jinsi uzoefu wa zamani unavyoathiri uwezo wetu wa kuwaamini wengine

Mambo tuliyopitia zamani mara nyingi huathiri namna tunavyowaona watu leo. Mtu anapopitia jambo lenye maumivu, akili yake kwa kawaida hujaribu kumlinda ili jambo hilo lisitokee tena, au asipitie hali yoyote inayofanana nayo.

Kwa baadhi ya watu, ugumu wa kuwaamini wengine unatokana na mambo waliyopitia utotoni. Mtoto anayekulia katika mazingira yenye ukosefu wa upendo na uangalizi wa kihisia, migogoro, au kutokuwa na utulivu anaweza kujifunza kuona mahusiano kama sehemu isiyo salama.

Maumivu au majeraha aliyopitia yanaweza kumfanya ashindwe kujisikia salama hata akiwa na watu wema wanaoweza kuaminiwa. Anapokua, uzoefu huu unaweza kuathiri namna anavyojenga na kudumisha mahusiano na wengine.

Kwa mfano, mtu ambaye ana hofu ya kuachwa anaweza kuwa na wasiwasi kila mara na kutafuta uhakikisho kutoka kwa wengine kwamba bado wanampenda na hawatamuacha. Lakini mtu anayejenga ukuta wa kihisia anaweza kushindwa kuruhusu watu wamkaribie na kuchagua kuweka umbali katika mahusiano yake.

Mara nyingi mifumo hii hujengeka ndani yetu bila sisi kufahamu. Huenda tukaanza kuwaona watu wote kama wasioweza kuaminiwa, kwa sababu mambo tuliyopitia zamani yametufanya tuwe na matarajio kwamba mwisho wake tutasalitiwa tu.

Basi, tunaweza kufanya nini kuhusu hali hii? Ni kweli kwamba yaliyopita yanaweza kuathiri namna tunavyoona na kuishi maisha yetu leo, lakini hayapaswi kuwa hadithi yote ya maisha yetu. Bado kuna tumaini la kesho, na uponyaji unawezekana.

Na mojawapo ya sehemu bora tunazoweza kupata uponyaji ni katika Neno la Mungu.

Biblia inasema nini kuhusu kuaminiana na mahusiano

An upclose photo of a man holding and reading an open Bible.

Photo by Emmanuel Phaeton on Unsplash

Biblia inaonyesha wazi jinsi wanadamu wanavyoweza kufanya makosa na kushindwa. Hata hivyo, Mungu hubaki kuwa mwaminifu na anayestahili kuaminiwa kikamilifu. Tunapotambua kwamba watu wanaweza kutuangusha, lakini Mungu hatatuacha kamwe, tunaweza kujifunza kujenga mahusiano yetu kwa msingi wa imani, hekima, na ufahamu sahihi wa wanadamu.

Zaburi 118:8 inasema:

“Ni heri kumkimbilia BWANA
Kuliko kuwatumainia wanadamu” (SUV).

Aya hii haisemi kwamba hatupaswi kamwe kuwaamini watu. Badala yake, inatukumbusha kwamba msingi wa usalama wetu wa kweli unapaswa kuwa kwa Mungu, sio kwa wanadamu ambao wanaweza kukosea na kutuangusha.

Biblia pia inatuhimiza kujenga mahusiano yenye afya yanayojengwa juu ya misingi kama vile uaminifu, uadilifu, na upendo:

“Rafiki hupenda sikuzote;
Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu” (Mithali 17:17, SUV).

Na sifa hizi zinahitaji kiwango fulani cha kuaminiana. Mfano mzuri ni urafiki kati ya Yonathani na Daudi. Akiwa mwana wa mfalme, Yonathani ndiye aliyekuwa mrithi wa kiti cha enzi kwa haki yake ya kuzaliwa. Lakini alipogundua kwamba baba yake alitaka kumuua Daudi, alisimama upande wa Daudi na kuahidi kudumisha urafiki wao.

Hakukubali kumdhuru Daudi ili ajipatie ufalme huo mwenyewe (1 Samweli 20). Badala yake, alimtafuta Daudi nyikani ili kumtia moyo na kumsaidia kuendelea kumtegemea Mungu (1 Samweli 23:14-18).

Huu ni mfano mmoja tu kati ya mifano mingi ya mahusiano yenye kujenga na jamii zenye mshikamano zinazopatikana katika Biblia. Mungu alituumba ili tuwe na uhusiano na wengine, tushirikiane, na kusaidiana, sio kuishi maisha ya kujitenga (Mwanzo 2:18).

Hata hivyo, imani inayofundishwa na Biblia huunganisha upendo na hekima. Mungu anatufundisha kutumia utambuzi katika kuchagua namna ya kuhusiana na wengine, bila kufunga mioyo yetu kwa mahusiano mazuri na yenye kujenga.

Hili linatufanya tujiulize swali muhimu: Tunawezaje kuweka uwiano kati ya kuamini na kutumia hekima baada ya kuumizwa?

Tofauti kati ya uaminifu, msamaha, na hekima

Kuaminiana, kusamehe, na kuwa na hekima vinaweza kuhusiana, lakini vinatofautiana. Tunapofahamu tofauti yake, tunaweza kuepuka kuchanganya mambo haya na kuwa na matarajio yasiyofaa katika mahusiano.

Msamaha unamaanisha kuachilia uchungu na kutokuchagua kulipiza kisasi. Mungu anatuita tuwasamehe wengine kwa sababu ametusamehe sisi (Waefeso 4:32).

Hata hivyo, kuaminiana mara nyingi huhitaji muda ili kujengwa upya. Huenda isiwe busara kumwamini mara moja mtu ambaye amekuwa akivunja ahadi mara kwa mara au amekuwa akikudhibiti kwa njia isiyo sahihi, hasa ikiwa bado hujaona mabadiliko ya kudumu.

Hekima hutusaidia kuweka mipaka inayofaa huku tukiendelea kuwa na moyo wa kusamehe.

Fikiria mfano huu:

  • Msamaha unasema: “Ninaachilia hasira yangu.”
  • Kuaminiana kunasema: “Ninahitaji kuona mabadiliko yanayoendelea kabla ya kuweza kumwamini tena kikamilifu.”
  • Hekima inasema: “Naweza kuwa mwenye wema huku pia nikijilinda na kulinda ustawi wangu.”

Watu wengi hufikiri kwamba wanapaswa kumwamini mtu kabisa au kukataa kabisa uhusiano naye. Lakini kujenga upya kuaminiana katika mahusiano yenye afya ni mchakato wa hatua kwa hatua, ambapo mtu aliyeumizwa anahitaji kuona ushahidi kwamba mwenzake anaweza kuaminika.

Hivyo, kujenga upya uaminifu huonekanaje katika maisha halisi?

Hatua za kujenga upya uaminifu kwa njia zenye afya

Inachukua muda kufikia hatua ambayo uko tayari kuwaamini wengine tena. Ingawa mchakato huu unahitaji juhudi za makusudi, kuwa mvumilivu na nafsi yako. Iwe unajifunza kuwaamini wengine tena au unajaribu kurejesha uhusiano ulioharibiwa, kanuni hizi zinaweza kukusaidia.

  1. Kubali maumivu yako

Uponyaji huanza kwa kuwa mkweli kuhusu maumivu yako. Kuficha maumivu ya kihisia kutayafanya kuwa makubwa zaidi. Tambua jinsi yale yaliyokupata yamekuathiri.

  1. Tambua chanzo cha tatizo

Jiulize:

  • Ni mambo gani niliyopitia ambayo yamesababisha niwe na ugumu wa kuwaamini wengine?
  • Hofu zangu zinatokana na hali ninayopitia sasa au majeraha ya zamani?
  • Namna yangu ya kujenga uhusiano wa karibu imeathiri vipi mahusiano yangu?

Kuelewa sababu zinazofanya iwe vigumu kuwaamini wengine kunaweza kukusaidia kuchukua hatua kwa hekima zaidi.

  1. Anza hatua ndogo

Kuaminiana sio jambo la kuwa na msimamo wa pande mbili tu. Kumwamini mtu bila tahadhari na kujifungia kabisa dhidi ya wengine vyote viwili sio njia yenye afya. Waruhusu watu wajenge uaminifu taratibu kupitia matendo yao yanayoonekana kwa muda.

  1. Angalia sifa za watu wanaoweza kuaminika

Watu wanaoweza kujenga mahusiano salama mara nyingi huonyesha:

  • Uaminifu
  • Kutegemewa
  • Unyenyekevu
  • Kuwajibika
  • Uthabiti

Zingatia mwenendo wao unaojirudia kuliko ahadi zao.

  1. Tafuta msaada unapouhitaji

Wakati mwingine changamoto za kuwaamini wengine zinahusiana na majeraha ya zamani au changamoto za afya ya akili.

Mtaalamu wa ushauri nasaha au mshauri Mkristo anaweza kukusaidia kuelewa na kushughulikia yale uliyopitia, pamoja na kujenga njia bora za kuhusiana na wengine. Ikiwa unaona kutafuta msaada wa ushauri nasaha ni ishara ya udhaifu, kumbuka kwamba sio hivyo. Inaweza kuwa chombo muhimu katika uponyaji na ukuaji.

Wakati mwingine tunahitaji mtu mwingine atusaidie kuona mambo kwa mtazamo tofauti na kutusaidia kuelewa hisia na mawazo yetu.

Lakini tunapochukua hatua hizi za vitendo, tukumbuke kwamba kuna chanzo kimoja cha usalama ambacho hakishindwi kamwe.

Jinsi kumtumaini Mungu kunavyoweza kukusaidia katika mahusiano yako na wengine

A pastor in grey suit and brown leather shoes preaching on the pulpit.

Kumtumaini Mungu huweka msingi imara unaowezesha kujenga mahusiano yenye afya. Tunapoweka tumaini letu lote kwa wanadamu, tunajiweka katika hali ya kuumizwa na kukatishwa tamaa mara kwa mara, kwa sababu hakuna mwanadamu aliye mkamilifu.

Hata hivyo, upendo wa Mungu haubadiliki.

Isaya 26:3 inatukumbusha:

“Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini” (SUV).

Tunapomwamini Mungu, hatuhitaji kujaribu kudhibiti kila hali au kuishi katika hofu ya kila wakati. Tunaweza kujifunza maana ya kuwa na ujasiri, kutumia utambuzi, na kuwa na uwiano mzuri wa kihisia katika mahusiano yetu.

Je, hii inamaanisha kwamba hatutaumizwa tena? Hapana. Tunaishi katika ulimwengu uliovunjika wenye mateso na maumivu. Lakini tegemeo letu liko kwa Yeye ambaye habadiliki kamwe, sio katika kujaribu kuepuka maumivu.

Mungu anaweza kuponya majeraha yaliyosababishwa na usaliti. Anaweza kutusaidia kushinda hofu na wasiwasi wetu, kurejesha uwezo wetu wa kuunganishwa na wengine, na kutufundisha kujenga mahusiano yenye afya na yanayotuletea uzima.

Kuamini tena inawezekana kwa msaada wa Mungu

Kupata ugumu wa kuwaamini wengine ni hali ambayo watu wengi hupitia. Huwa ni vigumu zaidi ikiwa hali hiyo inatokana na jeraha kubwa la kihisia. Changamoto ya kuwaamini wengine haiathiri tu mtu aliyeumizwa. Kutowaamini wengine kunaweza pia kupotosha namna tunavyowaona na kuhusiana nao.

Lakini uponyaji unawezekana.

Kwa kuelewa sababu zinazosababisha kutokuamini, kutumia hekima ya Biblia, kuweka mipaka yenye afya, na kumweka Mungu kuwa tegemeo lako kuu, unaweza kutoka kwenye hofu na kutokuamini na kuelekea kwenye mahusiano yenye afya na imara zaidi.

Ikiwa imekuwa vigumu kwako kuwaamini wengine, kumbuka kwamba Yesu anaelewa. Amepitia kukataliwa, kuvunjwa kwa ahadi, na kusalitiwa, pamoja na mambo mengine mengi. Anajua jinsi inavyokuwa kuumizwa. Lakini bado moyo Wake umejaa upendo usio na masharti. Hivyo, mletee Yeye hofu zako, masikitiko yako, na maswali yako. Anajua kila kitu, na anaweza kubeba yote.

Ikiwa ungependa kuendelea kuchunguza kile Biblia inachofundisha kuhusu mahusiano, tunakualika utembelee sehemu yetu ya Mahusiano. Utapata mafundisho ya vitendo yanayotegemea Biblia yatakayokusaidia kushughulikia mahusiano mbalimbali katika maisha yako, kama vile urafiki, familia, mazingira ya kazi, ndoa, na mengineyo.

Haya ni makala mazuri ya kuanzia:

Tunaomba kwamba, unapochunguza nyenzo hizi, utapata uponyaji na ujasiri katika mahusiano yako. Mungu anatamani ufurahie mahusiano yenye maana yaliyojengwa juu ya ukweli, hekima, na upendo—na Neno Lake linatoa mwongozo katika kila hatua ya safari hiyo.

Pin It on Pinterest

Share This