Kwa Nini Kuna Mateso Ulimwenguni?
Tazama tu runinga yako au pitia mitandao ya kijamii, na utashangazwa na vichwa vya habari:
Mauaji. Ukatili. Mashambulizi ya kigaidi. Vita. Majanga ya asili.
Mateso ya mwanadamu yapo kila mahali. Na tunapokumbwa na maumivu na kukata tamaa katika maisha yetu au ya wale tunaowapenda, tunaanza kujiuliza maswali ya kina zaidi.
Huenda unakumbana na unyanyasaji katika mahusiano yako. Au una mpendwa anayekufa kwa ugonjwa wa saratani. Au unapambana na matatizo makubwa ya kifedha hata ukiwa na nidhamu ya hali ya juu katika matumizi. Hali hizi zote ni ngumu na zinaumiza, na zinatufanya tuulize ni kwanini.
Kwa nini mambo mengi huharibika? Kwa nini Mungu anaruhusu mateso yatokee?
Hakuna jibu rahisi kwa hili.
Hili ni jambo linalotugusa kwa undani na kuamsha hisia nyingi. Hatupaswi kupuuza maumivu haya.
Wakati huohuo, tunapata kutiwa moyo kwamba Biblia inatuonyesha picha kubwa zaidi. Hii inatusaidia kuelewa kwa nini dunia imeharibika—kwa nini wakati mwingine mateso yetu hayana maelezo wala sababu.
Maandiko pia yanatuonyesha kwamba Mungu anaelewa mateso yetu—yote kabisa. Sisi sote ni sehemu ya hadithi kubwa zaidi—na kwa neema ya Mungu, ni hadithi itakayomalizika siku moja kwa kuondolewa kwa dhambi, pamoja na uchungu na mateso yote yanayotokana nayo.
Tuchunguze ukweli na tumaini tunaopata katika Biblia kwa kuangalia:
Mateso yalitokea wapi?

Photo by Liana Tril’
Kwa ufupi, mateso ni matokeo ya dhambi katika dunia yetu. Biblia inatufundisha kwamba dhambi ni uvunjaji wa sheria ya upendo ya Mungu (1 Yohana 3:4; Warumi 13:10). Kwa hivyo, dhambi ni nguvu inayopinga upendo halisi na usio na ubinafsi.
Dhambi ilianza zamani sana kupitia malaika mzuri aliyeitwa Lusifa. Alipojaa kiburi na uasi moyoni mwake, alimpinga Mungu na kupewa jina Shetani, linalomaanisha “adui” (Ufunuo 12:7-9). Baadaye, alikuja duniani na kuwajaribu Adamu na Hawa, binadamu wa kwanza, kupoteza imani na kutomtii Mungu (Mwanzo 3).
Kabla ya kukutana na Shetani, Adamu na Hawa waliishi katika dunia kamilifu ambayo Mungu aliiumba. Dunia isiyo na mateso. Lakini kwa sababu Mungu anathamini uhuru wa uchaguzi—uhuru ambao ni muhimu kwa upendo wa kweli—Hakuwazuia nafasi ya kuchagua kinyume na Mungu. Chaguo hili lilionyeshwa kupitia mti uliokuwa katikati ya bustani, unaoitwa “mti wa ujuzi wa mema na mabaya” (Mwanzo 2:9). Aliwaambia wasile matunda ya mti huo, lakini bado aliwapa uhuru wa kuchagua (Mwanzo 2:16-17).
Ndipo Shetani, akachukua mfano wa kiumbe kizuri, alienda kwa Adamu na Hawa, aliwashawishi kuhoji maelekezo ya Mungu, wakatilia shaka upendo wake na haki yake.
Walishawishiwa kula matunda ya mti huo na kupata maarifa yake. Na ingawa walikuwa wakiishi kwa upendo wa Mungu na walikumbuka onyo lake kuhusu mti huo, walivutwa na maarifa haya mapya—ya wema na uovu (Mwanzo 3:1-7).
Kama binadamu wa kwanza, walikuwa wamepata nafasi ya kuishi katika dunia isiyo na kasoro na kuzungumza ana kwa ana na Mungu. Wanawakilisha wanadamu wote kwa sababu walikuwa na kila kitu kwa faida yao…lakini bado walichagua kujua zaidi—nini Mungu alijua ambacho wao hawakujua?
Na hivyo ndivyo uchaguzi huo lilivyoingiza dhambi na ubinafsi katika dunia yetu. Kila mtu angefanya uamuzi huo huo. Kwa hiyo, dhambi ikawa sehemu ya maisha yetu kama wanadamu. Sasa tunaishi tukijua mema na mabaya, yote yakiwa yamechanganyika mbele yetu wakati wote.
Kwa nini Mungu aliruhusu hili kutokea?
Ili kujibu swali hili, tunapaswa kurudi kwenye kisa Lusifa. Ulimwengu ulikuwa kamilifu. Mungu ni mwema, na kila kitu alichoumba ni chema (Mwanzo 1:31). Hii inamaanisha kila sehemu ya ulimwengu ilikuwa kamilifu, pamoja na malaika.
Lakini kwa kuwa Mungu ni upendo, ilimbidi pia kuruhusu uhuru wa uchaguzi. Hangeweza kulazimisha viumbe wake wamfuate, kwa sababu alitaka kuwa na uhusiano wa upendo nao.
Lusifa ndiye kiumbe wa kwanza aliyekataa wema na njia za Mungu na kuchagua njia yake mwenyewe.
Na Lusifa hakuwa malaika wa kawaida. Ezekieli 28 inatuambia kwamba alikuwa “kerubi mlinzi” (mstari wa 14), au “ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye” (mstari wa 14, NKJV), ikionyesha cheo chake cha juu.
Mstari wa 12 unatuambia kwamba Lusifa alikuwa “Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri”(NKJV). Sehemu hiyo inaendelea, ikimweleza Lusifa, “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” (mstari wa 15, NKJV).
Uovu—neno linalomaanisha ‘uasi’—ulikuwa moyoni mwa Lusifa. Alijivuna sana hadi akatamani kuchukua nafasi ya Mungu. Alijiambia:
“Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini, Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye Juu” (Isaya 14:13-14, NKJV).
Mawazo haya yalipoendelea kukaa moyoni mwake, Lusifa alianza kuwashirikisha malaika wengine, ambao aliwavuta upande wake. Mwishowe, uasi uliokuwa moyoni mwake ukageuka kuwa uasi mkubwa mbinguni. Angalia jinsi Ufunuo 12:7-9 inavyoelezea:
“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakuwashinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye” (NKJV).
Shetani (jina lake jipya linaloonyesha kuwa sasa ni adui wa Mungu) alitupwa kutoka mbinguni pamoja na malaika zake.Yesu hata alisema, “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme” (Luka 10:18, NKJV).
Na hatimaye akajikuta duniani.
Ni kweli kwamba Mungu angeweza kumwangamiza Shetani na malaika wake mara moja. Angeweza kuyamaliza yote kabla ya dhambi na uovu kuenea.
Kwa nini hakufanya hivyo?
Yote haya yanaashiria ukweli kwamba Mungu ni upendo (1 Yohana 4:8). Kama Mungu wa upendo, zawadi Yake kwa kila kiumbe alichoumba ni uhuru wa uamuzi(Hiari). Uhuru wa uamuzi ndio njia pekee inayowezesha uhusiano wa upendo kati ya Mungu na viumbe vyake—na hataki kupoteza hilo!
Kwa upendo, Mungu aliruhusu matokeo ya uchaguzi wa Lusifa yawe wazi kwa wakati wake. Kama angemuangamiza Lusifa mara moja, malaika wengine wangejiuliza, Je, Lusifa alikuwa mkweli? Wangeweza kumtumikia Mungu kwa uoga wasije angamizwa. Wangefikiria kwamba Mungu haruhusu uhuru kamili wa maamuzi kama alivyosema.
Ili malaika wengine waone kuwa Mungu alikuwa mwenye haki, walihitaji kuona sheria ya upendo wa Mungu ikilinganishwa na njia za dhambi na ubinafsi wa Lusifa. Walihitaji kuelewa madhara ya dhambi.
Kwa njia hii, malaika—na viumbe wote walioumbwa—wangemtumikia Mungu kwa upendo.
Na uhuru wa kuchagua upo pia kwa wanadamu wote. Kwa sababu kuna uchaguzi unaopingana na Mungu, ulijulikana kwetu, na kuenezwa na yule wa kwanza aliyechagua—Shetani
Matokeo yake, dunia ikalaaniwa (Mwanzo 3:17-19), na ubinafsi ukajitokeza mara moja. Adamu na Hawa walikimbia, wakajificha wasionekane na Mungu, na kila mmoja alianza kumlaumu mwenzake kwa maamuzi aliyofanya. Dhambi ilikuwa tayari inafanya kazi.
Adamu na Hawa punde walikabiliwa na janga lingine wakati mwana wao mkubwa Kaini alimuua mwana wao Habili (Mwanzo 4:8).
Tokea hapo, madhara ya dhambi yalizidi. Binadamu walikuwa wakijali tu maslahi yao wenyewe, wenye majivuno, wauaji, waongo, na wasiowajali wengine. Sifa nzuri za upendo kama huruma, upendo, amani, na furaha zilibadilika kuwa ubinafsi, chuki, machafuko, na kukata tamaa.
Haya ndiyo yalitokea watu walipochagua njia ya dhambi badala ya kushikamana na njia ya upendo wa Mungu. Kufikia wakati wa Nuhu, waandishi wa Biblia walielezea dunia kwa namna hii:
“BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote”(Mwanzo 6:5, NKJV).
Ilimpasa Mungu kuisafisha dunia kwa gharika kwa sababu dhambi ilisababisha uovu na uharibifu mwingi sana—ulimwengu ulikuwa mbaya kiasi kwamba hata Biblia inasema… “BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo” (Mwanzo 6:6 NKJV).
Ingawa gharika ilisaidia kupunguza kuenea kwa dhambi, haikuikomesha.
Dhambi iliendelea kuenea na kuleta uovu, maumivu, na mateso. Mpaka sasa, tunaweza kuona chanzo na matokeo yake kila mahali. Hebu tuangalie njia tatu ambazo dhambi inatuathiri:
Athari za dhambi

Photo by Chris Gallagher on Unsplash
Dhambi imeleta matokeo kwenye ulimwengu ulioasi, maumivu na mateso. Mateso haya yanaweza kuwa bila utaratibu maalumu au ya sadfa bila sababu ya kimantiki ya moja kwa moja.
Changizo za dhambi katika historia zimetengeneza mazingira ambapo maumivu, maafa na mateso hutokea kila wakati. Matokeo yake ni vita, tamaa, kiburi, rushwa na kuzorota kwa mazingira. Mtu anaweza kuwa alizaliwa kwenye familia yenye unyanyasaji.
Taifa lisilo na hatia linaweza kuvamiwa na nchi jirani.
Ama ungeweza kuishia kwenye ajali mbaya barabarani.
Katika hali hizi zote, yule anayeteseka hajafanya jambo lolote la kujiletea mateso hayo. Yote ni matokeo ya ulimwengu ulioanguka uliofunikwa na dhambi. Mara nyengine, inaweza kuwa ni mashambulizi ya moja kwa moja kutoka kwa ibilisi. Mengine mengi yanafuata.
Shambulizi la kiroho
Bibilia inatukumbusha kuwa katika ulimwengu huu wa dhambi, “kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1 Petro 5:8, NKJV).
Ufunuo 12:12 anaongeza:
“…Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu” (NKJV).
Wakati mwingine, mateso yanaweza kuwa ni shambulizi binafsi kutoka kwake.
Tunaona mfano wa hili katika maisha ya Ayubu ndani ya Biblia, ambaye alipoteza watoto wake na mali zake ndani ya muda mfupi sana (Ayubu 1-2). Kisha, alipoteza afya yake alipokumbwa na vidonda vya maumivu makali mwilini mwake.
Shetani alihusika katika mateso haya yote. Alikuwa akimjaribu Ayubu aone kama Ayubu angemwacha Mungu wakati mambo yote yalipokuwa mabaya maishani mwake (Ayubu 1:9-12).
Mwandishi wa kisa hiki anasisitiza kwamba Ayubu alikuwa mtu mcha Mungu, asiye na hatia (Ayubu 1:1). Na wakati mwingine, wafuasi wa Mungu leo wanaweza pia kukumbana na hali kama hizi za mashambulizi.
Kwa mfano, unaweza kupata ugonjwa wa ghafla, usioelezeka. Au labda, watu wakugeukie kwa sababu ya imani yako. Hali hizi hazitarajiwi na mara nyingi ziko nje ya udhibiti wetu.
Nyakati zingine, hata hivyo, mateso yanaweza kuwa matokeo ya maamuzi yetu binafsi.
Wajibu wetu binafsi
Kwa sababu tunaishi katika ulimwengu wa dhambi, na tuna miegemezo ya kutenda dhambi, wakati mwingine tunafanya maamuzi yanayochangia mateso yetu au kuleta madhara kwetu.
Kwa mfano, kutojali afya ya mwili kunaweza kuchangia ugonjwa. Ama kutelekeza rafiki au mwanafamilia kunaweza kusababisha hisia za chuki na uhusiano kuvunjika.
Bila shaka, Mungu hapendi tuteseke. Lakini mateso yanaweza kuwa matokeo halisi ya maamuzi yetu.
Fikiria kwa mtazamo huu:
Kama wewe ni mzazi, huenda umemwonya mtoto wako asiguse birika la kuchemshia kwenye jiko. Unataka kumlinda mtoto wako.
Lakini ikiwa mtoto wako atachagua kugusa birika hilo?
Mtoto huyo huenda akaungua na kupata maumivu kiasi fulani. Na kama mzazi anayependa, bila shaka utamfariji na kusaidia kutibu jeraha hilo.
Hatimaye, mtoto wako atajifunza somo muhimu: kutokugusa jiko la moto.
Vivyo hivyo, Mungu anatupatia mwongozo na mipaka juu ya namna ya kuishi maisha bora na salama, lakini tunapokwenda kinyume na mipaka hiyo, wakati mwingine tunaweza kujifunza kwa njia iliyo ngumu.
Tunapochagua kulewa na kisha kuendesha gari mahali fulani, tunajiweka katika hatari ya ajali ya gari inayoweza kutudhuru sisi na wengine.
Kama tutajihusisha na tabia za ngono zinazopingana na kanuni za Biblia, tunajiweka katika hatari ya magonjwa yasiyohitajika, hisia zilizochanganyikiwa, au ujauzito usiopangwa.
Hata hivyo, Mungu hataki madhara yatupate.
Dhambi ipo katika ulimwengu wetu kwa sababu tunairuhusu kuingia—kupitia haki ya uchaguzi wetu wa kuijua, Anaruhusu chanzo na matokeo kufuata mkondo wake. Lakini wakati wote, atakuwepo kutufariji na kutuhimiza kwenye njia bora.
Kwa kweli, kile tunachokiamini kuhusu mateso kitaathiri namna tutakavyokabiliana nayo na kupata faraja. Imani zetu zinaweza kutuelekeza kwenye kukata tamaa, au zinaweza kutupatia tumaini. Ndio maana ni muhimu sana kuzingatia kile tunachokiamini kuhusu mateso.
Sehemu ifuatayo itatazama baadhi ya imani za kawaida na kuzitathmini kwa mujibu wa Biblia.
Imani zilizozoeleka kuhusu mateso

Photo by Valerie Sigamani on Unsplash
Mateso mara nyingi hayana maelezo bayana. Hata katika mtazamo wa kibiblia wa dhambi na athari zake, tunaweza bado kukumbana na changamoto ya kuelewa kwa nini sisi au wapendwa wetu tunakabiliwa na ugumu mwingi. Inaweza kuwa rahisi kuanguka katika imani kuhusu mateso ambazo hazikubaliani na Maandiko.
Tutatazama imani tatu muhimu:
- Mateso ni adhabu kwa jambo fulani ulilofanya wewe au jamaa/ mababu zako.
- Mateso ni matokeo ya laana au aina nyingine za uchawi.
- Mateso ni hatima yako au mapenzi ya Mungu kwako.
Hapa ni namna Maandiko yanavyosema kuhusu kila moja ya haya:
Mateso kama adhabu
Wengi wanaamini kwamba mateso ni adhabu ya kiungu kwa kufanya jambo baya au kosa. Katika mtazamo huu, hata kama hujafanya chochote kibaya, mpendwa wako, jamaa, au mababu wanaweza kuwa wamefanya jambo ambalo kwa sasa unalipia.
Inashangaza kwamba, Wayahudi wa wakati wa Yesu pia walikuwa na dhana hii potofu. Wakati Yeye na wanafunzi wake walipokutana na mtu kipofu, wanafunzi walimuuliza:
“….Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?” (Yohana 9:2, NKJV).
Yesu aliweka wazi kwamba jibu haikuwa moja wapo.
Ndio, wakati mwingine tunaweza kukumbana na matokeo asili ya uamuzi (kama tulivyoona katika mfano wa jiko la moto), lakini Mungu hatuadhibu kwa uamuzi huo.
Na kwa hakika hatuadhibu kwa dhambi za wengine. Tunawajibika kila mtu kwa dhambi tunazofanya:
“Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe…..” (Ezekieli 18:20, NKJV).
Sura nzima ya (Ezekieli 18:4-20) inajadili namna ambavyo baba anaweza kuchagua kutenda dhambi, lakini mwana anaweza kuona dhambi ya baba yake na kuchagua kuishi tofauti. Kwa hivyo, mwana hatabeba dhambi ya baba yake.
Hata hivyo, ikiwa tutafanya maamuzi mabaya kama vile mababu zetu au jamaa zetu walivyofanya, tunaweza kukabiliwa na matokeo sawa kwa maamuzi hayo.
Kutoka 20:5-6 inanakili Mungu akizungumza na kusema kwamba Yeye “…nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu” (NKJV).
Tena, tunakabiliwa na matokeo ya mababu zetu au wazazi wetu tunapochagua kufuata nyayo zao. Lakini tunapompenda na kumfuata Mungu, tunapata kuona upendo wake wa uaminifu ukiwa juu yetu.
Aya hizi zinaonyesha wajibu wa kibinafsi kwa maamuzi yetu.
Laana
Imani juu ya laana na uchawi ni ya kawaida katika tamaduni za Kiafrika. Kama anavyosema mchungaji mmoja nchini Nigeria, watu, hata Wakristo, wanaamini kwamba mambo mengi yanaweza kulaaniwa: “familia, ndoa, ardhi, jengo, mahali pa kazi, hata kanisa.”1 Wanaishi katika hofu ya laana hizi ambazo wachawi wanadai wanaweza kuleta kwa watu.2
Msingi wa kibiblia unakubali kwamba uchawi na umizimu ni halisi na hatari.
Hata hivyo, watu wengi hawaelewi jinsi zinavyofanya kazi. Watu katika tamaduni hizi wanaweza kufikiri kwamba wanaweza kutumia uchawi au mizimu kudhibiti mapepo. Hata hivyo, Biblia inafundisha kwamba mapepo ni malaika wa ibilisi—wale waliotupwa duniani pamoja na Shetani (Ufunuo 12:7-9).
Habari njema ni hii, Yesu amewapa wafuasi wake nguvu juu ya mapepo na roho wabaya (Luka 9:1). Hatuhitaji kuogopa nguvu za wachawi kwa sababu Mungu ana nguvu zaidi, na ameahidi kutulinda (Zaburi 91).
Unaweza kujiuliza, kwa hivyo, Kwa nini basi Biblia inazungumzia Mungu akitoa laana?
Laana hizi ni tofauti na laana za kishetani au za kimizimu tunazo fikiria.
Laana ya mwisho ni laana ya dhambi, ambayo ni kifo cha milele. Lakini laana hiyo haina nguvu juu yetu tunapochagua kumfuata Kristo (Wagalatia 3:10-13). Kama mpaji wa uhai, Yesu anatuunganisha tena na Mungu ili tusikue chini ya laana hiyo ya kifo.
Biblia pia inazungumzia dhana ya baraka na laana. Katika muktadha huu, laana sio matokeo ya uchawi bali ni matokeo ya kutotii (Kumbukumbu la Torati 30:19).
Hatima au mapenzi ya Mungu
Mtazamo wa mwisho wa kawaida kuhusu mateso ni kwamba ni hatima yetu au kwamba ni mpango wa Mungu tupitie fulani ya mateso.
Huu mtazamo, hata hivyo, unapingana na mtazamo wa kibiblia wa Mungu mwenye upendo.
Maandiko yanatuonyesha Mungu anayetupenda na amefanya kila kitu kiwezekane—ikiwemo kutoa maisha yake—kutupatia sisi yaliyo bora. Hatupatii mambo mabaya kwa makusudi (Maombolezo 3:33).
Ndio, Anaturuhusu kukabiliana na athari za matokeo ya dhambi na matokeo ya maamuzi yetu binafsi. Anaweza pia kuturuhusu kukutana na mashambulizi ya kiroho, lakini kupitia yote haya, Yeye ni Mungu anayeelewa mateso yetu kwa sababu Yeye mwenyewe ameteseka (Isaya 53:3-6). Alikuja katika dunia hii na kupitia mateso yetu ili aweze kuhusiana nasi na kutusaidia (Waebrania 2:18).
Jifunze kuhusu mtazamo huu wa kibiblia katika sehemu inayofuata.
Biblia inafundisha hivi kuhusu mateso

Photo by Nick Moore on Unsplash
Biblia inafundisha kwamba mateso ni uhalisia wa kuishi katika ulimwengu wenye dhambi, wakati ambapo njia za upendo za Mungu hazifuatwi. Kadri watu wanavyochagua tabia zinazopingana na sheria za Mungu kama vile wizi, uongo, na mauaji (Kutoka 20:3-17), kutakuwa na uwezekano wa mateso kila wakati. Hata hivyo, Biblia pia inatuonyesha kwamba Mungu anaweza kuchukua mateso yetu na kuyageuza kuwa jambo jema (Yakobo 1:2-4).
Bila shaka, Mungu hataki kamwe tupitie mateso. Bali pamoja na mateso ambayo tayari yapo, Anaweza bado kuleta mambo mazuri kutokana nayo.
Zaidi ya hayo, Mungu anapitia mateso pamoja nasi. Alikataliwa na watu wake, alitelekezwa katika nyakati zake ngumu zaidi, alisalitiwa na mmoja wa wafuasi wake, na kisha akadharauliwa, akateswa na kuuawa. Na ni kwa sababu ya maumivu hayo anaweza kutuhurumia, kutufariji na kutupa tumaini la maisha bila maumivu.
Hebu tuchunguze kila moja ya vipengele hivi kwa undani
Mateso yanaweza kuleta mema katika maisha yetu
Katika barua yake, Yakobo anawaambia Wakristo “hesabuni ya kuwa ni furaha tupu” wanapokutana na magumu au kuteseka. Kwa sababu “ mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi” (Yakobo 1:2-3, NKJV). Alikuwa akimaanisha kwamba kuteseka, ambacho kinaonekana kuwa kibaya kwa wakati huo, bado kinaweza kuleta mema katika maisha yetu.
Wakati wa kuandika barua za Agano Jipya, Wakristo katika Ufalme wa Kirumi walikuwa wakikabiliwa na mateso kwa sababu ya imani yao.
Yakobo alitaka wajue kwamba mateso yao hayakuwa bure.
Petro alituma ujumbe kama huo kwa Wakristo waliokuwa wanateswa:
“Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu” (1 Petero 5:9-10, NKJV).
Tena, mema yalitokana na majaribu yao. Na kupitia yote hayo, Kristo alikuwa pale kuwaimarisha, kuwapa nguvu, na kuwasaidia.
Paulo anasema pia:
“Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake”
(Warumi 8:28, NKJV).
Mungu kamwe hachezei mateso yetu. Anataka kuyakomboa ili kweli yawe ya thamani. Kama alivyofanya katika maisha ya Yusufu…
Tazama, Yusufu alipitia aina zote za mateso wakati ndugu zake, kutokana na mioyo yao ya dhambi na wivu, walipomuuza kuwa mtumwa (Mwanzo 37:18-28). Mungu hakusababisha Yusufu kuuzwa, lakini aliruhusu uchaguzi uovu wa wengine kufuata mkondo wao.
Na bado, Mungu hakuutumia vibaya utumwa wa Yusufu nchini Misri. Alimsaidia Yusufu kukua katika uaminifu na hekima hadi Yusufu akawa mtawala wa pili katika mamlaka ya Misri. Kwa sababu ya uwezo wake alioupata kutoka kwa Mungu wa kutafsiri ndoto za Farao na nafasi aliyopata, alisaidia kuokoa taifa zima la Misri na mataifa jirani (ikiwemo familia yake) kutokana na njaa kali. (Tazama Mwanzo 41-45 kwa hadithi.)
Mwishoni mwa maisha yake, badala ya kuwa na chuki kuhusu hali yake ya maisha, Yusufu aliweza kuwaambia ndugu zake:
“Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo” (Mwanzo 50:20, NJKV).
Tunapotazama mateso yetu yaliyopita, nasi tunaweza kuona jinsi Mungu alivyoyageuza kuwa mema. Lakini katikati ya hayo, wakati mwingine jambo bora tunaloweza kufanya ni kukumbuka Yeye yuko pamoja nasi. Yapo mengi zaidi kuhusu hili yanafuata.
Mungu yuko nasi na anateseka pamoja nasi
Mungu wa Biblia hayuko mbali nasi tunapoteseka. Anajua maumivu ya dhambi na athari zake katika ulimwengu huu kwa sababu Yeye mwenyewe ameteseka kutokana na athari hizo.
Kulingana na 2 Wakorintho 5:21, Allifanyika dhambi kwa ajili yetu. Ilikuwa hali ya namna gani kwake Yeye?
Ilikuwa kama kujisikia bila msaada na peke yake akiwa amebeba mzigo mzito (Luka 22:44).
Ilikuwa maumivu makuu na kuomba Mungu aondoe hiyo (Mathayo 26:38-39).
Ilikuwa kama kujisikia hali ya kutisha ya kutengwa na Mungu (Mathayo 27:46).
Isaya 53:4-6 ilitabiri kwamba Yesu kama Mwana wa Mungu angejihusisha na mateso yetu
“Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu;Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote” (NKJV).
Tunapopitia maumivu ya mateso yetu, tunaweza fahamu kwamba Mungu yupo nasi katika hali zetu. Anatupatia tumaini na faraja ndani yake kwa sababu Amepitia hayo.
Pia alipitia hayo ili kufanya ulimwengu bila mateso uwezekane.
Mungu ana mpango wa kukomesha mateso
Mungu amekubali dhambi na mateso kuwepo katika ulimwengu wetu kwa sababu. Anatusaidia kuona kwamba njia zake ni njia za upendo, zilizoundwa kutulinda dhidi ya dhambi na uovu.
Wakati huo huo, Anampa Shetani muda wa kuonyesha asilia yake ili ulimwengu wote uwe na hakika kuhusu uovu wa njia zake.
Hapo ndipo Mungu anaweza kumaliza dhambi kwa haki na kwa usawa.
Ingawa mateso yote tunayokabiliana nayo sasa sio mpango wake, bali ni njia bora zaidi ya kuwa na ulimwengu usio kuwa na mateso. Ni sehemu ya mpango wa Mungu wa kitu bora zaidi.
Ufunuo 21 na 22 inaelezea dunia mpya ambayo siku moja Mungu ataiumba. Sehemu hii inasisitiza kwamba katika ulimwengu huo, “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita” (Ufunuo 21:4, NKJV).
Ahadi hii inatupa tumaini katikati ya mateso yetu.
Ni kwa njia zipi nyingine tunaweza kupata tumaini na faraja?
Jinsi ya kupata tumaini na faraja katika Kristo katikati ya mateso

Photo by Dan Meyers on Unsplash
Tunapokabiliana na mateso, daima ni faraja kujua kwamba hatuko peke yetu, kwamba kuna mtu mwingine anaelewa tunachopitia.
Kristo anatupatia faraja hiyo:
“Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa” (Waebrania 2:18, NKJV).
Tunaweza kumgeukia na kujua Yeye yuko pamoja nasi na anatupa neema, amani, na uponyaji. Wakati mwingine, hiyo inakuja moja kwa moja kupitia kuwa na muda pamoja Naye na Neno Lake. Na nyakati nyingine, hutumia watu.
Hizi ni baadhi ya njia za halisi za kutafuta faraja:
Omba
Tunapoomba, tunaunganishwa na Mungu anayetuelewa sisi na mapambano yetu (Isaya 63:9).
Basi, uombe kitu gani unapojisikia kukata tamaa?
Unaweza usiwe tayari kumshukuru Mungu au kumtukuza. Na huenda ukahisi kwamba kuombea hali yako hakutasaidia.
Lakini maombi yako yanaweza kuwa rahisi kama kumwambia Mungu unachopitia sasa hivi. Mwambie kila kitu kinachokuudhi na kukusumbua. Anaweza kukabiliana nacho.
Yesu alitupa mfano wa hili alipokuwa akiomba kwa uwazi na ukweli kwa Baba Yake huko Gethsemane na msalabani (Mathayo 27:46; Marko 14:32-36). Hakuwa na hofu ya kuwasilisha hisia zake…ambayo inatupeleka kwenye hoja yetu inayofuata.
Jipatie muda wa kuhuzunika
Huzuni ni mwitikio wa kiafya kwa aina yoyote ya hasara ambayo tunaweza kumbana nayo, iwe ni kupoteza mpendwa wetu, kupoteza afya, au kupoteza kitu kingine chochote tulichokithamini.
Mifano ya Biblia ya watu waliokuwa na huzuni inatupa ruhusa ya kuhuzunika, badala ya kuficha tunachopitia au kujifanya hatuna huzuni.
Tafakari kuhusu Zaburi nyingi zinazoonesha huzuni, hasira, au kukata tamaa (Zaburi 22, 42, 109). Kila moja inatukumbusha kwamba njia bora ya kushughulikia huzuni yetu ni kumwambia Mungu kwa uwazi na ukweli.
Katika tamaduni nyingi leo, kuonyesha huzuni hukemewa, lakini tamaduni za Kiyahudi (kuanzia nyakati za Biblia hadi sasa) zina desturi na mila nyingi zinazoruhusu kuonyesha na kukabiliana na huzuni.
Mojawapo ya mila hizo ni keriyah, ambapo mtu hurarua mavazi yake kama ishara ya majonzi makubwa.3 Katika Biblia nzima, watu walipasua mavazi yao na kuvaa nguo za gunia na majivu walipokabiliana na hisia kali (Mwanzo 37:29, Esteri 4:1, Ayubu 1:20). Ingawa huenda hatuombolezi kwa njia hii leo, ni ukumbusho kwetu kwamba ni sawa kuonyesha huzuni tunapokabiliana nayo.
Tafuta msaada wa jamii
Tunapokabiliana na mambo magumu, watu wanao tuzunguka wanaweza kuwa na msaada mkubwa katika kutusaidia kupata uponyaji na kuendelea mbele katika maisha.
Hata hivyo, Mungu alituumba kuishi katika jamii, na anatuhimiza kupitia maneno ya mtume Paulo “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.” (Wagalatia 6:2, NKJV).
Hivyo, ni watu gani unaoweza kuwafikia katika maisha yako? Kuwa wazi kwao kuhusu mapambano yako na jinsi wanavyoweza kukusaidia sasa hivi.
Wakati mwingine, unaweza kuhitaji msaada zaidi ya kile rafiki au mwanafamilia anaweza kutoa. Hapo ndipo inaweza kuwa busara kutafuta ushauri wa kitaalamu au msaada wa afya ya akili. Kufanya hivyo si kosa wala si ubinafsi. Kujali afya za akili zetu ni muhimu kama vile kujali afya za miili yetu, na tunapofanya hivyo, tutakuwa na ufanisi zaidi na baraka kubwa kwa wale wanaotuzunguka.
Jikite katika ahadi za Mungu

Photo by Emmanuel Ikwuegbu on Unsplash
Kusoma na kukariri ahadi za Mungu kunaweza kutupa ujasiri wa kuendelea kusonga mbele wakati maisha yanapokuwa magumu.
Huenda tusipate majibu ya maswali yetu yote kuhusu mateso, lakini ahadi zake zinaweza kutusaidia kuamini wema wake na nguvu zake hata wakati hatuelewi yale tunayopitia.
Hapa kuna ahadi kadhaa ambazo unaweza kuanza nazo:
“Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwamambo yenu” (1 Petro 5:7, NKJV).
“Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele” (2 Wakorintho 4:16-18, NKJV).
“Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33, NKJV).
“Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 4:6-7, NKJV).
Biblia inatusaidia kukabiliana na mateso tukiwa na lengo na tumaini
Mateso yaliingia katika ulimwengu kama matokeo ya dhambi—uvunjaji wa sheria ya Mungu ya upendo —na kadri dhambi inavyokuwepo, yataendelea kuwa sehemu ya maisha yetu.
Kama haya yangekuwa ndiyo kila kitu tunachojua, mtazamo wetu ungekuwa wa kukatisha tamaa.
Lakini Biblia inatupatia ahadi ya tumaini baada ya maisha haya yaliyojaa dhambi. Yesu anakuja kuharibu dhambi na mateso na kutupa makao ambayo tutapata amani na faraja ya milele!
Hadi wakati huo, tunaweza kukabiliana na mateso yetu tukiwa na malengo kwa maisha ya sasa na tumaini kwa ajili ya siku zijazo. Mungu pia ametupa njia za kupata faraja na uponyaji—maombi, jamii, na ahadi katika neno Lake.
Je unahitaji nyenzo zaidi kwaajili ya kukusaidia unapotafuta amani katika nyakati ngumu?
- “How Christians Can Break the Stronghold of a Curse-Informed Worldview,” Christianity Today, Sept. 11, 2023. [↵]
- Ibid. [↵]
- “Death & Bereavement in Judaism: Death and Mourning,” Jewish Virtual Library. [↵]