Ahadi za Biblia Kuhusu Ulinzi

Kuna wakati tunapitia hali za wasiwasi na hofu—tunahofia afya zetu, usalama wetu, changamoto za kifedha, au hata maisha ya wale tunaowapenda.

Ingawa tunaweza kuwashirikisha wengine na kutafuta faraja na matumaini kuwa mambo yatakuwa sawa, kuna wakati inaweza kuwa ngumu kumpata mtu huyo. Na wakati mwingine, faraja ya kibinadamu haitoshi kutupatia tumaini, mwelekeo, au uhakika ambao kwa kweli tunauhitaji.

Haijalishi tuko katika hali gani, Biblia imejaa ahadi kwamba Mungu atakuwa nasi wakati tunapomhitaji.

Hebu tuangalie aya mbalimbali za maandiko ambako tutapata:

Tutaanza na Visa muhimu kutoka kwenye Biblia vinavyoonyesha jinsi Mungu anavyofanya kazi na kuwalinda watu wake.

Visa mbalimbali kuhusu Mungu anavyowalinda watu wake

Ushahidi wa uwezo na shauku ya Mungu ya kuwalinda watu wake unaweza kupatikana katika nyakati za kihistoria zilizoandikwa katika Maandiko. Haikujalisha watu walikuwa na matatizo makubwa kiasi gani. Aliwalinda na kuwasaidia katikati ya njaa, mapigo, magonjwa, maadui wenye nguvu, majanga ya asili, na mengine mengi.

Ulinzi wa Mungu kwa Nuhu na familia yake (Mwanzo 6-8)

Katika sehemu hii ya historia ya biblia, Mungu alitoa onyo kwamba angeiharibu dunia kwa gharika kwa sababu ya dhambi na uovu uliokuwa umeenea na kuifanya dunia kutofaa kwa watu wa Mungu kuishi. Nuhu alisikiliza sauti ya Mungu na kujenga safina huku akiwahubiria watu wengine kwamba gharika ilikuwa inakuja. Mara mvua na gharika ilipoanza na “chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu,” hakukuwa na mahali salama pa kujificha isipokuwa ndani ya safina (Mwanzo 7:11-16, NKJV). Lakini Nuhu na familia yake walikuwa salama katika safina wakilindwa na mkono wa Mungu usioonekana.

Mungu alimlinda Nuhu, hata katika hali ambayo ilionekana kana kwamba haiwezekani. Kwa sababu watu wa wakati huo hawakuwa na dhana yoyote kuhusu safina, Mungu alimpa Nuhu maelekezo sahihi ya kujenga. Na ili kumtia moyo, Mungu alimpa ishara za wakati wa kuingia kwenye safina na wakati uliokuwa salama kutoka.

Ukombozi wa Waisraeli katika Bahari ya Shamu (Kutoka 14)

Wakati wanaondoka Misri wakikimbia kulikwepa jeshi la Farao, wana wa Israeli walijikuta kwenye njia iliyokuwa imezuiliwa na milima kila upande, Bahari ya Shamu mbele yao, na askari wa Farao nyuma yao.

Lakini Mungu alitimiza neno lake alilowaambia kupitia Musa akisema, “Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele” (Kutoka 14:13, NKJV).

Mungu aliwaokoa wana wa Israeli kutoka katika hali hii ngumu kwa kufanya jambo lisilowezekana kwa uwezo wa kibinadamu: kugawanya Bahari ya Shamu ili kuwapa njia ya kupita.

Lakini baada ya wao kuvuka salama upande wa pili, Wamisri waliokuwa wakiwafuatilia walikufa kwa sababu Mungu alifunga Bahari ya Shamu kwa njia ile ile aliyotumia kuifungua kwa Waisraeli. Kile kilichowaletea usalama watu wa Mungu kilikuwa mtego kwa adui zao.

Kama alivyowalinda Waebrania, Mungu atamlinda kila mtu anayemtumaini.

Daudi alindwa dhidi ya njama za Sauli (1 Samweli 23-26)

Baada ya kupakwa mafuta ili awe mfalme anayefuata na kusifiwa na wana wa Israeli, Daudi alijikuta akiwindwa na mfalme mwenye wivu wa wakati huo, Sauli.

Kupitia njia mbalimbali—maonyo ya wakati, uingiliaji wa kimungu, na kwa uongozi wake, Mungu alimlinda Daudi mpaka alipoketi katika kiti cha ufalme. Kwa kweli, “…Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake” (1 Samweli 23:14, NKJV).

Pia Mungu aliubariki urafiki kati ya Daudi na mwana wa mfalme Sauli, Yonathani. Hatimaye, Yonathani aliikuwa tayari kuikabili hasira ya baba yake mfalme kwa kumwambia wazi wazi aache njama zake mbaya dhidi ya Daudi. Wakati Sauli alipoazimia kwa dhati kufanikisha mipango yake ya uovu, Yonathani alimpa Daudi taarifa muhimu, ambayo ilimwezesha kutoroka. Hata Mikali, binti wa Sauli, alikuwa sehemu ya watu waliomsaidia Daudi kutoroka (1 Samweli 19).

Esta na Wayahudi waokolewa dhidi ya Hamani (Esta 3-9)

Wayahudi walikuwa katika hatari ya kuuawa mikononi mwa Hamani, afisa wa mfalme wa ufalme wa Uajemi. Lakini Mungu alingilia kati kwa namna ya ajabu.

Hii ilianza wakati Hamani alipokasirishwa na kitendo cha Mordekai, Myahudi (na baba Mlezi wa Esta) ambaye alikuwa mfanyakazi kwenye lango la ikulu. Hakukubali kusujudu mbele ya Hamani, kwani alipaswa kusujudu katika ibada kwa Mungu pekee. Hivyo Hamani alipanga njama za kumuangamiza yeye na watu wake.

Lakini kupitia maombi ya Mordekai na ujasiri wa binti yake wa kumlea Esther, ambaye alipata kibali cha mfalme na kuwa malkia, Wayahudi waliokolewa na Hamani akaaangamizwa kwa njama zake mwenyewe.

Sheria ya Waamedi ilikataza mtu yoyote Kwenda mbele ya mfalme bila kualikwa . Mtu yeyote aliyethubutu kufanya hivyo angeweza kuishi tu ikiwa mfalme angenyoosha fimbo yake. Katika hatari ya kifo, Esta alikwenda mbele ya mfalme bila mwaliko ili aweze kupata nafasi ya kueleza kwamba chuki ya Hamani ilikuwa dhidi ya watu wake. Nafasi yake na kibali alichopata kwa mfalme kilifanya miujiza hii iwezekane (Esta 4:14), na Hamani aliuawa na mfalme. Na baadaye, Esta akawa malkia na Mordekai akawa waziri mkuu.

Hivyo hata wakati walipokuwa chini ya utawala wa taifa lingine, bado mungu aliwalinda na hata kuwainua wale waliokuwa waaminifu kwake hata mbele ya adhabu au kifo.

Kuangamia kwa jeshi la Senakeribu (2 Wafalme 19:32-37, 2 Mambo ya Nyakati 32:1-23, Isaya 37:33-38)

Wakati wa utawala wa Mfalme Hezekia, Yerusalemu ilitishiwa na Senakeribu, mfalme wa Ashuru—ufalme wenye nguvu zaidi wakati huo.

Mfalme Hezekia alimwelekea Mungu kwa maombi, akimwomba aingilie kati, naye Mungu akamhakikishia kuwa hawatapata madhara. Hivyo, Hezekia akawatia moyo watu wa Yuda.

Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye; kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda” ( 2 Mambo ya Nyakati 32:7-8 , NKJV).

Kwa kujibu maombi, malaika wa Bwana aliwaua askari 185,000 wa Ashuru usiku mmoja, na hivyo akaikomboa Yerusalemu bila hata jeshi la Israeli kupigana.

Mungu anaweza kuwaokoa watu wake kutoka kwa maadui wenye nguvu kwa mbinu zinazopita upeo wa ufahamu wa kibinadamu.

Danieli katika tundu la simba (Danieli 6)

Danieli, kupitia tabia njema na tabia isiyo na lawama, alikuwa amejitengenezea njia na kuwa mfanyakazi wa ikulu katika ufalme uliokuwa unawatawala watu wake.

Bidii, uaminifu, na uadilifu wa Danieli vilimfanya awe wa kwanza kati ya magavana watatu ambao Mfalme Dario aliwaweka kusimamia ufalme wa Umedi na Uajemi. Alipendwa na Dario kuliko maafisa wengine wa mfalme (Danieli 6:3).

Lakini hii iliwafanya maafisa wengine wa ikulu kuwa na wivu.

“Basi, mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshtaki Danieli kwa habari ya mambo ya ufalme.; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danielii huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake’” (Danieli 6:4-5, NKJV).

Hivyo wakamlaghai mfalme ili kupitisha sheria ya kifalme na kuweka sheria kali kwamba yeyote atakayemuomba Mungu au mwanadamu kwa muda wa siku thelathini, isipokuwa kwa Mfalme Dario, atauawa.

Lakini Danieli alibaki mwaminifu kwa Mungu pekee na akaendelea kumuomba waziwazi. Maafisa waliokuwa wamepanga njama ile walimwona akifanya hivi na kuripoti uasi wake wake dhidi ya amri ya mfalme, na Danieli alitupwa katika tundu la simba wenye njaa kama hukumu ya kifo.

Lakini Mungu alimlinda dhidi ya simba. Watu waliona jinsi utii wa Danieli kwa Mungu ulivyozawadiwa. Mfalme alitambua kwamba Danieli alimtumikia Mungu mmoja wa kweli, na hii ikawa ushuhuda katika ufalme wote wa Wamedi na Waajemi.

Yesu awalinda wanafunzi wake dhidi ya dhoruba (Marko 4:35-41)

Yesu na wanafunzi wake walikuwa kwenye mashua ya uvuvi kwenye Bahari ya Galilaya walipokumbana na dhoruba kali iliyotishia maisha yao. Wote walikuwa na hofu na walijiuliza kwa nini Yesu alikuwa amelala wakati mashua yao ipo hatarini.

Akiamka kutoka usingizini, Yesu alisimama na kuukemea kwa sauti upepo na kuyaamuru maji yatulie na kuleta amani (Marko 4:39).

Wanafunzi walijifunza kwamba hata pale mambo yanapoonekana kama hayaendi sawa, ulinzi wa Mungu daima upo na tunaweza kuzitegemea njia zake.

Paulo aokolewa kutoka katika ajali ya meli (Matendo 27)

Katika safari yake kuelekea Rumi, Ajali ya meli ilitishia Maisha ya mtume paulo na wengine waliokuwa kwenye meli. Walikabiliwa na hatari ya kujeruhiwa na mateso ya njaa, na vitu vyao vingi vilitupwa baharini wakati wa dhoruba. Lakini kabla ya tukio hilo, Paulo aliwatia moyo wote kwamba kila kitu kitakuwa sawa kupitia maneno haya ya kutia moyo:

“Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe'” (Matendo 27:23-24, NKJV).

Uhakika wa Paulo katika ulinzi wa Mungu, ulitosha kutangaza kwamba wangefika salama pwani, uliwapa tumaini watu wote. Wakati meli ilipovunjika vibaya, kila mtu aliyekuwa ndani alitafuta kuogelea pwani, lakini askari waliamuru kuwa wafungwa wote wauawe, wakihofia kwamba wangeweza kutoroka. Lakini Paulo alipata kibali kwa jemadari ambaye alitaka kumuokoa Paulo na akuzuia wafungwa wasiuawe, na Kila mtu alifanikiwa kufika nchi kavu (Matendo 27:41-44).

Mungu anapokuwa na mpango, hakuna chochote ambacho wanadamu wanaweza kufanya kumzuia.

Aya za Biblia zinazohusu ulinzi

Ili kutusaidia kuelewa zaidi kuhusu namna Mungu anavyotulinda, hebu tuangalie aya kadhaa zinazotuhakikishia nguvu za Mungu na shauku Yake ya kutuongoza. aya hizi zina umuhimu katika nyakati tofauti tofauti tunzaoweza kukutana nazo katika maisha , kama vile:

  • Ulinzi dhidi ya maadui au wapinzani
  • Ulinzi dhidi ya kifo
  • Ulinzi dhidi ya shambulio la kimwili
  • Ulinzi dhidi ya shambulio la kiroho au uovu
  • Ulinzi dhidi ya msongo wa kihisia
  • Ulinzi katika shida
  • Ulinzi dhidi ya majanga ya asili au maafa

(Aya zote zimetolewa kutoka katika toleo la Biblia la New King James).

Ulinzi dhidi ya maadui

  • Kumbukumbu la Torati 31:6
    “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”
    Maelezo: Uwepo wa Mungu usiotikisika na ulinzi wake utakuongoza unapowakabili maadui zako.
  • Zaburi 9:3
    “Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako.”
    Maelezo: Uwepo wa Bwana mara nyingi unatosha kuwaangamiza maadui zetu wakubwa zaidi.
  • Isaya 54:17
    “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.”
    Maelezo: Aya hizi zinatoa ahadi ya usalama na ulinzi dhidi ya maadui na watu wanaokusudia kutudhuru. Hakuna yeyote anayeweza kuinuka dhidi ya watoto wa Mungu na kushinda.
  • Warumi 8:31
    “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”
    Maelezo: Tukiwa na msaada kutoka kwa Mungu, hakuna adui anayeweza kushinda. Ulinzi wa Mungu unatuhakikishia ushindi dhidi ya adui yeyote.

Ulinzi dhidi ya kifo

  • 1 Wakorintho 15:26
    “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.”
    Maelezo: Katika mwisho wa dahari, Mungu atatu kinga dhidi ya kifo pia

Ulinzi dhidi ya shambulio la kimwili

  • Zaburi 34:7
    “Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.”
    Maelezo: Mungu hutuzingira kwa upendo na ulinzi wake.
  • Isaiah 41:10
    “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
    Maelezo: Mungu anawatia moyo watu wake kwamba uwepo wake ni wa kudumu. Yeye hutoa nguvu, msaada, na ulinzi, akiondoa hofu na wasiwasi.
  • Methali 18:10
    “Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama’’
    Maelezo: Jina la Mungu huwakilisha tabia na uwezo wake. Kwa wenye haki, kumwita Mungu hupata mahali salama pa kukimbilia, kama ngome imara ikiwalinda dhidi ya hatari.
  • Nahumu 1:7
    “BWANA ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao.”
    Maelezo: Wale wanaomtumaini Mungu aliyejuu watakuwa salama katika siku ya taabu.

Ulinzi dhidi ya uovu au shambulio la kiroho

  • Waefeso 6:11
    “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.”
    Maelezo: Unaweza kupigana vita ya kiroho kwa kutumia silha za kiungu peke yake, ambazo hupatikana kupitia uhusiano na Mungu.
  • 2 Wathesalonike 3:3
    “Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.”
    Maelezo: Ikiwa tutamwendea Mungu na kukubali ulinzi wake, atatulinda dhidi ya nguvu za Shetani.

Ulinzi dhidi ya msongo wa kihisia

  • Wafilipi 4:6-7
    “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
    Maelezo: Badala ya kuwa na wasiwasi,wale wanaomwamini wanaalikwa kuomba, wakiamini kwamba amani ya Mungu itawalinda wasishindwe kabisa na yale yanayowakabili.

Ulinzi katika shida

  • Zaburi 23:1-3
    “BWANA ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.”
    Maelezo: Bwana ni kama mchungaji anayejali watu wake. Wale wanaomwamini wanaweza kumtegemea kwa ulinzi katika shida za maisha na kwa ajili ya kuwatimizia mahitaji yao.

Ulinzi dhidi ya maafa au majanga ya asili

  • Zaburi 91:1-2
    “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.’’
    Maelezo: Ulinzi wa Bwana kwa wale wanaobaki katika ushirika wa karibu naye ni wa uhakika.
  • Zaburi 57:1
    “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.”
    Maelezo: Tunaweza kupata katika Mungu mahali salama tunapowindwa na majanga ya asili.
  • Zaburi 46:1
    “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.”
    Maelezo: Aya hii inathibitisha kwamba Mungu ni ngome salama na chanzo cha nguvukatika nyakati za shida, akitoa msaada wa kudumu na wa kutegemewa kwa watu wake.

Maandiko zaidi kuhusu ulinzi

Wakati Biblia imejaa maagizo yanayotuandaa kwaajili ufalme wa mbinguni, maandiko mengi yamekusudiwa kutuhudumia katika maisha yetu ya sasa. Kwa mfano, kitabu cha Zaburi, kimejaa nyimbo za ukombozi.

Unaweza kupata maandiko zaidi kuhusu ulinzi katika Biblia, haswa katika kitabu cha Zaburi. Hususan, Zaburi ya 3, Zaburi ya 18, Zaburi ya 32, Zaburi ya 16, Zaburi ya 121, Zaburi ya 119, Zaburi ya 27, na Zaburi ya 138 zimejaa maneno yanayotia moyo kuhusu nguvu za Mungu na huduma Yake kwetu.

Kudai ahadi hizi katika maisha yetu

Mungu habadiliki (Waebrania 13:8). Hivyo kama alivyoweza kuwalinda watu wengine katika Biblia, bado anatoa ahadi hizo kwetu leo. Tuko salama tunapojitoa kwaajili ya huduma ya Mungu badala ya kuwategemea wanadamu wengine au uwezo wetu binafsi.

Hakuna jambo linalotunyima amani ambalo ni dogo kiasi cha Mungu kulipuuuza au ambalo ni kubwa sana kwake kushughulikia.

Ingawa Mungu hatuhakikishii kwamba hatutakutana na hatari, pia anatufahamisha kwamba ana uwezo wa kufanya jambo lolote, na Yeye ni mwenye nguvu zaidi ya kitu chochote, hivyo ni Yeye pekee anayestahili kuwa Mlinzi wetu Mkuu na ikiwa anamjali hata shomoro aangukaye, anatujali na hawezi kutuacha kamwe.

Namna Mungu anavyowatendea watoto wake waaminifu katika historia unabakia kuwa faraja kwetu kwamba tunaweza kupata usalama ndani Yake katika wakati wa shida.

Hivyo, haijalishi unapitia nini sasa, usiogope maana Bwana atakutunza. Mungu yule yule aliyewalinda watu katika Biblia anakupatia ulinzi wake. Unahitaji tu kuupokea.

Video juu ya ahadi za Biblia kuhusu ulinzi

Muhtasari: Mchungaji Walter Leonard Pearson Jnr. anakuletea hubiri lenye nguvu namna Mungu anavyowalinfa watu wake wanaomwamini. Anatumia kisa cha Esta na Mordekai na mipango ambayo Hamani alikuwa nayo dhidi ya Wayahudi katika Shushan kuonyesha ulinzi wa Mungu juu ya watu wake. Mungu alizipinga njama ovu za Hamani na kuwaokoa watu wake.

Mada na aya hukusanywa kutoka nyenzo mbalimbali na kupitiwa na timu yetu. Ikiwa aya au mada haifai au haipo, tafadhali wasiliana nasi. Maandiko yamechukuliwa kutoka Toleo la New King James®. Hakimiliki © 1982 na Thomas Nelson. Limetumika kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa.

Jiunge na mazungumzo

Hapa ndipo unaweza kutoa maoni yako kuhusu mada hii. Shiriki mawazo yako kuhusu ahadi za Biblia zinazohusu ulinzi.

Tafadhali soma Sera Yetu ya Maoni.

Pin It on Pinterest

Share This