Ahadi za Ajabu za Biblia Kuhusu Uponyaji
Labda wewe au mwana familia umekuwa ukikabiliana na ugonjwa au jeraha ambalo linaonekana haliwezi kuondoka kamwe. Huenda unakabiliana na sonona au wasiwasi na inaonekana kana kwamba hakuna kinacho saidia. Wakati mwingine, mapambano ya kiakili yanaweza hata kuwa katika kiwango cha kiroho.
Lakini kumbuka hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Anataka kutuletea uponyaji na tumaini katika maeneo haya yote, kama vile alivyowaletea watu uponyaji katika Biblia.
Uponyaji ni mchakato wa kufanywa upya katika afya unaoondoa maumivu, huzuni, na udhaifu. Pia huturejeshea furaha yetu na kutupa nafasi mpya ya kuishi.
Yawezekana unakabiliana na magonjwa, majeraha, maumivu ya moyo, kujisikia mbali na Mungu, au changamoto binafsi, lakini neno la Mungu (kama vile Zaburi 107:20) linatukumbusha kwamba Yeye yuko tayari kutuponya na kuturejesha bila kujali tunakabiliana na nini.
Unapoitafuta faraja, tumia muda wako katika ahadi za Biblia za uponyaji zinazoweza kukutia moyo. Tafakari kuhusu mifano mbalimbali ya namna Mungu alivyogusa maisha na kuleta uponyaji kwa wale wanaohitaji kote katika historia.
Katika makala hii tutaangalia:
Mifano ya uponyaji katika Biblia

Photo by Aaron Burden on Unsplash
Biblia imejaa uzoefu wa kushangaza wa uponyaji, msaada, na kutiwa moyo.
Kupitia maendeleo katika matibabu na ufahamu zaidi kuhusu maisha yenye afya, tumefanya maendeleo makubwa katika kushinda changamoto mbalimbali za kiafya. Hata hivyo, bado tunakabiliwa na vikwazo katika maeneo mengine vinavyotufanya tuendelee kutafuta suluhisho. Ndio maana Mungu daima anatualika kuleta matatizo yetu kwake. Kile kinachonekana kuwa hakiwezekani kwetu kinawezekana katika Yeye.
Kwa mfano, wakati gari lako linapoharibika na unalipeleka kwa fundi, unamwamini mtu anayeelewa namna linavyofanya kazi. Vivyo hivyo, tunapokuwa wagonjwa, tumevunjika moyo, na kukata tamaa, tunaweza kumwamini Mungu, Fundi Mkuu, aliyetuumba (Mwanzo 1:26). Ana nguvu na hekima ya kutengeneza, kurejesha, na kufufua, akitufanya kuwa kamili tena kwa namna tusiyoweza kufikiria.
Tunajua tunaweza kumwamini Mungu kutusaidia kwa sababu tuna ushahidi wa namna alivyowasaidia watu wenye matatizo ya kiafya walipokuja Kwake katika Biblia. Hebu tuangalie baadhi ya mifano hii.
Mungu anamwinua Eliya aliyekata tamaa (1 Wafalme 19)
Nabii Eliya anatangaza kwa mafanikio utawala wa Mungu wakati wa ibada ya sanamu iliyoshamiri na tabia mbaya. Katika Mlima Karmeli, Anawapa fursa wapinzani wake kushuhudia ni nani Mungu wa kweli. Hata hivyo, baada ya hapo, aliangukia katika huzuni. Hili linaweza kutokea kwa watu hata baada ya uzoefu bora kabisa.
Hata hivyo baada ya kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Malkia Yezebeli aliyetishia uhai wake, Eliya alipitia hali ya kuvunjika moyo na kukata tamaa. Akijisikia uchovu na kuachwa peke yake, alikimbilia nyikani, hata akatamani kufa. Hata hivyo, Mungu anamwonyesha Eliya kwamba bado yuko pamoja naye. Anampa nafasi ya kupumzika, anampa chakula, na kumwambia kuwa kamwe hayuko peke yake.
Kama Eliya, tunaweza kupata faraja katika ukweli kwamba bila kujali changamoto tunazopitia sasa, Mungu yuko karibu nasi, tayari kutuinua, kututia moyo, na kutusaidia.
Mtu aliyewekwa huru dhidi ya kupagawa na pepo (Marko 5)
Mtu huyu alikuwa ameelemewa na mapepo (malaika walioasi) ambayo yanatuumiza na kututenga na Mungu. Alikuwa na mapepo mengi yaliyomtesa. Alitengwa na watu wake, ikimaanisha kuwa alilazimika kuishi kati ya makaburi, katika upweke, haikuwezekana kumfunga hata kwa minyororo au pingu. Maisha yake yalijawa mateso, vurugu, na kukata tamaa.
Lakini wakati Yesu alipofika kwenye eneo hilo, kila kitu kilibadilika. Kwa amri moja tu, aliyafukuza mapepo kutoka kwa mtu huyo, akamweka huru na kumrejeshea akili yake ya kawaida.
Kisa hiki kinatukumbusha kwa nguvu kwamba haijalishi tumepotea kiasi gani, tumevunjika moyo au tuko mbali na Mungu kiasi gani, Anaweza kubadilisha maisha yetu na kutuweka huru dhidi ya mapepo, dhambi, na majaribu. Yuko tayari kuondoa kizuizi chochote kinachotufanya tushindwe kumfikia. Anataka tuwe huru kutoka katika mambo haya.
Mwanamke aliyepata uponyaji baada ya kutokwa na damu kwa miaka 12 (Luka 8:40-48, Mathayo 9:18-26)
Hapa tunapata kisa cha kusikitisha cha mwanamke ambaye alipambana na tatizo la damu kwa miaka 12. Baada ya kukutana na madaktari wengi na kutumia pesa zake zote, hakupata uponyaji, bali aliachwa akiwa amekata tamaa na kukosa matumaini.
Aliposikia kwamba Yesu alikuwa karibu, aliamini kuwa kugusa vazi lake kungemponya. Na kweli, alipogusa pindo la vazi lake, kutokwa na damu kwake kulikoma mara moja na akapata uponyaji.
Kisa hiki kinatuonyesha jinsi imani ilivyo na nguvu, jinsi Kristo alivyo na upendo, na jinsi anavyoweza kutuponya na kuturejesha, bila kujali jinsi hali yetu ni ya kukatisha tamaa kiasi gani.
Tumeona jinsi Bwana daima anavyofurahia kutupatia uponyaji. Kama ilivyokuwa zamani, tunaweza kupata uponyaji ikiwa tutamwendea leo na kusalimisha mateso na mizigo yetu. Hebu tuangalie baadhi ya maandiko yenye nguvu ya uponyaji.
Aya za Biblia kuhusu uponyaji
Biblia inafundisha kwamba Mungu ni mponyaji. Ahadi zake za uponyaji zimejaa katika maandiko, zikionyesha upendo na nguvu yake ya kufanya upya.
Unapojisikia mgonjwa, mchovu, na mwenye wasiwasi, na unapojisikia kuwa huwezi kuendelea, Yesu anasema, “Njoo kwangu” (Mathayo 11:28). Anahidi kuupa mwili na roho yako iliiyochoka pumziko, faraja, na uponyaji.
Maandiko yafuatayo kuhusu uponyaji yanatukumbusha kuhusu upendo wa Mungu na hamu yake ya kuturejesha kikamilifu na uaminifu wake katika kuleta uponyaji:
1. Kutoka 15:26
“akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.”
Melezo: Mungu anajali kuhusu afya zetu, za kimwili na kiroho. Tunaweza kupata amani na uponyaji wake kama ilivyokuwa Waisraeli . Tutaisikia faraja yake tunapomkaribia, kusalimisha matatizo yetu kwake, na kuamini uangalizi na uongozi wake.
2. Zaburi 30:2
“Ee BWANA, Mungu wangu,Nalikulilia ukaniponya.”
Maelezo: Kuna nyakati katika maisha ambapo tunajisikia kulemewa kabisa na ugonjwa wa kimwili, mapambano ya kihisia, au hali ngumu. Tunapojisikia kama hakuna mtu anayeona kile tunachopitia, Mungu hutuona, hutusikia, na hutujibu. Mungu hatupuuzi au kutuacha tuteseke peke yetu. Hata kama hakuna uponyaji wa haraka unaofanyika, tunaweza kumwamini Mungu atatutunza na kutupa kile tunachohitaji.
3. Zaburi 34:19
“Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini BWANA humponya nayo yote.”
Maelezo: Haijalishi sisi ni nani, tunaamini nini, au tumefanya nini, sote tunakutana na mambo mabaya kwa sababu tunaishi katika ulimwengu ulioharibiwa na dhambi. Ingawa tunakutana na changamoto nyingi, hatuko peke yetu. Haijalishi safari ni ngumu kiasi gani, Mungu hataki tuhangaike, ni shauku yake kutuokoa. Anataka kutupa maisha yenye kuridhisha.
Anatupa nguvu na neema Yake ili kuvumilia hali zetu. Pia anatuhakikishia kwamba siku moja tutakuwa katika ulimwengu ambapo hatuteseka tena.
4. Zaburi 41:3
“BWANA atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.”
Maelezo: Akiwa mgonjwa na kitandani, Daudi anatukumbusha kwamba neema ya Mungu inatosha (1 Wakorintho 12:9). Yeye yupo sikuzote ili kututia moyo, kutuinua, na kutupa nguvu za kuvumilia hali yetu.
5. Zaburi 103:1-3
“Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,”
Maelezo: Tunaishi katika ulimwengu unaoteseka kutokana na madhara ya dhambi. Tunajaribu kutenda mema lakini bado tunateseka kutokana na madhara ya dhambi (katika ulimwengu au watu wanaotuzunguka). Lakini habari njema ni kwamba, Mungu anaweza kuponya maumivu yetu na kushughulikia chanzo cha maumivu yetu—dhambi katika ulimwengu na asili zetu za kibinadamu.
6. Isaya 41:10
“usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Maelezo: Wakati tunapougua au kukabiliana na changamoto, hofu huingia tunapokutana na kukosa uhakika kuhusu afya yetu. Hata hivyo, hatuhitaji kuogopa hata wakati mambo yanapoonekana kuwa magumu sana kwa sababu hatuko peke yetu. Uwepo wa Mungu utatufariji na kututia nguvu tunapokata tamaa na kujisikia dhaifu.
7. Isaya 57:18
“Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.”
Maelezo: Kama ilivyokuwa kwa Israeli, Mungu anataka kumpa amani kila mtu . Hata wale ambao wametenda dhambi na kumuumiza lakini waovu hawawezi kukubali amani anayotoa kwa sababu hawampokei—wanashikilia dhambi zao na matatizo na hivyo wanashindwa. Hata hivyo, tunaposikiliza maonyo kutoka kwa Mungu, Yeye hutuponya na kutufariji.
8. Yeremia 17:14
“Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.”
Maelezo: Tunakumbana na nyakati ambazo hutuacha tukiwa na uhitaji wa uponyaji, urejeshwaji, na mtu ambaye anaweza kutuokoa kutokana na mapambano yetu. Aya hii ya Biblia ni ombi ambalo wengi wetu tunaweza kulielewa tunapojikuta kwenye njia panda, tukitafuta tumaini na kufanywa upya.
9. Yeremia 30:17
“Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.”
Maelezo: Tunaweza kujisikia kama tumesahaulika au kuachwa na kana kwamba hakuna tumaini la kupona. Katika nyakati kama hizo, Mungu anatupatia ahadi ya faraja kwamba ataturejeshea afya.
10. Mathayo 4:23
“Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.”
Maelezo: Wakati Kristo Yesu alikuwa hapa duniani, hakuna ugonjwa aliokutana nao uliokuwa nje ya uwezo wake wa kuponya. Unaweza kuwa unakabiliwa na changamoto zisizowezekana, jipe moyo kwani hakuna jambo gumu kwa Yesu.
11. Waebrania 4:15
“Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”
Maelezo: Kristo anaelewa udhaifu wetu wote. Daima Yeye hutuvumilia na tunaweza kumkaribia kwa ujasiri pamoja na mahitaji yetu yote.
12. Yakobo 5:13-15
“Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. ”
Maelezo: Tunaweza kuja mbele za Mungu kwa ajili ya msamaha na urejeshwaji wa kiroho na pia uponyaji wa kimwili au kiakili. Yeye ndiye chanzo kikuu cha uponyaji, baada ya yote – kimwili, kiakili, na kiroho. Na hatuhitaji kusubiri kumwita Mungu wakati wa saa za kazi! Tunaweza kuja Kwake sisi wenyewe, tukiomba uponyaji wakati wowote, mahali popote. Maombi yana nguvu zaidi wakati Wakristo wanapokusanyika ili kuomba uponyaji kwa niaba ya wanaoteseka.
Tunaweza pia kuinua roho zetu tukimsifu Bwana na kuimba Zaburi (Zaburi 147:1), tukitumaini ukweli kwamba anafurahia kutuponya.
Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kuponya (Luka 5:17)

Photo by Tara Winstead
Tumeangalia uthibitisho wa uponyaji wa Mungu katika Biblia na tunaweza kutiwa moyo leo kwa kuangalia ahadi za Mungu za uponyaji.
Kumbukumbu la Torati 7:15 linatuambia kwamba Mungu anataka kuondoa matatizo yetu yote.
Tunapojisalimisha kwa Mungu, tukitegemea nguvu Zake (Wafilipi 4:13), Anatuahidi afya inayoridhisha.
Sote tunatamani uponyaji. Habari njema ni kwamba uponyaji siyo tu kwa ajili ya wachache wenye bahati bali unapatikana kwa wote. Haijalishi ukubwa wa ugonjwa au maumivu yetu, Yesu Mwenye haki (Malaki 4:2), yuko upande wetu daima.
Anaweza asituponye mara moja au kwa njia tunayoitarajia, lakini atatusaidia kustahimili chochote tunachokabiliana nacho.
Kristo anaelewa maumivu yetu. Alijeruhiwa na kujeruhiwa kwa makosa yetu. Alikubali maumivu na mateso ambayo yangepaswa kuwa yetu, na kwa majeraha yake, tumeponywa (Isaya 53:5, 1 Petro 2:24).
Leo Anatuaalika sote kukumbatia ahadi hizi zinazobadilisha maisha na kuziingiza katika maisha yetu ya kila siku kwa:
- Kudai ahadi za uponyaji katika maombi
- Kujifunza mada ya uponyaji katika Biblia
- Kuwa na Ibada maalum kwa ajili ya uponyaji
- Kukutana na waumini wenzetu kuomba kwa ajili ya maswala ya afya
- Kuimba zaburi na nyimbo za sifa
Uzuri ni kwamba uponyaji ambao Yesu anautoa hauna madhara mabaya, hakuna bili zinazohusishwa, na hakuna tarehe ya kuchakaa. Tunapotafakari ahadi hizi, Hebu zitupatie tumaini, amani, na uponyaji unaopatikana katika Kristo.
Sasa, hebu tuchukue muda kutazama mkusanyiko wa ahadi za Biblia zinazoinua. Imewasilishwa katika muundo wa video nzuri ikiwa na muziki tulivu na mazingira ya asili, video hii inakutia moyo na kuinua roho yako katika nyakati ngumu.
Video ya maandiko ya uponyaji
Ahadi za Mungu za uponyaji na faraja – Masaa 10 ya kujikita katika Neno la Mungu
Zaidi ya hayo, tunakualika kwa moyo mkunjufu ujiunge na mazungumzo na kushiriki changamoto na uzoefu wako wa kiafya. Unaweza pia kushiriki namna ya kupata faraja tunaposafiri kuelekea uponyaji pamoja. Sauti yako ni muhimu, na tuko hapa kusikiliza kwa moyo mkunjufu.
Sehemu ya maoni
Ikiwa makala hii imekuwa msaada kwako na ungependa kushiriki mawazo yako na uzoefu kuhusu ahadi za Biblia kuhusu uponyaji, jisikie huru kushiriki tafakari na maswali yako nasi. Tungependa kusikia mtazamo wako na namna mafundisho haya yanavyokugusa.