Je, naweza kujua Siku zijazo?
Daima mwanadamu amekuwa na shauku ya kujua mambo yajayo. Tunatamani kujua yale yanayokuja mbele yetu, iwe ni kuhusu kazi zetu, mahusiano, afya, au hatima ya ulimwengu. Watu wengi wanatafuta majibu, wakitafuta mwongozo kupitia njia mbalimbali—baadhi ni za kuaminika, nyingine ni njia za udanganyifu.
Lakini je, tunaweza kujua ya kesho? Ingawa hatuwezi kutabiri kila kitu kwa undani, tunaweza kuishi kwa ujasiri na matumaini tunapoamini katika chanzo cha kuaminika.
Mwongozo huu utaangazia:
- Kwa nini watu wanatafuta kujua kuhusu siku zijazo.
- Nini Biblia inasema kuhusu siku zijazo
- Namna Mungu alivyofunua mambo yajayo tangu zamani
- Njia zinazofaa katika kujua mambo yajayo
- Mbinu za udanganyifu zinazopaswa kuepukwa
- Ni nini ambacho kesho imebeba
Tuanze kwa kujifunza kwa nini watu wanatamani kujua kuhusu mambo yajayo.
Kwa nini watu wanatamani kuyajua mambo ya siku zijazo?
Watu mara nyingi wanataka kujua manbo ya siku zijazo kwa sababu ya kukosa uhakika, hofu, au udadisi. Baadhi ya sababu za kawaida ni pamoja na:
- Kutafuta utulivu na usalama: Maisha yamejaa mambo mengi tusiyoyajua, na kujua mambo yajayo hufanya watu kujisikia kuwa wamejiandaa na wana utulivu.
- Kupunguza wasiwasi katika maamuzi: Maamuzi makubwa kama vile kubadilisha kazi, ndoa, na miradi ya kifedha yanaweza kuonekana kuwa magumu. Watu hutamani kupata uthibitisho kwamba wanafanya maamuzi sahihi.
- Imani za kitamaduni na kidini: Jamii nyingi zina desturi za zamani na mazoea ya kiroho yanayohusiana na utabiri wa siku zijazo.
- Udadisi na kuvutiwa: Baadhi ya watu huvutiwa tu na mambo yajayo wanaweza kuwa wanatafuta ujuzi mpya binafsi au kwa ajili tu ya kujifurahisha.
Wakati shauku ya kujua mambo yajayo ni ya kawaida, ni muhimu kutafuta ukweli kutoka katika nyenzo za kuaminika.
Hebu tujifunze kile Biblia inachosema kuhusu siku zijazo.
Nini Biblia inasema kuhusu kujua siku zijazo

Photo by Luis Quintero
Biblia inafundisha kwamba ni Mungu pekee anayejua mambo yajayo kikamilifu. Yeye ndiye muumbaji na mtunzaji wa vitu vyote, na anatangaza:
“Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado… ” (Isaya 46:9-10, NKJV).
Mungu anafahamu mpangilio wote wa historia, na ameonyesha baadhi ya mambo yajayo kupitia Neno Lake. Hata hivyo, lengo Lake siyo kumridhisha mwanadamu bali kutuwezesha kuamini katika uangalizi Wake na kuishi kwa hekima.
Hebu tuangalie namna Mungu alivyofunua mambo yajayo tangu zamani.
Namna Mungu alivyofunua mambo yajayo
Katika historia yote, Mungu amekuwa akiweka wazi siku zijazo kupitia unabii, njozi, maono, na jumbe zilizoletwa na malaika. Hapa kuna baadhi ya mifano:
1. Unabii
Unabii wa biblia ndiyo njia iliyozoeleka zaidi ambayo Mungu ameitumia kuwajulisha wandamu kuhusu mambo yajayo. Kwa mfano:
- Biblia ilitabiri kuinuka na kuanguka kwa falme kuu (Babeli, Umedi na Uajemi, Ugiriki, na Rumi) katika kitabu cha Danieli 2 na 7.
- Zaidi ya nabii 125 kuhusu Yesu Kristo zilitimia katika maisha Yake, ikiwa ni pamoja na kuzaliwa Kwake, huduma, kifo, na ufufuo wake.
- Biblia inatabiri kupotoka kwa maadili katika siku za mwisho (2 Timotheo 3:1-5), unabii ambao umetimia kabisa katika ulimwengu wetu wa sasa.
Unabii huu uliotimia huthibitisha kwamba Neno la Mungu ni sahihi na la kuaminika.
2. Njozi na maono
Mungu mara nyingine alitumia njozi na maono ili kufunua mambo yajayo kwa watu aliowachagua kwa ajili ya kusudi muhimu.
Baadhi ya mifano ni pamoja na:
- Njozi za Yusufu kuhusu yeye kuwa mtawala wa baadaye (Mwanzo 37:5-11).
- Njozi ya Farao kuhusu miaka ya njaa (Mwanzo 41).
- Njozi ya Nebukadneza kuhusu kuinuka na kuanguka kwa falme za ulimwengu (Danieli 2).
Ingawa Mungu bado anaweza kuwasiliana kupitia njozi, Biblia hutuonya kuwa si njozi zote hutoka kwa Mungu.Ili njozi hizo ziwe njozi za kuaminika lazima ziendane na Maandiko.
3. Kutembelewa na malaika
Mungu amekuwa akiwatuma malaika kuleta habari ya mambo yajayo. Baadhi ya mifano ni pamoja na:
- Malaika alitabiri kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji (Luka 1:13-17).
- Malaika walimuonya Lutu juu ya kuharibiwa kwa Sodoma (Mwanzo 19:1-29).
- Malaika alimwambia Mariamu kuwa atamzaa Yesu (Luka 1:26-38).
Ingawa Mungu anaweza kutumia malaika, Biblia pia inaonya kwamba kuna pepo wachafu pia. Hivyo ufunuo wowote unapaswa kupimwa kwa mujibu wa Maandiko (Isaya 8:20).
4. Uongozi wa Roho Mtakatifu
Yesu aliahidi kwamba Roho Mtakatifu angewaongoza waamini katika kweli (Yohana 16:13). Kupitia Roho Mtakatifu, tunaweza kupata hekima, ufahamu, na faraja kuhusu siku zijazo.
Kwa kuwa Mungu ametupa njia za kuaminika za kuelewa mambo yajayo, Tunapaswa pia kuzitambua na kuziepuka njia zote za udanganyifu.
Njia za udanganyifu ambazo watu hujaribu kuzitumia kujua mambo yajayo
Watu wengi hugeukia mbinu zisizoaminika na hata ambazo ni hatari katika kutabiri mambo yajayo. Baadhi ya mbinu za udanganyifu ambazo zimezoeleka ni pamoja na:
- Astrologia na utabiri wa nyota: Kujaribu kutabiri matukio ya maisha kulingana na mpangilio wa nyota na sayari.
- Bahati nasibu na utabiri: Kuwaendea watu wanaodai kuwa na ufahamu wa kiroho kuhusu siku zijazo.
- Uchawi na kupiga ramli: Kushiriki katika matambiko, ramli, au shughuli za kimizimu ili kujua au kubadilisha matukio yajayo.
- Kuongea na wafu (mizimu): Kutafuta ufahamu wa kiroho kutoka kwa mizimu au mababu, biblia inatuonya juu ya jambo hili (Kumbukumbu la Torati 18:10-12).
Mbinu hizi sio za kutegemewa na zinaweza kuongoza watu mbali na mapenzi ya Mungu makamilifu na yenye upendo. Badala ya kutafuta ubashiri wa wanadamu, ni kwa faida yetu wenyewe kuigeukia hekima ya Mungu.
Njia zifaazo katika kujua mambo yajayo

Photo by Tima Miroshnichenko
Badala kuziendea mbinu za uongo, bila kujali ni kiasi gani zinavutia, hapa kuna njia ambazo Biblia inapendekeza kwa ajili ya kujua mambo yajayo:
1. Tafuta mwongozo kupitia maombi na kujifunza Maandiko
Biblia imejaa hekima kuhusu namna ya kukabiliana na hali ya kukosa uhakika katika maisha. Mungu anatualika kumtafuta:
“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu, usiyoyajua” (Yeremia 33:3, NKJV).
Maombi hutupa fursa ya kueleza hofu zetu na wasiwasi wetu kwa Mungu na hutusaidia kuamini katika mpango wake mkuu na kufanya maamuzi yenye busara, hata wakati siku zijazo zinapokuwa zimefichwa kwetu.
2. Amini katika wakati wa Mungu na mpango wake
Tunaweza tusijue kila kitu kuhusu siku zijazo, lakini tunaweza kuamini kwamba Mungu ana mpango bora kwa ajili ya maisha yetu.
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yeremia 29;11, NKJV).
Tunapoamini katika mpango wa Mungu tunaweza kuishi kwa amani badala ya hofu.
3. Ishi kwa hekima na jiandae kwa ajili ya kesho
Ingawa hatuwezi kujua kila kitu, tunaweza kuchukua hatua kwa ajili ya kujiandaa kwa siku zijazo. Biblia inatutia moyo kupanga mipango yetu kwa hekima:
“Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia” (Mithali 22:3, NKJV).
Kwa kufanya maamuzi ya hekima leo, tunaweza kuandaa kesho yetu iliyo njema.
Kesho yako imebeba nini
Hatima yetu iko mikononi mwa Mungu. Ameahidi siku zijazo ambapo uovu utaangamizwa, na wale wanaomtumaini wataishi milele kwa amani (Ufunuo 21:1-4). Yawezekana kuwa haujui mambo yote kuhusu kesho yako, lakini unaweza kuishi ukiwa na ujasiri kwa kumwamini Mungu. Anajua mipango aliyonayo kwa ajili yako, na kwa kumfuata, unaweza kutembea ukiwa na amani, matumaini, na uhakika.
Anza leo kwa kuomba uongozi wake, kusoma Neno la Mungu, na kuamini katika mpango wake mkamilifu kwa ajili ya maisha yako!