Desturi na Mila za Ndoa za Kiafrika—Muhtasari
Ndoa barani Afrika ni hafla ya kupendeza iliyojaa shangwe na nderemo. Hii inatokana na utajiri au wingi wa utamaduni wa bara hili, zikionyesha utofauti wa makabila na imani za kidini, hivyo hutoa aina mbalimbali za mila na desturi za ndoa.
Ikiwa unapanga kufunga ndoa kwa tamaduni za Kiafrika au unataka kuelewa matarajio ya kitamaduni kuhusu ndoa barani Afrika, basi uko mahali sahihi.
Katika ukurasa huu, tutazungumzia mila za ndoa za Kiafrika kutoka mwanzo hadi mwisho.
Tutaangalia mambo yafuatayo:
- Umuhimu wa ndoa katika tamaduni za Kiafrika
- Taratibu za kitamaduni kabla ya harusi
- Mila zinazo fanyika wakati wa sherehe ya harusi
- Mila baada ya sherehe ya harusi
- Inamaanisha nini kufunga ndoa kiafrika
Tuanze kwa kujadili ni nini kinachofanya ndoa kuwa muhimu sana katika jamii za Kiafrika.
Umuhimu wa ndoa katika tamaduni za Kiafrika

Photo by Steward Masweneng
Kwa jamii nyingi za Kiafrika, ndoa ni hatua muhimu ya maisha.
Jamii nyingi za Kiafrika leo huona ndoa kama muungano wa mwanamume na mwanamke, msingi wa familia unaosaidia kuendeleza kizazi, kukuza ukoo, na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Katika ukurasa huu, tutaona tamaduni mbalimbali za ndoa za Kiafrika katika muktadha wa ndoa kati ya mwanaume na mwanamke.
Tofauti za kikabila na kikanda barani Afrika
Ni muhimu kuelewa utofauti mkubwa wa tamaduni za Kiafrika. Hakuna kitu kama “Taratibu za Kiafrika”1 inapokuja kwenye suala la ndoa. Afrika ni bara kubwa lenye nchi 54, kila moja ikiwa na makabila na desturi zake za kipekee.
Afrika Kusini ni moja ya nchi yenye mchanganyiko wa rangi na makabila mbalimbali. Nchi hii ina makabila mengi ya watu weusi, jamii za kizungu, na watu wa mchanganyiko wa asili tofauti. Baadhi ya nchi kama Nigeria zina zaidi ya makabila 250, kila moja likiwa na desturi zake za kipekee.
Hata hivyo, kuna mfanano mkubwa katika jamii za Kiafrika zinavyoshughulikia ndoa. Ushirikiano wa familia, majadiliano ya mahari, na matarajio ya ndoa ni desturi zinazopatikana katika jamii nyingi za Kiafrika.
Mbali na mila za kitamaduni, Afrika ni bara lenye mchanganyiko mkubwa wa dini. Ukristo, Uislamu, na dini za asili za Kiafrika ni imani kuu zinazo athiri desturi za ndoa barani.
Mambo haya yote pia yanaathiriwa na tamaduni za ndoa kutoka ulimwengu wa Magharibi, athari inayoongezeka kutokana na ukuaji wa miji na utandawazi katika nchi nyingi za Kiafrika.
Hii husababisha mchanganyiko wa desturi za ndoa za kiasili na za kisasa.
Ndoa za kimila dhidi ya ndoa za kisasa

Photo by S and S Love Story
Ndoa za kimila ni sherehe za ndoa zinazofuata mila na desturi za jamii husika. Ndoa za kisasa, kwa upande mwingine, ni sherehe rasmi zinazounganisha desturi za kitamaduni, kidini, na kisheria za kisasa.
Kwa mfano, katika ndoa za kisasa, bibi harusi huvaa mavazi meupe ya harusi. Katika ndoa za kitamaduni, anavaa mavazi ya kiasili kama vile mavazi ya Ankara (kitenge) yenye rangi za kuvutia,na mara nyingine mavazi yake huendana na mavazi ya bwana harusi.
Pia, katika ndoa za kisasa, kiongozi wa dini au mwakilishi wa kisheria anasimamia ndoa. Katika ndoa za kitamaduni, wazee wa jamii huchukua nafasi kubwa zaidi, pamoja na viongozi wa kidini na kiraia.
Watu wengi huchagua kuwa na harusi zote mbili, ya kitamaduni na ya kisasa, na mara nyingi, hizi hufanyika katika nyakati na maeneo tofauti.
Sehemu zifuatazo zitaongelea mila katika sherehe za ndoa za kisasa za Kiafrika, ambapo desturi na ushawishi wa kisasa vinazingatiwa.
Hebu tuanze kwa kujadili tamaduni za Kiafrika zinazofanyika kabla ya harusi.
Mila kabla ya ndoa
Sherehe za ndoa za Kiafrika hujaa shamrashamra na matarajio mengi. Kwa kuwa familia ina nafasi kubwa katika ndoa, kutoroshana na kufunga ndoa bila ruhusa huonekana kama kitendo cha kukosa heshima.
Baadhi ya mila hizi ni pamoja na:
- Utambulisho wa mwenza
- Majadiliano ya mahari
Utambulisho wa mwenza
Chaguo la mwenza ni hatua muhimu ambayo inapaswa kufanywa kwa uangalifu. Ingawa mvuto wa kimwili ni sifa ya ziada, tamaduni nyingi za Kiafrika zinazingatia tabia na maadili kama vigezo vikuu katika uchaguzi wa mwenza wa ndoa.
Leo, watu wengi wanaotafuta mwenza wa ndoa hukutana shuleni, kazini, katika vikundi vya kidini, kupitia familia na marafiki, na hata mtandaoni. Baada ya kufahamiana kwa kina, ikiwa wataamua kuanzisha mahusiano thabiti, watakutana na familia za kila mmoja.
Hii ni tofauti na zamani, ambapo wazazi walihusika moja kwa moja katika upangaji wa ndoa, au ambapo mwanamume mwenyewe alihusika katika kutafuta mke. Katika jamii kama Wajaluo wa Kenya na Tanzania, kabila la Himba la Namibia, na kabila la Frafra la Ghana, bila kuzingatia utayari wa bibi harusi mtarajiwa. Hata hivyo, desturi kama hizo hazikubaliki tena katika jamii nyingi za kiafrika.
Baada ya wenza hao kukutana na familia za pande zote mbili, wazazi na walezi hufanya utafiti kuhusu mwenza mtarajiwa kwa kukusanya taarifa juu ya tabia zao, historia ya familia, na sifa zao kwa ujumla.
Ikiwa kuna wasiwasi wowote, familia zinaweza kuwashauri wachumba hao kufikiria upya uchaguzi wao. Hata hivyo, ikiwa kila kitu kinaonekana kuwa sawa, wataruhusiwa kuendelea na uchumba wao. Wanapojisikia kuwa wako tayari kuanza mipango ya harusi, wataandaa sherehe ya kuzikutanisha familia hizo mbili.
Utambulisho wa familia
Wachumba hao wanapothibitishwa na familia zao, wanapanga utaratibu wa kutambulisha familia hizo mbili.
Hapo zamani, wakati mawasiliano kati ya wanaume na wanawake yalikuwa na vizuizi, kama ilivyokuwa katika ndoa za kupangwa, sherehe za utambulisho zilijumuisha mapendekezo na mara nyingine kuwakutanisha wahusika wa ndoa hiyo kwa mara ya kwanza kabisa.
Lakini katika Afrika ya sasa, sherehe hii inaratibiwa na bibi harusi na bwana harusi baada ya uchumba uliofanikiwa. Mara nyingi, sherehe ya utambulisho hufanyika nyumbani kwa bibi harusi.
Sherehe hii inahusisha familia ya bwana harusi kuwasilisha nia ya mwana wao ya kumuoa bibi harusi. Ingawa bwana harusi atakuwa tayari ametoa posa isiyo rasmi kwa bibi harusi, hii hutumika kama posa rasmi, ambayo bibi harusi hukubali mbele ya familia yake.
Utambulisho uliofanikiwa unahitaji yafuatayo:
1. Wawakilishi wenye ufasaha
Familia ya bwana harusi na bibi harusi inahitaji mwakilishi ambaye anaelewa mila na desturi za sherehe hiyo ili kuongoza mazungumzo. Hii ni kwa sababu, Posa ya Kiafrika mara nyingi huwasilishwa kwa hotuba za kuvutia na ucheshi.
Kwa mfano, baada ya kufanya maandalizi makubwa ya kupokea familia ya bwana harusi, familia ya bibi harusi inaweza kuonyesha kana kwamba hawajui chochote kuhusu ujio wa familia ya bwana harusi. Kwa ucheshi, wanaweza kuomba familia ya bwana harusi kueleza wazi lengo la ujio wao, ili wasije wakachukuliwa kama wapita njia.
2. Zawadi

Photo by vierra Liezz
Familia ya bwana harusi itatuma pesa au bidhaa za chakula mapema kama mchango wa gharama za ugeni.
Kwa mila za Wakamba nchini Kenya, bwana harusi na msafara wake hupewa jukumu la kupika nyumbani kwa bibi harusi.
Kando na hili, hakuna gharama nyingine inayohitajika wakati wa hafla ya utambulisho. Hata hivyo, bibi harusi anaweza kupewa zawadi za thamani kama pete au vitu vya thamani ili kuonyesha kuwa sasa amechumbiwa rasmi.
3. Matarajio mengine ya kitamaduni
Wakati wa utambulisho, bibi harusi na bwana harusi wanatarajiwa kuonesha heshima na adabu. Katika tamaduni nyingi, hawaruhusiwi kusema chochote. Wawakilishi wa familia zao huwatambulisha, kisha familia ya bwana harusi hueleza lengo la ujio wao.
Kwa Wazulu wa Afrika Kusini, familia ya bwana harusi huandika barua rasmi ya posa kwa familia ya bibi harusi. Barua hii inapaswa kueleza kwa uwazi nia yao ya ndoa na mipango ya siku za usoni, ikiwa ni pamoja na tarehe maalum za majadiliano ya mahari (lobola), ambayo yanaweza kufanyika baada ya wiki kadhaa au miezi michache ijayo.
Majadiliano na malipo ya mahari
Mazungumzo na utoaji wa mahari ni hatua muhimu sana kwani yanaonyesha nia ya dhati ya bwana harusi ya kumuoa bibi harusi.
Katika utamaduni wa Kiafrika, mahari2 ni pesa au mali za thamani zinazotolewa na bwana harusi au familia yake kwa familia ya bibi harusi kama sehemu ya maandalizi ya ndoa.
Mahari mara nyingi ni ishara ya uwezo wa bwana harusi kutunza familia. Pia, ni njia ya bwana harusi kuonyesha shukrani kwa familia ya bibi harusi kwa kumlea na kumuandaa kuwa mke wake.
Ingawa desturi ya kutoa mahari mara nyingine imekuwa ikitumiwa vibaya, inapofanywa vizuri, huwa ni chanzo cha fahari kwa bibi harusi na bwana harusi. Bibi harusi huhisi kuthaminiwa na familia yake kutokana na bei wanayoweka, pamoja na bwana harusi kwa juhudi zake za kulipa ili kumuoa. Kwa upande mwingine, bwana harusi huona hili kama njia ya kujidhihirisha na kuthibitisha ahadi yake ya ndoa.
Hivi ndivyo kwa kawaida, mchakato mzima unavyofanyika:
1. Mchakato wa mazungumzo
Bwana harusi, akifuatana na msafara wa marafiki na familia yake, anatembelea familia ya bibi harusi tena. Na wakati huu, timu maalum ya wawakilishi wataalamu kutoka pande zote mbili inahusika. Hawa mara nyingi ni wanachama wazee wa familia ya bibi harusi na bwana harusi.
Mchakato wa majadiliano ya mahari hutofautiana kati ya jamii mbalimbali za Kiafrika.
Kwa kawaida, familia ya bibi harusi huweka bei yao, na familia ya bwana harusi hujaribu kupunguza kiasi hicho. Vinginevyo, familia ya bwana harusi inaweza kutoa pendekezo lao, na ikiwa familia ya bibi harusi inaridhika, wanakubali tu pendekezo hilo.
Desturi hizi zinabadilika na kizazi kipya, ambacho kinazingatia zaidi matakwa ya wanandoa.
Wanapunguza shinikizo kuhusu kiasi cha mahari, na sherehe inachukuliwa zaidi kama fursa ya familia mbili kuungana.
Bila kujali tofauti za tamaduni, jambo muhimu zaidi ni makubaliano ya pamoja kuhusu bei ya mahari.
2. Malipo ya mahari

Photo by Mark Stebnicki
Jamii tofauti za Kiafrika hutumia aina mbalimbali za vitu kama mahari.
Ng’ombe ni miongoni mwa vitu vinavyotumika zaidi kama malipo ya mahari. Mbali na hayo, vitu kama pesa, mavazi, na mapambo pia vinaweza kutolewa. Katika mazingira ya kisasa na mijini, baadhi ya familia hukubali pesa pekee.
Kwa mfano, miongoni mwa Waluo wa Afrika Mashariki, ng’ombe hutolewa kwa baba wa bibi harusi daima. Hata hivyo, pesa—zinazojulikana kama ayie (ikimaanisha ‘nakubaliana’) hutolewa kwa mama wa bibi harusi.
Katika jamii za Afrika Magharibi, karanga za kola ni sehemu muhimu ya mahari. Hii ni desturi inayopatikana katika nchi kama Niger, Nigeria, Benin, Ghana, Sierra Leone, na Liberia.
Katika baadhi ya matukio, utambulisho wa familia na makubaliano ya mahari hufanyika pamoja.
Kwa mujibu wa desturi nyingi za Kiafrika, wanandoa huchukuliwa kuwa wamefunga ndoa mara tu mahari inapolipwa. Baada ya hapo, wanaweza kuchagua mojawapo ya njia tatu:
- Kuchukulia jambo hili kama ndoa yao ya kimila na kuanza kuishi pamoja.
- Kupanga harusi ya kimila au ya kisasa baada ya muda fulani. (Au kufanya zote mbili!)
- Kuafikisha ndoa yao kupitia wakili.
Katika hatua hii, wanandoa wanaweza kutimiza mahitaji ya kidini na ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria ushauri wa kabla ya ndoa na kuomba cheti cha ndoa.
Haya yote yanapaswa kukamilika kabla ya tarehe ya ndoa iliyopangwa.
Sehemu zinazofuata zitajadili desturi za harusi za kisasa, zikichanganya tamaduni, imani za kidini na kiraia, pamoja na sheria za ndoa.
Mila zinazofanyika wakati wa sherehe ya harusi
Harusi ni mojawapo ya sherehe zinazopambwa sana katika tamaduni za ndoa barani Afrika. Kama ilivyo kwa sherehe nyingine, mila za harusi3 hutofautiana kati ya mataifa mbalimbali ya Afrika.
Baadhi ya watu huchagua kuwa na ndoa ya kitamaduni ya Kiafrika, lakini mara nyingi, mazoea ya kidini, mahitaji ya kisheria, na ushawishi kutoka kwa ulimwengu wa Magharibi husababisha wengi kufunga ndoa za kisasa. Hivyo, ndoa nyingi barani Afrika ni mchanganyiko wa ndoa za kitamaduni na za kisasa.
Hebu tuangalia aina hizi mbili tunapochunguza kinachoendelea kwenye harusi za Kiafrika.
Msafara wa bibi harusi

Photo by Gad Samuel
Harusi zote, za kitamaduni na za kisasa, huwa na msafara wa bibi harusi.
Msafara huu huchaguliwa na bibi harusi na bwana harusi, na unajumuisha:
- Wasindikizaji wa kiume na wa kike: Marafiki wa kiume na wa kike kutoka familia ya bibi harusi na bwana harusi.
- Wasichana na wavulana wanaobeba maua na vitabu: Rafiki na ndugu wa umri mdogo wa bibi harusi na bwana harusi.
- Wasimamizi: Wanandoa wazoefu waliochaguliwa kuwa walezi wa bibi harusi na bwana harusi.
- Matroni na waongozaji: Marafiki wa maharusi wanaoratibu msafara wa bibi harusi na shughuli za harusi.
Wote wana majukumu maalum yanayofanya harusi kuwa ya kuvutia na yenye mafanikio. Kwa mfano, wasindikizaji wa maharusi husherehekea na kucheza pamoja na wanandoa wakati wa kuwapokea.
Mara nyingi, wao huvaa mavazi yaliyopangwa kwa rangi zinazozingatia mitindo ya kitamaduni, ikiwa ni pamoja na vipengele vya mavazi ya Kiafrika au ankara.
Kwa mfano, katika makabila ya Nigeria kama vile Yoruba na Igbo, mavazi yao ya kitamaduni wanayovaa kwenye harusi yana maana kubwa. Yanawakilisha umoja, mshikamano, na utambulisho mpya wa pamoja wa wanandoa.
Kumpamba bibi harusi

Photo by Meshack Emmanuel Kazanshyi
Katika ndoa za Kiafrika, iwe za kitamaduni au za kisasa, bibi harusi hupambwa kwa uangalifu mkubwa. Mila mbalimbali za urembo hufanyika katika jamii nyingi za Kiafrika.
Mojawapo ya mila za kupendeza kwa bibi harusi ni sherehe ya hina, ambapo mikono na miguu yake hupambwa na wataalamu wa hina. Mila hii hupatikana Afrika Mashariki, Kaskazini, na Magharibi.
Mbali na hina, bibi harusi hupambwa kwa mapambo ya dhahabu na hereni za kipekee zilizotengenezwa kwa miundo maalum.
Sherehe ya kumchukua bibi harusi
Sherehe hii hufanyika asubuhi ya siku ya harusi. Bwana harusi, familia yake, na marafiki huenda nyumbani kwa bibi harusi kumchukua kabla ya sherehe.
Katika baadhi ya jamii, ndugu wa bibi harusi wanaweza kuwawekea vikwazo vya kuchekesha wakati msafara wa bwana harusi unapofika. Vikwazo hivi mara nyingi vinahusisha kuomba zawadi fulani kabla ya kuwaachia waingie nyumbani. Hii ni desturi ya kufurahisha na haipaswi kuleta ugumu wowote.
Kwa kawaida, familia ya bibi harusi hutayarisha kifungua kinywa kwa ajili ya kushirikiana na wageni na msafara wa bibi harusi.
Hii inaweza kufuatiwa na mchezo ambapo bwana harusi anafungwa macho na kupewa changamoto ya kumtambua bibi harusi kutoka kwa mstari wa wanawake waliovaa mavazi yanayofunika miili yao yote.
Kabla ya kuondoka kwenda kwenye sherehe ya harusi, kunaweza kuwa na wakati wa baraka kutoka kwa wazazi. Hii inaweza kuwa ibada ya maombii au desturi za kimila kama kutemewa mate ya baraka, desturi inayofanyika miongoni mwa Wamaasai wa Afrika Mashariki.
Baada ya yote kumalizika, wanatoka pamoja kwa msafara wa magari kuelekea kwenye sherehe.
Sherehe ya ndoa
Barani Afrika, ndoa ni ya wapenzi wawili, lakini harusi ni ya familia na jamii. Inaleta rasmi familia mbili pamoja. Hivyo basi, ushiriki wa familia ni mkubwa, na mara nyingi ni siku ya sherehe kubwa. Kwa kweli, idadi ya wageni inaweza kuwa kati ya 500 hadi 1000.
Ndoa inaweza kufungwa kanisani, katika kituo cha jamii, bustanini, ukumbini, nyumbani, au mahali popote wanandoa watakapochagua. Haijalishi ni wapi, sehemu hiyo hupambwa kwa maua na mapambo mengine ya sherehe.
Sherehe huanza na msafara wa bibi harusi, na unafikia kilele chake wakati bibi harusi anapofika.
Kisha, bibi harusi anatembea kwenye njia akiongozana na wazazi wake wote wawili hadi kukutana na bwana harusi. Mchungaji anayesimamia harusi atatoa mahubiri mafupi au hotuba, kisha kuwaongoza wanandoa kubadilishana viapo vyao, kusaini vyeti vyao vya harusi, na kushiriki ishara nyingine za umoja wao. Hii inaweza kuwa chochote kinachowakilisha umoja, kama vile kuchanganya rangi kwenye jagi ili kuashiria umoja usioweza kuvunjika.
Baada ya harusi, wanandoa wapya pamoja na msafara wa bibi harusi wataenda kupiga picha, kisha wataungana na kila mtu katika eneo la sherehe.
Sherehe ya mapokezi
Sherehe ya mapokezi ni hatua ya mwisho ya harusi, iwe ya kitamaduni au ya kisasa. Ni wakati wa furaha na shangwe, ambapo wanandoa wapya wanachukuliwa kama wageni wa heshima kwani sherehe inawalenga wao.
Wakati timu ya bibi harusi inaenda kupiga picha, wageni kwa kawaida huenda kwenye eneo la mapokezi. Hii inaweza kuwa katika eneo la harusi au mahali pengine, mara nyingi nje. Ukumbi hupambwa kwa rangi za harusi, mahema husimamishwa, na muziki hupigwa. Ni sherehe ya kusherehekea wanandoa wapya.
Hapa kuna maelezo maalum ya kuzingatia katika mapokezi ya harusi ya kisasa ya Kiafrika:
1. Vyakula vinavyotolewa
Mapokezi hayawezi kukamilika bila chakula, kwani chakula ni muhimu katika sherehe za Kiafrika. Wanandoa, familia zao na marafiki ndiyo wahusika wa kufanikisha bajeti ya chakula.
Menyu mara nyingi hujumuisha mchanganyiko wa vyakula pendwa kutoka kwa tamaduni za bibi harusi na bwana harusi.
Baada ya chakula, kuna tukio la kukata keki. Vinywaji pia vinatolewa, na hii inaweza kujumuisha vinywaji vya kitamaduni pamoja na juisi.
Kwa mfano, miongoni mwa Wakalenjin wa Afrika Mashariki, mursik—maziwa ya kienyeji yaliyosindikwa—ni ya thamani kubwa. Hutolewa katika koito (harusi ya kitamaduni ya Kalenjin) na pia kwenye mapokezi ya harusi za kisasa.
Yapo mafundisho ya kitamaduni ambayo yanahusianishwa na chakula kinacholiwa harusini.
Kukata keki huwa ni kati ya matukio muhimu sana. Wana ndoa wapya hukata keki kwa ajili ya kulishana wao kwa wao na kwa ajili ya kuwalisha watu wengine waliohudhuria. Hii huashiria umoja na ushirikiano ambao ni muhimu kwa familia mpya.
Baadhi ya makabila kama jamii ya Yoruba ya Afrika Magharibi hutumia mtindo wa kuonja vipengele vinne. Hii inalenga kuwakumbusha wanandoa wapya ukweli wa ndoa.
Vipengele vinajumuisha:
- Ndimu: Inawakilisha mapungufu ambayo wanandoa wanaweza kukutana nayo katika ndoa.
- Siki: Inawakilisha uchungu na mizozo ambayo wanandoa wanaweza kukutana nayo katika ndoa.
- Pilipili: Inawakilisha hamasa na ladha ambayo hufanya uhusiano wa ndoa kuwa wa kipekee.
- Kijiko cha asali tamu: Inawakilisha utamu wa ndoa.
Katika baadhi ya tamaduni, kumimina sadaka ya vinywaji hufanywa kama ishara ya heshima kwa mababu na kuonyesha uhusiano na roho za wafu. Hata hivyo, desturi hii inafanyika tu katika maeneo ambapo dini za tamaduni za Kiafrika zinaheshimiwa. Kwa upande mwingine,
Ukristo mara nyingi hauhusishi kipengele hiki, au hutafuta njia nyingine ya kuheshimu urithi wa familia, kwa kuwa mtazamo wa Biblia kuhusu wafu ni kwamba wamepumzika, hawajitambui, na hawahusiki na mambo ya walio hai.
Baada ya kula, wageni huketi kwenye viti vilivyopangwa kwa mpangilio maalum.
2. Mpangilio wa ukaaji
Katika harusi za kitamaduni za Kiafrika, mpangilio wa viti huwekwa kwa namna ambayo familia ya bwana harusi na familia ya bibi harusi huketi uso kwa uso. Wageni huketi kulingana na uhusiano wao na wanandoa, kwa mfano, wafanyakazi wenza wa bibi harusi huketi upande wa familia yake.
Desturi hii bado inatumika katika harusi za kisasa, ingawa kizazi cha sasa kimelegeza utaratibu huu na kuruhusu wageni kukaa kwa uhuru zaidi.
Wazazi huheshimiwa kwa kuhudumiwa chakula mezani badala ya kusimama kwenye foleni kama wageni wengine. Pia, wanandoa wapya na timu ya bibi harusi huketi katikati ya familia zao mbili kama ishara ya muungano wao.
Baada ya kupiga picha, wanandoa wapya na msafara wao wanapowasili ukumbini, wanakaribishwa kwa shangwe na nderemo kama ishara ya kuanza rasmi kwa sherehe.
3. Sherehe, muziki na ngoma

Photo by Tweve Nyamaka
Msafara wa bibi harusi utaingia kwenye sherehe wakicheza muziki wa harusi ya kitamaduni.
Muziki huu unaweza kuwa wa kitamaduni wa jamii husika au nyimbo maarufu za harusi kwa wakati huo. Wageni wote hujiunga na msafara kwa kucheza, na sherehe hii huendelea kwa muda. Bwana harusi na bibi harusi, wakiwa katikati ya msafara, huchukua nafasi kuu wakati wa kucheza.
Muktadha wa sherehe mara nyingi huakisi desturi za kitamaduni za kabila la wanandoa, ikiwemo mavazi, muziki, na baadhi ya mila muhimu zinazofuatwa wakati wa hafla.
Kwa mfano, katika baadhi ya jamii za Ethiopia, wanandoa wapya huvalishwa mavazi ya kifalme kama ishara ya heshima na hadhi yao mpya ya ndoa. Wanapowasili kwenye mapokezi, wanakaribishwa kwa heshima kama mfalme na malkia, jambo linaloashiria mwanzo wa maisha yao mapya pamoja.
Katika tamaduni za Ghana, wanandoa huruka juu ya ufagio kama ishara ya kuanza maisha mapya ya ndoa. Desturi hii pia hufanyika kwa Waafrika Wamarekani kama sehemu ya urithi wa mila za Kiafrika.
Baada ya kucheza muziki, timu ya bibi harusi huketi na kuendelea kula, huku hotuba zikiendelea kutolewa.
4. Hotuba
Katika desturi za harusi za Kiafrika, wazazi, wazee, viongozi wa jamii, na wageni wa heshima hutoa ushauri kwa wanandoa wapya. Wazazi hutoa ushauri wao wa mwisho na matakwa kwa wanandoa waliovaa pete. Mara nyingi, waongeaji wanamaliza hotuba zao kwa kutoa zawadi.
5. Kutoa zawadi
Zawadi katika harusi za Kiafrika hutolewa kwa makundi. Familia za bwana harusi na bibi harusi hupewa fursa ya kuwasilisha zawadi zao. Vilevile, makundi mengine yaliyohudhuria hupata muda wa kutoa zawadi zao. Makundi haya yanaweza kujumuisha marafiki, jamii ya kanisani, na wenzake wa kazi wa wanandoa. Zawadi mara nyingi ni vitu vya nyumbani na pesa ili kusaidia kuanzisha maisha yao mapya baada ya harusi.
Tamaduni baada ya sherehe ya harusi
Baada ya sherehe ya harusi kukamilika, wanandoa wanatarajiwa kuanza maisha yao mapya pamoja. Baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia ni:
Desturi za fungate na matarajio yake

Photo by Asad Photo Maldives
Baada ya sherehe ya harusi, wanandoa huenda mahali pengine au kurudi nyumbani kuanza maisha yao ya ndoa.
Kwa vyovyote vile, wanandoa wapya wanatarajiwa kuhalalisha ndoa yao baada ya harusi.
Katika tamaduni zingine, kama miongoni mwa Wankole wa Uganda, maharusi wapya hupata mshauri wa ndoa ambaye anawasaidia katika kujua maisha ya ndoa. Mshauri huyu anaweza kutoa mwongozo kuhusu masuala ya ndoa na pia kuwa mtu wa kuwasaidia kwa maswali.
Washauri hawa wanaweza kuwa ni wanafamilia au wakwe.
Majukumu haya hutekelezwa na wanandoa waliofanikiwa katika ndoa za kisasa za Kiafrika
Mahusiano na wakwe
Ingawa wanandoa wapya wanachukuliwa kama familia mpya, bado wanabaki kuwa sehemu ya familia zao za awali. Hivyo, wanatarajiwa kujifunza jinsi ya kushirikiana kwa ufanisi na familia zao na wakwe zao.
Katika baadhi ya tamaduni, kuna sherehe ambapo bibi harusi huwapikia wakwe zake kwa kipindi cha muda baada ya fungate. Kwa mfano, katika jamii ya Wamoagha wa Burkina Faso, bibi harusi huwapikia wakwe zake kwa muda wa siku saba baada ya harusi.
Mabadiliko ya majina na hadhi katika jamii

Photo by Askar Abayev
Baada ya harusi, mtu aliyeoa au kuolewa anachukuliwa kuwa mtu mzima na mara nyingi anaheshimika. Anaweza kuitwa Bwana au Bibi, na wanapokuwa na watoto, hutambuliwa kama baba au mama fulani. Mke mpya anaweza kuchukua jina la mumewe.
Mahali pa kuishi baada ya ndoa
Katika tamaduni nyingi za Kiafrika, mke anatarajiwa kuhamia nyumbani kwa mume wake baada ya harusi. Vijana hujenga nyumba ndogo katika maeneo yanayomilikiwa na wazazi wao. Katika jamii nyingi za Afrika Mashariki, hii hujulikana kama simba (ambayo ni neno la Kiswahili linalotumika kumaanisha nyumba ndogo au makazi ya vijana)
Mwanaume aliyeoa anaweza kuendelea kuishi katika simba yake baada ya harusi na kulea watoto wake huko. Hata hivyo, anatarajiwa kujenga nyumba yake mwenyewe. Watoto wake wa kiume hawawezi kujenga simba zao hadi baba yao atakapomaliza kujenga nyumba yake.
Wanandoa wapya hawatarajiwi kuishi pamoja na wazazi wao.
Katika mazingira ya mijini, wanandoa waliooana mara nyingi huhamia kwenye nyumba zao au kutafuta nyumba za kupanga kulingana na kazi zao, maeneo yao, na mapato yao. Wengine hata hubadilisha mtaa na kuanza uzoefu mpya kabisa.
Kuoa kiafrika
Ndoa ni moja ya mila zinazothaminiwa zaidi katika utamaduni wa Kiafrika. Hivyo, ni wazo zuri kuwa na uelewa wa tamaduni na desturi zinazohusiana na ndoa za Kiafrika.
Lakini bila kujali ni tamaduni zipi zinazo jumuishwa au kutokujumuishwa katika safari ya ndoa ya wanandoa fulani, mchakato mzima—kuanzia kutafuta wenzi, hadi sherehe ya harusi, na hata baada ya harusi—hupangwa kwa umakini ili kuhakikisha kuwa kuna msingi thabiti wa ndoa na familia mpya.
Wakati kila kitu kitakapokamilika, wanandoa watakuwa tayari kuanza hatua mpya ya maisha kama sehemu ya jamii.
Kila harusi ya Kiafrika ina upekee wake, lakini hutofautiana kulingana na chaguzi binafsi za wanandoa, utamaduni wa makabila yao, dini zao, na kiwango cha utamaduni wa kisasa wanachotaka kuingiza katika harusi yao.
Ikiwa unafikiria kuoa kwa njia ya Kiafrika, hatua nzuri ya kwanza ni kujifunza zaidi kuhusu tamaduni za ndoa za kabila la mwenza wako na kuona jinsi unavyoweza kuziunganisha na tamaduni za kabila lako.
- Parkin, D. J., & Nyamwaya, D. (Eds.). (1987). Transformations of African marriage (Vol. 3). Manchester University Press. [↵]
- Goody, J., & Tambiah, S. J. (1973). Bridewealth and dowry (No. 7). CUP Archive. [↵]
- “Discover The Most Intriguing African Wedding Traditions,” Josabi, June 23, 2020. https://www.josabimariees.com/tips/discover-african-wedding-traditions/ [↵]