Ni Nini Maana ya Kuwaheshimu Wazee?
Wazee ni sehemu muhimu ya jamii kwa sababu wao ndio waliotulea, ni mfano katika jamii zetu, na wana utajiri mkubwa wa uzoefu wa maisha tunaoweza kujifunza.
Katika tamaduni nyingi barani Afrika, heshima kwa wazee husisitizwa sana.
Kuwaheshimu na kuwathamini huchukuliwa kama wajibu wa kimaadili kwaajili ya ustawi wa jamii. Wazee wanaheshimiwa kwa sababu ya uzoefu wao wa maisha, utoaji, uongozi, na kudumisha tamaduni.
Hata hivyo, wengi wetu tungependa kujua maana ya kuheshimu wazee katika enzi hii ya leo. Ni nini huchukuliwa kama kuwaheshimu wale walio na umri mkubwa kuliko sisi, au wale walio na mamlaka juu yetu? Na je, bado tunawaheshimu bila kujali tabia zao?
Au wanapaswa kustahili heshima yetu? Na ni zipi njia bora zaidi za kuwaheshimu?
Ili kujibu maswali haya na mengineyo, ukurasa huu utaangazia:
- Nini maana halisi ya kuwaheshimu wazee
- Aya za Biblia zinazozungumzia heshima kwa wazee
- Kwa nini tunawaheshimu
- Njia za kivitendo za kuonyesha heshima
- Namna ya kuwatendea wazee wakorofi na wasiovutia
- Namna ya kuweka mipaka kati yetu na wazee
- Manufaa ya kuwaheshimu wazee wetu
Hebu tuanze kwa kuangalia maana halisi ya kuwaheshimu wale waliotutangulia.
Maana ya heshima kwa wazee
Hebu tujibu swali hili kwa sehemu mbili. Kwanza, ni nani ambao tunawachukulia kwamba ni wazee wetu? Na pili, heshima humaanisha nini hasa?
Mzee ni mtu yeyote anayekuzidi umri, na inaweza pia kumaanisha mtu mwenye mamlaka zaidi yako. Kwa kawaida, tunapozungumzia wazee tunamaanisha wazazi, babu na bibi, ndugu wakubwa, viongozi, wachungaji, walimu, wahadhiri, n.k.
Heshima humaanisha kuwa na “hisia za kuwasifu” au kuthamini na kuheshimu kwa namna ya heshima inayoonyesha kuwa tunaelewa haki na matakwa ya mtu.1 Na hii inapaswa kufanyika ndani ya mipaka sahihi ili isiwe utii kipofu.
Hivyo, kuwaheshimu wazee wetu humaanisha kuwatendea wazee au watu wenye mamlaka kwa adabu, huruma, na uangalifu. Inamaanisha kutambua na kuthamini nafasi yao katika maisha yetu, jamii zetu, na tamaduni zetu.
Sasa hebu tutazame kile ambacho Biblia inasema kuhusu heshima kwa wazee.
Heshima kwa wazee katika Biblia
Swala la heshima kwa wazee ni jambo la muhimu katika moyo wa Mungu. Ametoa ushauri juu ya namna tunavyopaswa kuwaheshimu wale walio na umri mkubwa, wazazi wetu na ndugu waliotuzidi umri, na wale walio katika mamlaka.
Hili huonekana kwa uhalisia katika ukweli kwamba aliweka hili katika Amri Kumi:
“Waheshimu baba yako na mama yako, siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako” (Kutoka 20:12, NKJV).
Hii inaonyesha kwamba Mungu anachukulia aina hii ya heshima kuwa muhimu kwa jamii yenye upendo na inayostawi.
Na baadaye, katika kitabu cha Mithali, mfalme mwenye hekima Sulemani anasisitiza jinsi ilivyo muhimu kwetu kuwaheshimu na kupata hekima kutoka kwa wazee wetu, na upumbavu unaoweza kuja kutokana na kuwapuuza au kuwasahau (Mithali 1:8-9; 3:1-6; 4:1-13; 13:1; 16:31; 19:20; 20:20; 28:7).
Kwa kweli, mada ya heshima kwa wale walio juu yetu hupatikana katika Maandiko yote. Hivyo basi, hebu tuangalie kwa ukaribu baadhi ya aya kutoka Agano la Kale na Agano Jipya juu ya namna Mungu anavyotuhimiza kuwaheshimu wazee wa aina mbalimbali katika maisha yetu.
Heshima kwa wazee
Mungu aliamuru Israeli kupitia Musa kusimama kwa ajili ya wazee na “kuheshimu uwepo wa mzee” (Mambo ya Walawi 19:32, NKJV). Hii inamaanisha walipaswa kuwa makini na tabia zao wanapokuwa karibu na wazee au dhidi ya wazee.
Kwa mfano, katika Agano Jipya, Paulo anamwambia Timotheo asimkemee mzee, bali amwonye kama baba… na wanawake wazee kama mama (1 Timotheo 5:1-2).
Na tukitazama upande mwingine wa mambo, tunaweza kumtazama Rehoboamu, mmoja wa wafalme waasi wa Israeli. Upumbavu wake wa kukataa ushauri wa wazee uligawanya ufalme wa Israeli na akaishia kutwala makabila mawili tu badala ya kumi na mbili (1 Wafalme 12).
Heshima kwa viongozi wa kidini
Hannah aliomba kwa miaka mingi ili aweze kupata mtoto. Alipofanikiwa, alimweka wakfu mwanawe Samueli kwa Bwana akiwa na umri mdogo sana. Alimruhusu aishi katika hekalu ili kufundishwa na Eli, kuhani mkuu, jinsi ya kutunza na kuangalia hekalu la Israeli. Na ingawa Eli hakuwa mfano bora wa kiongozi wa kidini wakati mwingine, Samueli mdogo alimheshimu na Mungu alimbariki kupitia utii na bidii yake (1 Samueli 1-3).
Kwa upande mwingine, hata hivyo, tunaweza kuangalia kisa cha Kora katika Hesabu 16. Korah na kundi lake walitilia shaka mamlaka na kufaa kwa Musa, kiongozi aliyeteuliwa na Mungu kuwa kiongozi wao. Na mambo hayakuisha vizuri kwa Korah na wale walioshiriki katika uasi pamoja naye!
Sasa hii haimaanishi kwamba Mungu atamwadhibu yeyote anayemdharau mtu ambaye yeye amemchagua kwa kusudi fulani. Lakini hadithi hii inatuonyesha kwamba dhihaka za wazi na kujaribu mamlaka ya mtu hadharani si jambo linaloweza kuisha vizuri. Kuna njia za heshima zaidi za kukabiliana na shauku zetu dhidi ya mtu aliyepewa mamlaka, na Mungu anaweza kutusaidia katika hali hizo kama alivyofanya kwa Samueli.
Heshima kwa wazazi
Mungu anatuambia tuwaheshimu wazazi wetu, kama ilivyoandikwa katika amri ya tano iliyotajwa hapo mwanzoni. Hii ni sehemu ya msingi na muhimu ya upendo na umoja katika familia.
Mtume Paulo pia anawahimiza watoto kuwatii “wazazi wao katika Bwana, kwa maana hii ndiyo haki,” na “inampendeza Bwana” (Waefeso 6:1-3; Wakolosai 3:20, NKJV).
Pia, tukirudi katika kitabu cha Mithali, tunapata ushauri maalum kwa watoto kuzingatia maelekezo ya baba yao na ushauri wa mama yao, kwa sababu kwa ujumla, watoto watiifu huwafanya wazazi wao kufurahia na huwakinga na huzuni zinazoweza kuja kutokana na maamuzi mabaya (Mithali 1:8; 10:1; 19:26-27). Ni kanuni nzuri ya kuishi nayo.
Yesu Mwenyewe ni mfano bora kuliko yote. Ingawa ni mungu, wakati alipokuwa akiishi kama mtoto hapa duniani miongoni mwetu, Yesu “alikuwa mtiifu” kwa wazazi wake wa duniani, Mariamu na Yusufu (Luka 2:5, NKJV).
Tunaweza pia kupata visa mbalimbali kuhusu kile kinachoweza kutokea tunapowakosea heshima au kuwadhihaki wazazi wetu. Katika 2 Samweli 15-18 tunajifunza kuhusu Absalomu, mwana wa Mfalme Daudi, ambaye aligombana na baba yake na kujaribu kudhoofisha utawala wake kama mtawala wa Israeli. Baadaye, Absalomu alijitokeza waziwazi kuasi dhidi ya Daudi, jambo lililo sababisha vita, na maisha yake yakakatishwa mapema (2 Samweli 18:9-10, 14-15).
Ingawa hii ni hali ya kusikitisha zaidi, bila shaka, tunaposoma hadithi nzima, tunaweza kuona jinsi mbegu za uasi na kutotii zinaweza kukua na kutoa hisia kali mno na ujeuri.
Kuna njia bora zaidi ambazo Absalomu angetumia kukabiliana na kutoridhika na mienendo ya mzazi.
Heshima kwa viongozi wa umma

Photo by Kindel Media
Biblia inatuagiza kuwaheshimu viongozi wa serikali na wale walio na mamlaka katika jamii zetu.
Paulo anaagiza ”Kila mtu …aitii mamlaka iliyo kuu…” (Warumi 13:1, NKJV).2 Hebu fikiria jinsi jamii itaimarika ikiwapo kutakuwa na heshima kwa mamlaka na sheria?
Mfano mmoja unaotuonyesha jinsi tunavyoweza heshimu mtu aliye na mamlaka hata kama hatukubaliani kabisa na mienendo au mitazamo yao.
Katika 1 Samweli 13:13-14, 24:1-22, ttunasoma kuhusu Daudi, ambaye aliwekwa wakfu kuwa mfalme mtarajiwa wa Israeli. Na mfalme wa wakati huo, Sauli, hakufurahia jinsi Daudi alivyokuwa akiheshimika na kuwa maarufu kumliko. Alijawa na wivu dhidi ya Daudi kiasi cha kutaka kumuua!
Lakini Daudi bado aliheshimu mamlaka ya Mfalme Sauli hata wakati alipokuwa akitendewa mabaya. Daudi alikuwa na nafasi ya kulipiza kisasi na hata kumuua Mfalme Sauli, na hata rafiki zake walimhimiza kufanya hivyo. Lakini alichagua kutunza uaminifu wake na kuheshimu nafasi ya Sauli
Heshima kwa walimu na walezi
Biblia inatoa mifano ya watu walio waheshimu wale waliowasaidia kutengeneza maisha na maamuzi yao.
Kwa mfano, tukimtazama Timotheo, kijana aliye lelewa na Mtume Paulo. Kwa kufuata mwongozo wa mlezi wake kwa makini, alikabidhiwa majukumu makubwa, pamoja na kutumwa kumwakilisha Paulo sehemu mbalimbali (1 Timotheo 1:1-4; 1 Wathesalonike 3:2). Paulo aliona namna Timotheo alivyo iheshimu imani ya wazee wake, kama mama yake na bibi yake (2 Timotheo 1:5-6).
Kabla ya kifo cha Paulo, kwenye barua yake ya mwisho kwa Timotheo, anamkabidhi Timotheo wito wa huduma yake, akimhimiza aendelee na kazi hiyo, sawa kabisa na kumkabidhi mwenge (2 Timotheo 4:1-2, 5).
Sasa tuangalie kwanini tunapaswa kuwaheshimu watu walio na umri mkubwa kuliko sisi au walio katika mamlaka.
Kwa Nini Tuwaheshimu Wazee Wetu

Photo by Ian Macharia on Unsplash
Wazee wana jukumu kubwa katika jamii. Wengine ni kama wanariadha waliotangulia katika mbio za vijiti, wakisubiri kukabidhi kijiti kwa kundi linalofuata. Wengine bado wana nguvu na wako tayari kuendelea. Uzoefu wao unawafanya kuwa wa thamani sana kwa jamii.
Zifuatazo ni baadhi ya sababu za kuwaheshimu:
Wameumbwa kwa mfano wa Mungu
Jambo la kwanza na la muhimu, wazee wetu pia ni wanadamu walioumbwa kwa mfano wa Mungu, na kwa sababu hiyo, wanastahili heshima.
Kwanini iko hivyo?
Kwa sababu kati ya vitu mbalimbali visivyo na idadi vilivyoumbwa na Mungu, alifanya jambo la pekee kwa wanadamu. Kwanza, aliwaumba kwa mfano na sura yake (Mwanzo 1:26-27; 5:1).
Pili, tofauti na viumbe vingine ambavyo viliumbwa kwa neno la Mungu (Zaburi 33:6, 9; Mwanzo 1), Mungu alitumia muda na nguvu kuwaumba wanadamu kwa mikono yake mwenyewe. Kisha, akainama karibu na mwanadamu wa kwanza aliyemuumba,”akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7, NKJV).
Kwa kufanya hivi, Mungu aliwapa heshima kubwa wanadamu
Hili pia huendana na tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba “Wanadamu wote wana haki ya kutendewa kwa heshima na staha.”3
Wana hekima
Wazee wetu wamepata hekima kutokana na uzoefu wao. Kwa kuwaheshimu na kuwathamini, tunakaribishwa katika chemchemi ya hekima yao na tunaweza kujifunza kitu kutoka kwao.
Pia, kutokana na uzoefu wao wa maisha na maarifa, wazee mara nyingi hutoa mwongozo kwa wale wanaokuja nyuma yao.
Wamejifunza kutoka kwa makosa na mafanikio yao, na wana uwezo wa kutusaidia kuepuka vitu vinavyoweza kutupotezea mwelekeo wa maendeleo yetu.
Methali ya zamani ya kiafrika inatukumbusha kwamba, “Kile ambacho mzee anaweza kuona akiwa ameketi, kijana hawezi kuona akiwa amesimama juu ya mti .” Kuashiria kwamba hekima ya mzee inaweza kuona mbali zaidi kuliko ile ya kijana.
Hata kama “mzee” katika maisha yako ni mtu mwenye umri mdogo katika mamlaka, bado unaweza kujifunza kutokana na uongozi na uzoefu wake.
Watunza historia
Baadhi ya tamaduni, zinaendeleza mila za masimulizi na mambo muhimu hupokezwa kizazi na kingine kupitia hadithi. Hivyo, wazee huwa maktaba iliyojaa taarifa muhimu na mtazamo wa kurithisha kizazi kijacho.
Chemichemi ya upendo na msaada
Ndugu wakubwa ni chanzo kizuri cha upendo na msaada katika nyakati ngumu. Wanaweza kutoa ushauri, kulia pamoja nasi, na kututia moyo.
.
Pamoja na hayo, tunapowasaidia, wanajisikia kutambulika na kuthaminika katika uzoefu wao. inawasaidia kujihisi wako salama, wanapotambua kwamba tunawajali na kuwathamini.
Ripoti ya Stanford ya mwaka 2016 pia inaonyesha kwamba aina hii ya ushirikiano mwema na wazee huwasaidia “Kujisikia kuridhika kihisia , kuimarisha afya zao za kimwili na kiakili.4
Hivyo, kuna tofauti kubwa tunapowajali wazee wetu kwa heshima, ufahamu, na wema.
Hebu tuone njia halisi za kuonyesha heshima hii.
Njia halisi za kuonyesha heshima kwa wazee
Tunaweza kupata njia mbalimbali za kuwaheshimu wazee kwa kutazama ndani ya tamaduni zetu. Wakati mwingine vijana huonyesha heshima yao kwa kuinama kidogo mbele ya wazee. Katika tamaduni nyingine, kuishi maisha ya unyenyekevu huonyesha heshima kwa malezi yetu.
Ingawa ni muhimu kujifunza desturi za kitamaduni zinazokubalika ili usionekane kukosa heshima, kuna kanuni za heshima ambazo zinapita tamaduni, dini, rangi, au wakati.
Baadhi ya njia za kuonyesha heshima kwa wazee:
Kutenga muda kuwa pamoja nao

Photo by Kampus Production
Kutumia muda wetu na wazee wetu huonyesha tunawathamini kiasi cha kuacha shughuli zetu mbalimbali na kutumia muda pamoja nao. Hii inatupa fursa nzuri ya kupata ushauri wao au kushiriki katika shughuli ambazo tunaweza kujifunza kutoka kwao.
Njia ambazo tunaweza kutumia muda pamoja na wazee wetu ni pamoja na:
- Kushiriki chakula pamoja
- Kuwafundisha ujuzi mpya kama matumizi ya kifaa fulani, kujifunza lugha pamoja, n.k.
- Kuimba au kufanya mazoezi ya muziki pamoja
- Kutembea pamoja nao, n.k.
Kupitia shughuli kama hizi, wazee wako wata “jisikia furaha ya kuiona dunia kupitia mtazamo wa vijana,”5wakitengeneza uhusiano wa kudumu na kumbukumbu.
Kutanguliza mahitaji yao
Njia nyingine ya kuonyesha heshima kwa wazee ni kuyapa kipaumbele mahitaji yao. Ikiwa mzee anaingia kwenye basi au katika chumba ambapo hakuna viti vya kutosha, tunaweza kumpisha kiti . Au kuwasaidia kufika kwenye miadi au kufanya kazi zao.
Na wanapokuwa katika umri wa uzee na wanahitaji kulelewa kama wazee, vijana wanaweza kutimiza mahitaji yao ya msingi, kutoa msaada wa kifedha, kutunza kile wanachokipenda, au kuwasaidia katika kazi kubwa ambazo hawawezi tena kufanya.
Kuwasikiliza kwa umakini
Kuwasikiliza kwa umakini na utulivu ni njia nyingine ya kuonyesha heshima kwa wazee.
Hii inaweza kufanyika kwa kuwapa muda wa kuelezea mawazo yao na kuuliza kwa adabu ikiwa hatujaelewa.
Je mazungumzo hayaonekani kuwa na maana zaidi wakati mtu mwingine anapouliza maswali, anataka kujua zaidi, au anatoa mawazo au majibu yake wakati unaofaa?
Tunaweza kuwaheshimu wazee wetu kwa kuwapa aina hii ya umakini unaostahili, na wanaweza kujua kwamba wamesikilizwa.
Kuwapenda
Wazee wetu wanaweza kuwa na uzoefu zaidi kuliko sisi, lakini bado wanahitaji upendo kama binadamu wengine wakati wowote katika maisha yao. Kuwapenda kwa dhati na si kwa maslahi binafsi kutawafanya wajisikie kuthaminika na kukubalika. Tunaweza kuonyesha upendo kwao kwa:
- Kuwasiliana nao mara kwa mara
- Kuwaruhusu kuwa na muda pamoja na watoto wetu.
- Kuwaonyesha upendo
- Kuheshimu maoni yao, mambo wanayopendelea na chaguzi wao, hata kama hatukubaliani nao
Kwa mfano, fikiria kwamba wewe ni kijana unayejiandaa kwa chuo. Na unakutana na wazee ambao wana msimamo kuhusu desturi zao zinazohimiza ndoa za mapema.
Hawakuwahi kwenda shule na hawaoni umuhimu wa kuwa na elimu rasmi.
Unapozungumza nao, wanakueleza kuwa unapaswa kuzingatia kuolewa hivi karibuni, ili kuonyesha heshima kwa tamaduni zako.
Lakini ingawa unaona ni muhimu zaidi kuendelea na elimu, unaweza kuwasikiliza wanachosema. Na unaweza kuwaonyesha kuwa unaelewa msimamo wao kuhusu swala hili. Hii inawaonyesha kwamba unawaheshimu na uko tayari kuwaskiliza kikamilifu.
Unaweza kutambua desturi na imani zao na kuchukua muda wa kutafakari, ingawa maoni yako yanaweza kuwa kinyume kabisa.
Muhimu ni kuepuka mgongano usio wa lazima, au kujaribu kuwalazimisha kubadilika.
Lakini huenda bado unajiuliza: Tunawezaje kukabiliana na wazee wasiovutia? Je, ikiwa kutokuelewana kuna uzito zaidi kuliko mtazamo wako tofauti kuhusu chuo? Je, tunapaswa kuwaheshimu licha ya tabia zao? Na vipi?
Hebu tuone.
Namna ya kukabiliana na wazee wasiopendeka

Photo by Kindel Media
Ingawa inaweza kuwa vigumu kuwaheshimu wazee kama hawa, tunaweza bado kuwatendea kwa namna ambayo tungependa kutendewa tunapofanya makosa (Mathayo 7:12). Kwa kufanya hivyo, tunaushinda ubaya kwa wema (Warumi 12:21; Luka 6:27-29).
Hii haimaanishi kuwa tunakubaliana na ubinafsi, ukali au tabia zinazoumiza.
Lakini ikiwa tutalazimika kuishi na wazee ambao hawakubaliani nasi (na kuna uwezekano mkubwa kwamba tutakutana nao), hapa kuna mapendekezo yanayoweza kusaidia kupunguza hali mbalimbali.
- Kubali kwamba hata wazee wetu ni wanadamu wanaoweza kufanya makosa.
- Kubali kwamba imani zao zinatokana na uzoefu wao—hawashikilii maoni yao kiholela. Wakati mwingine wanaweza kuwa wanatamani tu kujisikia kuwa wanasikilizwa au kueleweka.
- Waulize kwa upole kwanini wana mtazamo tofauti katika mambo mbalimbali, au ni nini kinacho wakasirisha au kuwapa wasiwasi. Kisha ishi nao kwa namna inayoonesha heshima. Hii itawasaidia kutafakari upya mienendo yao na inaweza kuleta upatanisho.
- Katika baadhi ya mivutano mikali, kuondoka kwa heshima kunaweza kuwa njia bora ya kusaidia kupunguza mwingiliano.
- Kumbuka, tabia ya mtu mwingine haipaswi kuwa kisingizio cha tabia zetu mbaya. Hivyo usishushe viwango vyako vya maadili na kuathiri uadilifu wako kwa kufuata mfano wao katika hali hizi.
Upendo na heshima, hata kwa wazee wasiovutia, husaidia sana katika kuyeyusha mioyo yao. Inaweza kuchukua muda lakini italeta matokeo. Na Yesu Kristo ni mfano mzuri katika kugeuza hali mbaya kabisa kuwa fursa ya kuelewana (Waebrania 12:3; Mathayo 5:43-44; 22:15-22; 26:47-56; Yohana 8:1-11; 18:33-38).
Hebu tujaribu kadri tuwezavyo kuchukua hatua ya kuwa wema, wapole, wenye kujali, na wenye heshima kwa wote (Waefeso 4:32).
Lakini katika nyakati ambazo hata juhudi zetu bora hazifanyi kazi, hebu tukumbuke kwamba kuna nyakati ambapo tunaweza kuhitaji kwa heshima kuweka mipaka na wazee wetu.
Namna ya kuweka mipaka kati yetu na wazee
Kuna nyakati ambapo wazee, iwe ni wazazi au wale walio na mamlaka, wanaweza kuweka masharti au kupitisha sheria ambazo zinakandamiza haki au imani za wengine. Kwa kuweka mipaka ya kimaadili kati yetu nao, tunaweza kuwa na nafasi ya kusimama kwa kile kilicho sahihi.
Kwa mfano:
Tunaweza kufanya nini ikiwa wazee wetu wanataka tufanye mambo ambayo yanaweza kuumiza maisha yetu ya kiakili, kimwili, au kiroho?
Ili kupata Mawazo mapya, tunaweza kujifunza kutoka kwa watu wengine ambao wamepitia uzoefu kama huo katika siku za nyuma. Na Biblia ni nyenzo bora kwa ajili ya hilo.
Danieli akataa chakula cha mfalme
Danieli alikuwa kijana Mwebrania ambaye alichukuliwa kama mateka kwenda Babeli. Katika malezi yake ya Kiebrania, alifundishwa kanuni za Mungu za afya ambazo zilizowataka kula wanyama walio safi tu (Mambo ya Walawi 11; Kumbukumbu la Torati 14).
Hata hivyo, watekaji wake, Wababeli, “kama mataifa mengine ya kipagani, walikula wanyama najisi, wanyama hawakuwa wameuawa ipasavyo kulingana na sheria ya Kilawi (Mambo ya Walawi 17:14, 15), na sehemu ya wanyama waliokula ilitolewa kwanza kama dhabihu kwa miungu ya kipagani.”6
Na baadaye katika maisha yake, Danieli alikuwa mhudumu mafunzoni katika ikulu ya mfalme. Kama sehemu ya maandalizi yake, alipewa chakula kutoka kwenye meza ya mfalme (Danieli 1:1-5). Hata hivyo, aliamua kuwa ni bora kushikilia mipaka yake ya kiafya badala ya kufanya kitu kingine ambacho kingeathiri ustawi wake wa kiakili, kimwili, na kiroho.
Hivyo “Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa…” (Danieli 1:8, NKJV). Badala yake, aliiomba kwa heshima chakula chenye mboga, nafaka, na kunde, ambacho aliamini kingekuwa bora kwa ustawi wake wa kiakili na kimwili.
Zaidi ya hayo, alimwomba afisa wa mfalme kumjaribu afya na nguvu zake baada ya siku kumi za kula kwa chakula cha namna hii (Danieli 1:12-16).
Hivyo ingawa alionyesha kutokubaliana na afisa wa mfalme, ambaye alikuwa na mamlaka juu yake, alifanya hivyo kwa utulivu na heshima kwa kutoa mbadala ambao ungeweza kuwa na matokeo sawa (au bora) zaidi ya yale yaliyopendekezwa kwake.
Badala ya kukataa kwa jeuri chakula cha mfalme, alikigeuza kuwa fursa si tu ya kupendekeza mbadala, bali pia kumpa nafasi mtu mwenye mamlaka kujaribu mbadala wake.
Kanuni bora kwa ajili ya nyakati ngumu

Photo by Diva Plavalaguna
Katika kisa cha Danieli tunaweza kupata mfano mwingine mzuri, wakati amri ya mfalme mwingine ilipoingilia imani yake.
Kama mfuasi mwaminifu wa Mungu, Danieli alikuwa raia mwema. Hii ilipelekea mfalme kutaka kumteua kuwa msimamizi juu ya maafisa wengine wa ufalme. Hata hivyo, maafisa wengine walimshawishi mfalme kupitisha sheria ambayo ingekuwa kinyume na imani ya Danieli kwa Mungu pekee.
Amri hii mpya ilikataza aina yoyote ya ibada kwa yeyote isipokuwa mfalme. Hata hivyo, Danieli aliendelea kuomba kwa wazi kwa Mungu.
Lakini wakati Danieli aliposhtakiwa mbele ya mfalme kwa kukiuka mamlaka yake, mfalme alitambua kwamba Danieli alikuwa mfanyakazi mwaminifu na anayetimiza wajibu wake kwa miaka kadhaa na hakuwa na chuki dhidi yake. Kwa kweli, baadaye mfalme aliwaangamiza maafisa waliomdanganya kupitisha sheria hiyo (Danieli 6:1-28)!
Migogoro au kutokubalina kunaweza kushughulikiwa kwa urahisi zaidi ikiwa tayari tunafuata na kuheshimu mamlaka ya wazee katika njia zote ambazo haziingiliani na mipaka yetu.
Ikiwa wewe ni mwaminifu, mwenye heshima, na mtiifu kwa wazee wako katika mambo mengine yote, ni rahisi kujadili migogoro inapotokea. Kwa sababu tayari umejibainisha kama mwana jamii mwaminifu, hawatajisikia kama unaonyesha upinzani au uasi.
Petero na mitume na uamuzi wao wa kuwa waaminifu kwa Yesu
Tunaweza pia kuangalia jinsi Petro na mitume wengine walivyofungwa kwa sababu ya imani yao katika Yesu Kristo na baadaye kuamriwa wasihubiri habari zake. Viongozi wa kidini walidhani wangeweza kuwanyamazisha kwa vizuizi vyao.
Lakini je, mitume walikubali kutii vizuizi vyao?
Hapana.
Walijibu, “…Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu” (Matendo 5:29, NKJV).
Hivyo, inapofikia mambo ya dhamira na imani au uhuru, tunaweza kuhitaji kusimama kwa ajili ya kile kilicho sahihi. Na hii inaanza kwa kuweka wazi wazi mipaka kulingana na imani zetu za msingi.
Kwa ujumla, kuna faida kubwa kwetu na kwa wengine tunapoonyesha heshima kwa wazee wetu wakati wote.
Faida za kuwa na heshima
Kuwaheshimu wazee wetu kuna faida kwa yule anayetoa na anayepokea heshima.
Baadhi ya faida hizo ni:
Ukuaji binafsi
Kuheshimu wazee wetu kunachochea ukuaji binafsi. Tunajifunza kuwa na subira, kujidhibiti, na kuwa na uwezo wa kihisia kupitia kuheshimu wazee. Pia, tunapojisikia kuwa na manufaa kwa mtu fulani inakuza thamani yetu binafsi.
Kuwahudumia wengine pia kunakuza uwezo wa kujitolea, ambayo inatufanya kuridhika zaidi katika maisha. Inatuepusha na kuzingatia mambo yetu wenyewe tu—ambayo inaweza hata kusababisha wasiwasi na msongo ikiwa mara chache tunapanua mtazamo wetu kuwatazama pia wengine na mahitaji yao.7 Si ajabu Biblia inatutia moyo kutoangalia tu “…mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine” (Wafilipi 2:4, NKJV).
Kuifanya heshima kuwa ya kudumu kunajenga tabia njema, ikihusisha “hatima yetu kwa wakati huu na kwa ajili ya umilele.”8
Inaboresha afya ya akili
Kuishi kwa heshima na wazee wetu hukuza maisha yenye usawa na kuleta hisia za kuridhika na umuhimu, ambayo huboresha afya za akili zetu.
Kuwa tayari kujifunza kutoka kwao pia inatusaidia kukuza uwezo wa kufikiri na ujuzi wa kutatua matatizo, ambazo ni funguo za mafanikio katika maisha.9
Inakuza umoja
Faida nyingine ya heshima kwa wazee ni umoja. Kuheshimu wazee kunajenga daraja kati ya vizazi, kunakuza upendo, na kuimarisha umoja katika jamii. Kwa sababu upendo na heshima huleta mwitikio sawa kutoka kwa wapokeaji.10
Pia, kwa kuwaheshimu wazee wetu, tunaweka mfano mzuri kwa wale walio wadogo kwetu. Inawatia moyo kuthamini huruma, upendo, na wema.
Heshima kwa wazee bado ni muhimu
Kuheshimu wazee wetu kuna manufaa makubwa sana, huleta ukuaji na kuimarisha mahusiano. Kwa kuwa wema na wenye upendo kwa wale walio karibu nasi, hatuboreshi tu maisha yao, bali Maisha yetu pia.
Hivyo hata katika kizazi hiki, heshima kwa wazee wetu bado ni muhimu. Na hiyo ndiyo sababu ya Biblia kusisitiza umuhimu wake. Kuwa na adabu na uvumilivu hata kwa wale ambao si kila wakati wanastahili, tunaweza kuishinda mioyo yao na kukuza jamii iliyo na umoja.
Zaidi ya yote, tunahitaji wazee wetu katika miaka yetu ya ujana. Tunahitaji kuwaheshimu kwa ajili ya mchango walio nao katika maisha yetu.
Fikiria kuhusu wazee walio karibu na wewe na mahitaji yao. Kisha angalia namna unavyoweza kuwapa faraja na matumaini, na kutumia vyema kila wakati unaoupata kuwa pamoja nao.
- Respect, The Britannica Dictionary, https://www.britannica.com/dictionary/respect [↵]
- 1 Peter 2:13-17; Mark 12:17; Heb 13:17 [↵]
- Rule of Law and Human Rights, The United Nations, https://www.un.org/ruleoflaw/rule-of-law-and-human-rights/ [↵]
- “Older people offer resources that children need, Stanford report says,” Stanford Report, September 8th, 2016 https://news.stanford.edu/stories/2016/09/older-people-offer-resource-children-need-stanford-report-says [↵]
- Ibid. [↵]
- Nichol, Francis D., ed. 1977. The Seventh-Day Adventist Bible Commentary. Vol. 4. Review and Herald Publishing Association. [↵]
- Philippi, Carissa. The Relationship Between Self-Focus and Anxiety, University of Missouri-St Louis, https://irl.umsl.edu/urs/39/ [↵]
- White, G. Ellen, Christ’s Object Lessons, (Review and Herald Publishing House, 1900), p. 356 [↵]
- Stanford Report [↵]
- Price-Mitchell, Marilyn Ph.D., The Language of Respect: Walking our talk with teenagers. Psychology Today, February 10, 2014
https://www.psychologytoday.com/us/blog/the-moment-of-youth/201402/the-language-of-respect [↵]