Aya 10 katika Biblia za kukusaidia unapohisi kukata tamaa
Ni kawaida kuhisi kuvunjika moyo unapopitia matatizo binafsi au ya kifamilia, mashaka, kushindwa kufikia malengo, kulemewa na majukumu, kuvunjwa moyo, ukosefu wa fedha wa kulipia mahitaji yako, kufeli mtihani, au kuvunjika kwa mahusiano.
Mambo haya yote yanaweza kukuchosha kiakili na kimwili, na mara nyingine kuhisi kama huwezi kusonga mbele tena.
Katika nyakati ngumu kama hizo, Biblia huwa kimbilio letu la faraja na matumaini.
Neno la Mungu linatoa ukumbusho wenye nguvu kuhusu upendo Wake, uaminifu Wake, na nguvu Zake.
Tunafahamu kuwa Mungu ana mamlaka juu ya kila kitu, na anatujali sisi pamoja na changamoto tunazo pitia. Yeye hutamani tuwe na amani ya moyo katika kila hali, haijalishi ni ngumu kiasi gani.
Basi hebu tujifunze zaidi kuhusu:
- Jinsi Mungu alivowatia moyo watu Wake katika Maandiko
- Aya za Biblia za kukutia moyo unapohisi kuvunjika moyo
- Jinsi ya kumtumaini Mungu katika nyakati ngumu za maisha
Tutaanza kwa kuchunguza jinsi Mungu alivowatia moyo watu Wake katika Biblia.
Jinsi Mungu alivowatia moyo watu Wake katika Maandiko

Photo by Aaron Owens on Unsplash
Mara nyingi Biblia inaonyesha nyakati ambapo watu wa Mungu walikutana na changamoto. Hebu tuchunguze jinsi Yoshua, Daudi, na Ayubu walivyopata tumaini wakati wa majaribu.
Ahadi ya Mungu ya ushindi kwa Yoshua (Yoshua 7-8)
Baada ya Israeli kushindwa na mji wa Ai, watu walivunjika moyo.
Yoshua alimgeukia Mungu ili apate mwongozo, na Mungu alimwambia akusanye tena watu na kutambua makosa waliyoifanya mbele za Mungu kwa kutotii uongozi Wake.
Kisha, Mungu alimwambia Yoshua, asijali wala kukata tamaa, akimuhakikishia kwamba tayari alikua ameandaa njia ya kuwashinda adui hawa watakapokutana nao tena.
Kwa kufuata agizo la Bwana, Yoshua aligawanya sehemu ya jeshi lake na kuwatuma kujifanya kuwa wanakimbia kutoka Ai ili kuwavuta maadui watoke nje ya mji. Wakati huo, kundi lingine la Waisraeli lilivamia na kuchukua mji.
Wanajeshi wa Ai, walipokuwa wakiwafuatilia Waisraeli waliokimbia, walijikuta wamezungukwa, na kusababisha ushindi wa Israeli.
Daudi alitiwa moyo wakati wa matatizo ya kifamilia (2 Samweli 15-16)
Daudi, mtu aliyependwa sana na Mungu, alikuwa mfalme wa Israeli. Baada ya shida kubwa za kifamilia, mwanawe Daudi, Absalomu, aliasi na kujaribu kuchukua ufalme kutoka kwake.
Akiwa amekata tamaa na kujawa na huzuni, Daudi alilazimika kukimbia na kujificha, na mwishowe kuandaa vita dhidi ya mwanawe na jeshi lake.
Hata hivyo, Daudi hakuwa peke yake katika kipindi hiki cha maumivu na usaliti. Alijifunza masomo magumu na akamgeukia Mungu, na ingawa matukio haya ya huzuni hayakuweza kufutwa, Mungu alirejesha mustakabali wa Daudi na kumrudishia ufalme wake.
Ayubu alipoteza kila kitu lakini alipata zaidi (Ayubu 1-2, 42)
Labda hakuna mtu mwingine katika Biblia (isipokuwa Yesu) aliye pitia magumu mengi ya kukatisha tamaa kama Ayubu. Katika siku moja, alipoteza Watoto wake aliowapenda sana, na alipoteza mali na vitu vyote alivyokuwa navyo.
Alipoteza hata afya yake, alipata majipu yenye maumivu mwili mzima na hata mkewe alimshauri amlaani Mungu ili afe. Hata hivyo, katika yote haya, alimlilia
Mungu katika maombi ili kupata msaada, akimwambia uchungu na huzuni zake zote.
Hatimaye, Mungu alimjalia baraka nyingi zaidi, akazidisha mara mbili mali zake na kumpa nafasi nyingine ya kujenga familia. Mwisho wake ulikuwa bora zaidi kuliko mwanzo wake.
Mifano hii inaonyesha jinsi Mungu anavyowatia moyo watu Wake katika nyakati ngumu. Hebu pia tugeukie neno la Mungu, ambalo hututia moyo na kufunua tabia ya Yesu kama rafiki wa kuaminika ambaye kweli anatujali.
Mungu aliyewasaidia mashujaa wa Biblia anaweza kutusaidia leo.
Aya katika Biblia za kukutia moyo unapohisi kuvunjika moyo
Kila siku huja na changamoto na vikwazo vyake. Maisha huweza kutuletea matatizo yasiyotarajiwa, lakini jinsi tunavyo chukuliana na hali ndiyo huamua safari yetu ya maisha. Hata sasa, huenda unahisi kama unabeba mzigo wa dunia mabegani mwako, na kwamba hakuna mtu wa kukusaidia.
Iwe ni msongo wa mawazo, kukatishwa tamaa, au kupoteza kitu, nyakati hizi huacha mtu akiwa na huzuni na wasiwasi. Lakini habari njema ni kwamba hauko peke yako.
Hapa kuna baadhi ya aya katika Biblia kutoka tafsiri ya NKJV zinazotukumbusha kwamba Mungu yupo pamoja nasi, anatujali kwa kina, na anataka kutusaidia kupitia changamoto zetu. Anaona magumu tunayopitia na anatusaidia katika nyakati zetu ngumu:
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”
Maelezo: Maneno haya yalielekezwa kwa Wayahudi walipokuwa mateka Babeli. Kama wao, huenda nawe unajihisi umenaswa na hali ngumu au ushawishi mbaya kama mahusiano mabaya, madeni, uraibu, n.k. Ingawa dunia inatarajia uanguke, nia ya Mungu kwako ni njema daima kuleta tumaini, uzima, na mustakabali uliojaa nuru.
2. Yoshua 1:9
“Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
Maelezo: Ingawa Yoshua alipitia mambo magumu sana, kilichompa ushindi kama kiongozi ilikuwa ni uamuzi wake wa kumruhusu Mungu amuongoze. Hili ni somo muhimu kwetu kwamba hakuna uchungu au changamoto inayotupata ambayo Mungu haoni, yupo pamoja nasi na anatamani kutusaidia kila hatua.
3. Zaburi 27:3, 5
“Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”…“Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”
Maelezo: Kama Daudi, mara nyingine tunajikuta tumezungukwa na maadui wa kila aina. Wapo wanaotusema vibaya, wanaotuonea wivu, au hata wanaoweza kutudhuru ili kupata wanachotaka. Lakini hata katika hali mbaya zaidi, tunaweza kukumbuka kuwa Mungu yupo pamoja nasi na hatatuacha kamwe. Yeye ni ngao na mlinzi wetu.
4. Zaburi 34:17-18
“Walilia, naye BWANA akasikia, Akawaponya kutoka kwa taabu zao zote.
BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.”
Maelezo: Maisha yanaweza kuwa magumu na kujaa maumivu na huzuni, na mara nyingine tunajikuta tumepotea au kuvunjika moyo. Hata hivyo, kama Daudi alivyofanya, tunapomgeukia Mungu kwa maombi, Yeye huwa tayari kutuinua, kutuponya, kutufariji, na kuturejeshea amani ya kweli.
5. Isaya 41:10
“usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Maelezo: Wakazi wa Yuda mara nyingi walimkataa na kumwacha Mungu, lakini Yeye hakuwahi kuwaacha. Hivyo basi, hata kama tumefanya makosa mengi au maamuzi mabaya, hatupaswi kuwa na wasiwasi kwamba Mungu ametutupa. Tukimtafuta, Yeye hutufikia pia. Na huwa na hamu ya kuwasaidia wote wanaomwomba msaada na nguvu.
6. Mathayo 11:28
“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”
Maelezo: Haijalishi ni magumu au mashaka gani tunayokabiliana nayo, tunahimizwa kumweleza Mungu kila kitu. Kadri tunavyojisikia wanyonge na wasio na msaada, ndivyo tunavyoweza kutambua nguvu zake. Kadri mizigo yetu inavyokuwa mizito, ndivyo baraka ya kupumzika kwa kuyatwika kwa Mchukua Mizigo wetu wa mbinguni inavyokuwa ya thamani zaidi.
7. Yohana14:1-3
“Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.”
Maelezo: Maneno haya ya Yesu yanatualika tumwamini Mungu kuliko hali tunazopitia. Yesu anatuambia kuwa Anatuandalia makao, ambapo tutapata amani na pumziko. Haijalishi majaribu tunayokutana nayo hapa duniani, tuna hakika ya makao ya milele yenye amani.
8. Yohana 16:33
“Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”
Maelezo: Kama Wakristo, tuna ahadi ya wokovu na uzima wa milele. Lakini maisha hapa duniani iliyojaa dhambi yataendelea kuwa na changamoto. Habari njema ni kwamba hatupaswi kuruhusu majaribu haya kututawala, kwani Mungu yupo pamoja nasi hata katikati ya haya yote, na atatusaidia kutoka tukiwa na nguvu zaidi.
Maneno ya Yesu si tu ahadi ya amani, bali pia ni ukumbusho kwamba matatizo tunayopitia si hatima ya maisha yetu. Kwa kuwa Yeye alishinda kila kitu kwa ajili yetu, ana uwezo wa kutusaidia kushinda kila jambo tunalokutana nalo.
9. 1 Wakorintho 15:51-52
“Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.”
Maelezo: Ni kawaida kuwa na wasiwasi kuhusu maisha ya baadaye, hasa baada ya kifo. Paulo anatupa mwanga kidogo juu ya fumbo hili lenye utukufu. Waliokufa wakiwa ndani ya Kristo watafufuliwa, pamoja na wenye haki walio hai, watapokea miili isiyoharibika Yesu atakaporudi. Kisha, tutaishi naye milele katika mbingu na Dunia Mpya bila mateso tena (1 Wathesalonike 4:16-17).
Hii ni ahadi kwamba wale wanaomfuata Mungu watapata uzima wa milele usioharibika pamoja naye.
10. Wafilipi 4:6-7
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Maelezo: Ni rahisi sana kuwa na wasiwasi kuhusu maisha ya baadaye, mambo tusiyoweza kuyadhibiti, na misukosuko ya kila siku isiyo na mwisho. Badala ya kubeba mizigo yetu peke yetu, Paulo anatukumbusha tumgeukie Mungu na mahangaiko yetu (Zaburi 55:22), tukimletea kwa maombi. Kwa kufanya hivyo, tunapokea amani inayopita ufahamu wetu. Tunapomkabidhi Mungu wasiwasi wetu, tunayaachilia kutoka akilini mwetu na hatuendelei kuyafikiria tena, naye anatupatia utulivu na faraja.
Bado kuna tumaini

Photo by Pixabay
Kupitia Yesu, Mwana wa Mungu, kuna tumaini kwa kila mmoja wetu (Yohana 3:16). Ukimkaribia kwa maombi (Mathayo 6:9-13), na kudai ahadi hizi za Biblia, utapata amani. Ukimkabidhi maisha yako leo, utapata maisha ya furaha kupitia Yeye atupaye amani ya kweli.
Maneno ya Yesu katika injili (Mathayo, Marko, Luka, Yohana) yanatuhakikishia kwamba:
- Wasiwasi hauna uwezo wa kutabiri yajayo, lakini Yesu anaona kila kitu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
- Katika kila gumu, Yesu tayari ameandaa njia ya kutuletea faraja.
- Baba yetu wa mbinguni ana njia zisizo na idadi za kututunza, nyingi ambazo hatujui.
- Wale wanaomtanguliza Mungu kuwa wa kwanza huona shida zao na wasiwasi vikififia na njia ikifunguka.
Tunakuhimiza kuzifanya ahadi hizi kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku.
Iwe kupitia:
- Masomo kuhusu ahadi za Mungu
- Kutafakari hadithi za Biblia za tumaini
- Kusoma na kutafakari Biblia wewe binafsi pamoja na watu wengine, mkiambatana na kushirikiana katika uzoefu wa kiroho unaotia moyo.
- Kusali kwa unyenyekevu huku ukiwasilisha haja zako mbele za Mungu.
Utaweza kumjua Yesu Kristo kwa undani zaidi na kufurahia uhusiano wa karibu naye, Yeye anayetoa tumaini na amani. Ukitafakari ahadi hizi na kumruhusu Roho Mtakatifu aziweke ndani ya mioyo yetu, tutapata faraja na utulivu wa kweli.
Unaweza kupata faraja kwa kuchunguza ukurasa huu ikiwa una wasiwasi, hofu, au mashaka.
Hauko peke yako katika safari hii. Ukurasa huu unaonyesha jinsi Biblia inaweza kutoa tumaini wakati wa nyakati ngumu.
Pia, tazama video ya kuhamasisha, jinsi ya kumtumainia Mungu wakati wa nyakati ngumu za maisha. Tunatumaini italeta faraja na tumaini moyoni mwako.
Video
Jinsi ya kumwamini Mungu katika nyakati ngumu za maisha –
Katika video hii, Mchungaji Mark Finley anaeleza kanuni za kibiblia zinazogusa moyo zikilenga kutuinua wakati wa wasiwasi, hofu, na woga. Gundua namna ya kupata amani na nguvu kupitia maarifa yake yenye nguvu.
Mada na aya hukusanywa kutoka nyenzo mbalimbali na kupitiwa na timu yetu. Ikiwa aya au mada haifai au haipo, tafadhali wasiliana nasi. Maandiko yamechukuliwa kutoka Toleo la New King James®. Hakimiliki © 1982 na Thomas Nelson. Limetumika kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa.
Sehemu ya Maoni
Tunathamini sana mawazo na uzoefu wako. Tungependa kujua ni mbinu zipi unatumia kumtegemea Mungu kwa faraja unapokabili nyakati ngumu. Tafadhali jisikie huru kuchangia maoni yako pamoja nasi.
Majadiliano yanaratibiwa. Tafadhali soma Sera Yetu ya Maoni.