Aya za Biblia za Kutia Moyo Wakati wa Mitihani
Ni jambo la kawaida kuhisi wasiwasi unapojiandaa kufanya mitihani mikubwa, au kazi yoyote inayohitaji kutathmini kile ulichofanya. Lakini pale ambapo hisia za msongo wa mawazo zinapozidi, fahamu kuwa Biblia inatoa ushauri na faraja ya kukusaidia kufanikisha mambo magumu yanayokukabili.
Hii haimaanishi kwamba kusoma si jambo la msingi zaidi katika maandalizi ya mitihani. Biblia inafundisha umuhimu wa kujiandaa. Lakini wakati mwingine tunakumbwa na wasiwasi usio na manufaa tunapokutana na changamoto inayotathmini mafanikio yetu au kushindwa.
Hebu tuangalie aya kadhaa za Biblia zinazoweza kukutia moyo na kukupa mtazamo mpana unapokuwa na wasiwasi au msongo wa maandalizi ya mtihani.
Tutajadili:
- Nyakati ambazo Mungu alitoa hekima kwa watu katika Biblia.
- Aya za Biblia zinazozungumzia kukua katika hekima na elimu
- Hamasa ya kujifunza
Tuanze kwa kuona jinsi Mungu huwa anawapa maarifa wale wanaoyatafuta kwa moyo wote.
Nyakati ambazo Mungu alitoa hekima kwa watu katika Biblia
Biblia inaonyesha mara nyingi jinsi Mungu alivyoingilia kati kuwasaidia watu kwa kuwapa hekima, motisha, na msaada iwe walihitaji au walitafuta kwa moyo.
Uaminifu wake wa zamani unatupa sababu ya kumtumaini leo kwa mahitaji kama hayo. Kama ambavyo watoto hujifunza kumtumaini mzazi kutokana na uaminifu wa mara kwa mara, ndivyo nasi tunavyopata msingi wa imani yetu kwa Mungu kutokana na uaminifu wake wa siku za nyuma.
Ombi la hekima la Suleimani

Photo by Nitin Arya
Baada ya kumrithi baba yake Daudi kama Mfalme wa Israeli, Bwana alimuahidi Sulemani kumpa chochote atakachoomba. Badala ya kuomba utajiri, mamlaka, au maisha marefu, aliomba hekima.
Mungu alipendezwa na jibu la Sulemani:
“Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote” (1 Wafalme 3:10-13, NKJV).
Mungu alimpa Sulemani hekima kama alivyo-omba, na pamoja na hilo, alimpa pia kila kitu chengine alichohitaji ili kufanikisha uongozi wake. Kutokana na kisa cha Sulemani, tunajifunza kwamba Mungu hatoi tu hekima, bali hufurahia kutupatia hekima. Anataka tumwombe msaada Wake, kwa kuwa hekima ni jambo la maana machoni pake.
Mungu aliwafanya Danieli na rafiki zake kuwa “mara kumi bora zaidi”
Danieli na rafiki zake watatu—Hanania, Mishaeli, na Azaria—walikuwa miongoni mwa Waisraeli waliotekwa mateka na kupelekwa utumwani Babeli.
Mfalme Nebukadneza alichagua baadhi ya vijana hao ili wapewe mafunzo maalumu yaliyokusudiwa kuwaandaa kwa ajili ya kuhudumu katika ikulu ya kifalme.
Mafunzo hayo yaliwalazimisha Danieli na rafiki zake watatu kufanya uchaguzi mgumu kati ya kufuata mwongozo ya Mungu kuhusu afya, au kujitosa katika matumizi ya chakula na mazoea ya Babeli ambayo yangewaharibu kiroho.
“Lakini Danieli aliazimia moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi” (Danieli 1:8, NKJV).
Kwa sababu ya dhamira ya dhati ya Danieli ya kumtii Bwana, Mungu alikubali ombi lao na kuwapa kibali na huruma kutoka kwa mkuu wa matowashi, ambaye alikubali maombi yao.
Biblia inasema kwamba,
“Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto” (Danieli 1:17, NKJV).
Mwisho wa mafunzo, Biblia inasema hivi:
“Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake” (Danieli 1:19-20, NKJV).
Vivyo hivyo, kufuata njia ya Mungu ya mafanikio—ambayo inahusiana kwa karibu na maisha ya kujitolea na kufanya mapenzi Yake—kunaweza kutufanya kuwa bora mara kumi zaidi.
Mungu alimpa Yusufu hekima katika nyakati ngumu
Licha ya kujitoa kwake kwa uaminifu na kuishi kwa uadilifu, Yusufu alikumbana na hali ngumu sana.
Mke wa Potifa, ambaye alikuwa bwana wake, alimtamani sana na alimshawishi mara kwa mara ili alale naye. Hata baada ya kumsisitiza sana, Yusufu alikataa kuzini naye. Kwa hasira na chuki, mwanamke huyo alimwekea mtego na kumzushia Yusufu shtaka la uongo, akidai kwamba alitaka kumbaka.
Yusufu aliwekwa gerezani, na hali yake ilionekana kuwa ya kukatisha tamaa kabisa—akiwa sasa ni mtumwa na pia mfungwa. Lakini Mungu aliingilia kati na kubadilisha kila kitu.
Mungu alimjalia Yusufu kipawa cha kutafsiri ndoto, na aliweza kufafanua ndoto ya Farao iliyokuwa ikimsumbua. Kupitia hili, Mungu alimuandalia njia ya kutoka jela na kuingia katika ikulu, kwani Farao alikiri, “Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe” (Mwanzo 41:39, NKJV).
Hekima na mwongozo wa Mungu vilifanya Yusufu apandishwe cheo na Potifa, ambaye alimweka kuwa msimamizi wa kila kitu katika nyumba yake. Mungu alimtoa gerezani na pia akamfanya ajulikane mbele ya Farao.
Mifano hii yote, pamoja na mingine mingi, ni ushahidi kwamba Mungu hujitokeza kutusaidia kila tunapohitaji msaada Wake. Hakuna jambo kubwa sana au dogo sana lisilostahili uangalizi wake. Tunapomtafuta Mungu kwa maombi, huku tukifanya kazi kwa bidii, tunaweza kuwa na uhakika kwamba atatusaidia.
Hebu sasa tuangalie baadhi ya mafungu ya Biblia yanayozungumzia kukua katika hekima na maarifa.
Aya za Biblia zinazohusu kukua katika hekima na maarifa
Kuna aya nyingi katika Biblia zinazotuhakikishia kuwa Mungu atatuongoza na kutupa maarifa na hekima. Ahadi hizi zote ni za kweli hadi leo, na tunaweza kuzidai kwa imani. Hapa kuna baadhi ya mafungu ya Biblia ya kusisimua (yote kutoka tafsiri ya NKJV) kuhusu jinsi Mungu anavyotoa hekima na maarifa:
Zaburi 16:7
“Nitamhimidi BWANA aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.”
Maelezo: Mungu ndiye chanzo cha hekima na ushauri ulio bora.
Zaburi 119:105
“Neno lako ni taa kwa miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”
Maelezo: Neno la Mungu litakuongoza kujua kile unachopaswa kufanya katika kila hatua. Ingawa Mungu hawezi kutupa maelezo ya kila hatua, tunaweza kuwa na uhakika kwamba Atatuongoza na hata tutakapokutana na changamoto, hatatuacha.
Zaburi 138:8
“BWANA atanitimilizia mambo yangu; Ee BWANA, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.”
Maelezo: Bwana atashughulikia mashaka yetu. Hatatuacha ili tukabiliane na matatizo yetu peke yetu.
Joshua 1:8
“Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawa sawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”
Maelezo: Kama vile tukiazimia kusoma Maandiko kwa bidii kutatuletea mafanikio ya kiroho, Vivyo hivyo tukiwa na bidii katika masomo pia utatuletea mafanikio. Aidha, kujifunza Neno la Mungu kutatufanya kuwa na uwezo mkubwa wa kujifunza mambo mengine.1
Isaiah 41:10
“usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Maelezo: Uwepo wa Mungu upo ili kukutia nguvu na kukupa ujasiri wa kukabiliana na changamoto—kama vile wasiwasi wa mitihani na hofu ya kushindwa—bila hofu.
Jeremiah 29:11
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”
Maelezo: Mungu anajua vizuri kile anachofanya. Unaweza kumwamini kwa hekima Yake hata wakati hali inapoonekana kutokuwa wazi. Hata unapojisikia umejaa wasiwasi, Mungu ana mpango kwako. Atakuongoza mahali anapotaka ufike. Hakuna jambo litakalosimama mbele ya mipango Yake kwako kadri utakavyomruhusu Mungu kukuongoza.
Danieli 1:17
“Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto.”
Maelezo: Baraka za kipekee za Mungu zinapatikana kwa wale ambao wamejizatiti kuishi maisha ya maombi na ibada kila wakati, wakitafuta kuishi kulingana na mapenzi Yake aliyoyadhihirisha.
Mathayo 6:33
“Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Maelezo: Tunapomtanguliza Mungu, Yeye anafurahia kutupatia kila tunachohitaji ili tuweze kufanikiwa mbele ya kila changamoto itakayokuja kwetu, ikiwa ni pamoja na kutupatia hekima.
Yohana 14:26
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”
Maelezo: Roho Mtakatifu daima yupo tayari kutusaidia kuimarisha akili zetu na tabia zetu.
Yakobo 1:5
“Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”
Maelezo: Hekima ya Mungu inapatikana kwa wingi kwa yeyote anayemuomba kwa imani. Mungu anasubiri tu tuombe. Hakuna kitu anachokipenda zaidi ya kutusaidia.
Wafilipi 4:6-7
“Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Maelezo: Tunapohisi wasiwasi, Mungu anataka tuende kwake ili atupatie amani ya kweli, inayodumu, na hakikisho lisilopatikana kokote. Anajua madhara ya wasiwasi na anataka kutusaidia kuushinda.
Wakolosai 3:16
“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”
Maelezo: Neno la Kristo ndani yako—kusoma na kukariri Maandiko—kutakufanya uwe na hekima.
1 Wakorintho 2:12
“Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.”
Maelezo: Roho Mtakatifu hutusaidia kupokea hekima kutoka kwa Mungu.
Msukumo wa Kusoma kwa Bidii

Photo by Makmot Robin on Unsplash
Kwa Wakristo, ubora ni zaidi ya kupata alama nzuri darasani. Tunaweza kupata alama nzuri lakini bado tukakosa kufikia uwezekano wa kiungu uliowekwa kwa ajili yetu. Mafanikio ya kweli yanahusiana sana na kufanya tuwezalo kwa bidii na kumwamini Mungu atufanyie yale tusiyoweza kuyafanya sisi wenyewe.
Ni muhimu kukumbuka kwamba Mungu anajali mahitaji yetu na anaweza kuimarisha juhudi zetu za kujisomea na kutupa amani tunapokuwa na wasiwasi kuhusu kufanya vizuri.
Ikiwa tunatamani hekima na ufahamu, na tukafanya sehemu yetu kwa uaminifu na bidii, Mungu atatupa kile tunachohitaji. Na hata kama tumefanya makosa, tunaweza kurejesha fursa tulizopoteza, au kupata mpya, kwa kupitia Kristo atutiaye nguvu.
Kuna vifungu vingi vyenye nguvu katika Biblia vinavyotukumbusha kwamba Mungu hataimarisha tu ufahamu wetu, bali pia ataongoza maamuzi yetu.
Tukifuata ushauri wa Biblia—kufanya kazi kwa bidii, kujiandaa kikamilifu, na kisha kumwachia Mungu yaliyobaki—tunaweza kwenda kwa ujasiri tukijua kwamba Mungu atatusaidia kushinda changamoto zozote tutakazokutana nazo.
Video kuhusu jinsi Biblia inatutia moyo wakati wa maandalizi ya mtihani
Kichwa: Aya za Biblia kuhusu kusoma kwa bidii na maandalizi kwa mafanikio katika mtihani
Muhtasari: Video hii inakupatia aya za Biblia zinazokutia moyo, zikikupa ujasiri na uhakika unapojiandaa kwa ajili ya mitihani.
- Cartwright, Kelly. (2001). Cognitive Developmental Theory and Spiritual Development. Journal of Adult Development. 8. 213-220. 10.1023/A:1011386427919. https://www.researchgate.net/publication/225987547_Cognitive_Developmental_Theory_and_Spiritual_Development
Jiunge na mazungumzo
Hapa ndipo unaweza kutoa mchango wako kuhusu mada hii. Changia kwa kutoa mawazo yako kuhusu aya za Biblia zinazoweza kukutia moyo wakati wa maandalizi ya mtihani
Mazungumzo yanadhibitiwa. Tafadhali soma Sera Yetu ya Maoni.