Biblia Inasemaje Kuhusu Maisha katika Siku za Mwisho?
Vita, magonjwa ya mlipuko, majanga ya asili, kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili…
Tunapoona mambo haya yakitokea, mara nyingi tunabaki tukijiuliza ikiwa tunashuhudia nyakati za mwisho za historia ya dunia.
Tangu katika unabii wa kale mpaka katika utabiri wa kisasa, swali limedumu kizazi na kizazi: Je, tunaishi katika siku za mwisho?
Kwa wengi wanaotafuta kujua mambo kupitia mtandao, hasa katika misimu isiyo na uhakika, huu siyo udadisi wa kitheolojia tu—ni swali binafsi la kina lililojikita katika hofu, kuchanganyikiwa, na kutafuta maana.
Katika makala hii, tutaangalia kile ambacho Biblia inasema kuhusu siku za mwisho—siyo kupitia vichwa vya habari vya kusisimua au nadharia, bali kupitia uchunguzi makini wa maandiko, wenye msawaziko na uliojaa matumaini.
Utajifunza:
- Kile Biblia inachoeleza kama “siku za mwisho”
- Dalili kuu na alama za kinabii za siku za mwisho
- Namna Yesu anavyoeleza siku za mwisho katika Mathayo 24
- Nafasi ya maandalizi binafsi na ukuaji wa kiroho
- Kwa nini unabii wa Biblia unatupatia tumaini, si maonyo tu
Makala hii ni kwa ajili yako ikiwa wewe au mtu unayempenda amekuwa ukijiuliza maswali haya moyoni mwako. Hebu tugeukie Biblia ili kupata majibu ya kweli, mwongozo unaofaa, na amani iliyofanywa upya kuhusu wakati ujao.
“Siku za mwisho” kulingana na Biblia ni zipi?
Maneno “siku za mwisho” yanaonekana mara kadhaa katika Biblia, yakielekeza kwenye kipindi tofauti cha historia ya mwanadamu ambacho kinaashiria kukaribia kwa ujio wa pili wa Kristo.
Tangu wakati wa mitume hadi sasa, Wakristo wameamini tuko katika “siku za mwisho,” au kile ambacho wanatheolojia wengi hukiita kipindi cha eskatologia.
Kulingana na kitabu cha Waebrania, “Mungu …siku hizi amenenena nasi katika Mwana” (Waebrania 1:1-2 NKJV), ikituonyesha kwamba kipindi cha kati ya ujio wa kwanza na wa pili wa Yesu zinaweza kutambulika kama siku za mwisho.
Lakini kwa kweli hicho ni kipindi kirefu sana cha wakati. Kwa hivyo hii inamaanisha nini?
Biblia haitaji tarehe halisi, kwa sababu sio lengo lake. Unabii wa wakati wa mwisho unatuambia kuhusu maendeleo ya ulimwengu—sio kipima muda cha kuisha kwake. Inakusudiwa kututayarisha sisi kuelewa nyakati kupitia matukio ya ulimwengu na hali za kiroho. Kupitia unabii wa Biblia, waamini wanaitwa kuwa makini badala ya kufanya makisio, kulingana na maneno ya Yesu.
Kwa hiyo, tunawezaje kutambua “siku za mwisho” tunapoishi ndani yake?
Dalili za siku za mwisho katika Biblia
Njia rahisi zaidi ni kupitia kutazama dalili zinazotajwa katika Biblia.
Biblia ilitabiri mfululizo wa matukio yatakayotokea ulimwenguni kote ambayo yangeonyesha nyakati za mwisho. Nyingi kati ya hizi zinaweza kupatikana katika kitabu cha Ufunuo, katika unabii wa Danieli, na hasa katika Mathayo 24, ambapo Yesu anaeleza nini tunachopaswa kutarajiwa.
Hapa kuna baadhi ya dalili kuu za mwisho kulingana na Maandiko:
- Vita na uvumi wa vita (Mathayo 24:6).
- Njaa, tauni na matetemeko ya ardhi (Mathayo 24:7).
- Kuongezeka kwa uasi (ubinafsi) na kupungua kwa upendo (Mathayo 24:12).
- Udanganyifu ulioenea na manabii wa uongo (Mathayo 24:11).
- Kuongezeka kwa maarifa na kusafiri (Danieli 12:4).
Watu wanapouliza ikiwa matukio yanayotokea sasa yanaashiria mwisho, mara nyingi huelekeza dalili hizi. Ingawa hali hizi zimekuwepo ulimwenguni kwa karne nyingi, Biblia hututia moyo kuziona kama uchungu wa kuzaa—unaoongezeka kadiri ujio wa pili wa Kristo unavyo karibia.
Hebu sasa tugeukie mafundisho ya moja kwa moja kutoka kwa Yesu Mwenyewe.
Maneno ya Yesu mwenyewe: Ufafanuzi wa Mathayo 24
Mathayo 24 ni miongoni mwa sura zilizo wazi zaidi kati ya sura zote za Biblia zinazohusu nyakati za mwisho. Yesu alitoa hubiri la kina akijibu swali la wanafunzi wake kuhusu siku za mwisho:
“Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?’” ( Mathayo 24:3, NKJV).
Katika sura hii, Yesu anaeleza sio tu majanga ya asili au machafuko ya kisiasa, lakini matukio ya kiroho ambayo yangeashiria siku za mwisho:
- Mkanganyiko wa kidini: Wengi wangekuja wakidai kumwakilisha Kristo, wakikusudia kuwadanganya watu (aya ya 5).
- Mateso ya waumini: Kanisa lingekabiliana na uadui, ugumu, na usaliti kutoka kwa wale walio upande wa ulimwengu badala ya upande wa Mungu (Aya ya 9-10).
- Injili ya Milele: Katikati ya machafuko, tumaini moja kuu limesalia—“Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14, NKJV).
Hii ndiyo hatua ya mwisho muhimu zaidi.
Ingawa misiba inazingatiwa zaidi, Yesu anakazia kutangazwa kwa injili ulimwenguni kote kama kiashiria cha wazi zaidi kwamba mwisho umekaribia. Hii inapatana na picha katika kitabu cha Ufunuo inayoonesha malaika wakitangaza injili ya milele kwa wakazi wote wa dunia (Ufunuo 14:6).
Kwa kuzingatia dalili hizi zote na maonyo ya moja kwa moja ya Yesu, swali la msingi lifuatalo ni: tufanye nini kuhusu hilo?
Je, tunapaswa kujiandaa vipi? Wito wa kuwa tayari
Tukijua kwamba tunaishi katika nyakati ambazo Biblia ilizungumzia si wito wa kuwa na hofu, bali ni wito wa kujiandaa. Maneno ya Yesu yanatuhimiza kujihadhari, kuwa macho kiroho, na watendakazi katika kueneza injili. Lengo la unabii siyo kuleta hofu kamwe—ni kuishi kwa uaminifu.
Hivi ndivyo tunavyoweza kuitikia unabii wa Biblia leo:
- Imarisha uhusiano wako na Mungu: Maombi, kujifunza Biblia, na jumuika pamoja na waumini wengine huimarisha imani yetu
- Ishi ukitambua ujio wa haraka wa Yesu, sio kwa wasiwasi: Acha kurudi kwa Kristo kuchochee upendo na huduma yako.
- Shiriki injili kwa ujasiri: Huu ni wakati wa kuhubiri injili, siyo kubahatisha au kujiondoa
- Uwe na hekima: Nadharia kuhusu siku zijazo zinapojitokeza, rudi kwenye Maandiko—sio mitandao ya kijamii—ili kupata ukweli.
Ingawa hakuna ajuaye wakati halisi, tunaitwa “kujua majira” (Warumi 13:11). Utimizo wa unabii wa Biblia unapoendelea, sasa ndio wakati wa kuchagua imani badala ya hofu.
Hatimaye, tumalizie Biblia inapoishia—kwa matumaini.
Kwa nini ujumbe kuhusu siku za mwisho unahusu tumaini

Photo by Marc-Olivier Jodoin on Unsplash
Katika misukosuko yote na matukio yanayotokea ulimwenguni kote, Biblia inatupatia mtazamo tofauti kabisa: tumaini.
Yajayo yanafurahisha.
Ingawa baadhi wanaweza kuonyesha hali ya siku za mwisho wakijikita katika uharibifu, Habari kuhusu siku za mwisho inahusu ukombozi.
Kitu pekee kitakachoangamizwa kabisa ni: uovu wenyewe.
Katika Ufunuo, tunaona si tu hukumu dhidi ya nguvu zinazo kandamiza na kutesa wanadamu, lakini kuinuka kwa ulimwengu mpya—ambapo dhambi, mateso, na kifo havipo tena ( Ufunuo 21:1-4 ).
Ndiyo, kutakuwa na wakati wa dhiki kuu, na ndiyo, ulimwengu utabadilika sana. Lakini ujumbe mkuu ni kwamba Yesu anakuja tena kufanya mambo yote kuwa mapya. Kama waumini, hatuangalii tu utabiri; tunatazamia ahadi: ujio wa pili wa Kristo.
Kwa hiyo, je, tunaishi katika nyakati za mwisho? Kulingana na Biblia, ndiyo ni kweli. Lakini muhimu zaidi, tunaishi katika siku za fursa—kukua, kushuhudia, na kujiandaa. Na hiyo ni habari njema kweli kweli.
Kuishi tukishuhudia mwisho wa mambo
Wakati mada kuhusu siku za mwisho inaweza kutujaza hofu na kukosa uhakika, kumbuka kwamba mara nyingi hofu ni njia ya dunia. Ulimwengu usio na imani au tumaini. Ulimwengu unaotegemea nguvu na akili ya mwanadamu.
Hatupaswi kuwa na mwitikio wa namna hii. Badala yake, Maandiko yanatuita kwa jambo kubwa zaidi—utayari, matumaini, na ukombozi wetu.
Biblia haituachi tukikisia kuhusu wakati ujao. Kurasa zake zinafunua Mungu mwenye upendo anayetayarisha watu wake na kutoa wokovu kupitia Yesu Kristo. Unabii wa Biblia unapoendelea kutimizwa, tunaitwa kuendelea kusonga mbele, kuendelea kuishi maisha yetu huku Mungu akiwa kiongozi wetu.
Huenda tusijue saa halisi ya kurudi kwa Kristo, lakini tunajua hili: sasa ni wakati wa kutembea kwa imani, kushiriki katika injili, na kuandaa mioyo yetu. Unabii wa wakati wa mwisho kutoka kwa Biblia kwa hakika ni mwaliko wa kuanza kuishi kikamilifu kwa ajili ya Mungu leo.
Je, unatafuta kutiwa moyo na mwongozo zaidi kuhusu siku zijazo?
Chunguza makala haya yaliyojaa matumaini:
Kila moja ya makala haya hutoa maarifa muhimu, yenye msingi katika Biblia ili kukusaidia kukabiliana na yasiyojulikana kwa ujasiri na imani.