Namna ya Kumtegemea Mungu Unaposubiri
Kusubiri kunaweza kuwa miongoni mwa mambo magumu zaidi maishani. Wakati maombi yanapoonekana kutojibiwa au mabadiliko yanapochukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa, ni rahisi kujisikia kukatishwa tamaa, kukosa uhakika, au hofu.
Lakini kumwamini Mungu katika kipindi hiki cha kusubiri ni muhimu kwa ajili ya kupata uzoefu wa mipango na wakati wake bora zaidi. Na habari njema ni kwamba hata wakati mambo yanapoonekana kutokuwa na uhakika, Mungu anafanya kazi kwa ajili ya mema yako, na wakati Wake ni sahihi daima.
Kwa Nini Kuamini Katika Wakati wa Mungu Ni Muhimu
Wakati wa Mungu ni kamilifu, hata wakati ambapo hauendani na mipango yetu.
Biblia inatukumbusha katika Mhubiri 3:11 kwamba “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake” (NKJV).
Aya hii inaonyesha kwamba Mungu anaona picha kubwa na anakuandalia kitu kizuri, hata kama hakionekani mara moja.
Kujifunza kumwamini Yeye katika kusubiri kunakuruhusu kukua katika imani na uvumilivu, ukijua kwamba mipango yake daima ni kwa faida yako.
Mifano ya Kibiblia Juu ya Kungoja kwa Uaminifu
Katika Biblia, tunaona mifano ya watu ambao walilazimika kungojea ahadi za Mungu, lakini waliendelea kuwa waaminifu.
Visa vyao huonyesha kwamba ingawa kusubiri sio jambo rahisi, wakati wa Mungu daima huwa ni kamilifu.
1. Ibrahimu – Mungu alimwahidi Ibrahimu kwamba atakuwa baba wa mataifa mengi, lakini alisubiri kwa miongo kabla ya Isaka kuzaliwa.
Mwanzo 21:1-2 inaweka wazi kwamba “BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema…..kwa muhula alioambiwa na Mungu.” (NKJV). Imani ya Ibrahimu katika ahadi ya Mungu inatukumbusha kwamba Mungu ni mwaminifu, hata kama wakati wa kusubiri ni mrefu.
2. Yusufu – Aliuzwa na ndugu zake kuwa mtumwa na kufungwa bila haki, Yusufu angeweza kupoteza tumaini kwa urahisi. Hata hivyo, alimtegemea Mungu wakati wa miaka yake ya shida. Hatimaye, akawa mtawala wa Misri na kuokoa familia yake dhidi ya njaa.
Mwanzo 50:20 inaonyesha mtazamo wa Yusufu kuhusu hali hiyo kwa ujumla aliporejea nyuma na kusema, “Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema.” (NKJV).
Kisa chake hutufundisha kwamba Mungu anaweza kutumia hata nyakati ngumu kwa kusudi kubwa zaidi.
3. Hana – Mwanamke huyu aliomba kwa miaka mingi ili apate mtoto, akivumilia maumivu na kukatishwa tamaa. Hata hivyo, aliendelea kumtegemea Mungu, na Mungu alimbariki kwa kumpa Samweli, ambaye alikuwa nabii mkubwa.
1 Samweli 1:20 inasema, “Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume” (NKJV).
Uthabiti wake katika maombi unaonyesha kwamba Mungu husikiliza, hata wakati inaonekana kama hakuna kinachotokea.
Visa hivi vinatukumbusha kwamba kungoja siyo wakati uliopotea—Mungu yuko kazini, akitayarisha kitu kikubwa zaidi kuliko tunavyoweza kufikiria.
Hatua za Kumtumaini Mungu Wakati wa Kusubiri
Wakati kusubiri ni jambo gumu, yapo mambo ya kiroho ambayo yanaweza kukusaidia kubaki ukiwa imara katika imani na uaminifu.
1. Jikite katika maombi
Maombi ndiyo ufunguo wa kuendelea katika uhusiano na Mungu wakati wa kipindi cha kusubiri.
Wafilipi 4:6-7 inatwambia, “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” (NKJV).
Omba uvumilivu, uongozi wake, na nguvu ya kumwamini Mungu katika wakati wake.
2. Tafakari Ahadi za Mungu
Wakati mashaka yanapokujia, tafakari maandiko yanayokukumbusha kuhusu uaminifu wa Mungu.
Aya kama Warumi 8:28, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” (NKJV), hukuhakikishia kwamba Mungu anafanya kila kitu kwa faida yako.
3. Kukuza Uvumilivu Kupitia Imani
Uvumilivu unakua kwa kumwamini Mungu, hata muda wa kusubiri unapoonekana kuwa mrefu.
Yakobo 1:3-4 inatuhimiza kwamba “mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi….mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.” (NKJV).
Elewa kwamba kusubiri hujenga nguvu za kiroho na kukuweka tayari kwa ajili ya baraka zinazokuja.
Ushindi dhidi ya mashaka, Kukatishwa Tamaa, na Hofu
Ni kawaida kuwa na mashaka, kukatishwa tamaa, au hofu wakati wa vipindi virefu vya kusubiri. Lakini Mungu anatutaka tuweke wasiwasi wetu kwake.
1 Petro 5:7 inakualika “huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (NKJV).
- Wakati wa mashaka, jikumbushe kuhusu uaminifu wa Mungu katika siku zilizopita. Fikiria jinsi alivyojibu maombi katika siku za nyuma na uamini kwamba bado anafanya kazi katika maisha yako.
- Wakati wa kukatishwa tamaa, kumbuka kwamba kukatishwa tamaa mara nyingi kunatokana na kujaribu kudhibiti matokeo. Hivyo, acha kujaribu kudhibiti na amini kwamba mpango wa Mungu ni bora kuliko wako.
- Wakati unapolemewa na hofu ya yasiyojulikana, kuamini ahadi za Mungu kutakusaidia kupata amani. Tafakari aya kama Isaya 41:10 inasema “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.” (NKJV).
Kupata Amani katika Wakati wa Mungu
Kumwamini Mungu katika kipindi cha kusubiri kunahitaji uvumilivu, imani, na kujisalimisha.
Hata wakati mambo yanapoonekana kutokuwa uhakika, Mungu anafanya kazi nyuma ya pazia kwa ajili ya mema yako.
Kama Abrahamu, Yusufu, na Hana, unaweza kuwa na uhakika kwamba wakati wa Mungu ni kamilifu, na mipango Yake daima inastahili kusubiri.
Ili kutiwa moyo zaidi kuhusu namna ya kuimarisha imani yako kwa Mungu, tembelea kurasa za HFA kuhusu imani, au jiandikishe katika masomo ya Biblia mtandaoni bure.
Jifunze zaidi kuhusu kumtegemea Mungu katika video hii
Tahadhari: Hope for Africa haihusiani na video ifuatayo. Inatolewa tu kama nyenzo muhimu katika kumtegemea Mungu
Kumtegemea Mungu – Randy Skeete 2022 | sabato na Stream Facts
Aya 7 za Biblia kuhusu kumtegemea Mungu na kusubiri
Imeandaliwa na wafanyakazi wa Hope For Africa mnamo Septemba 25, 2024
Aya za Biblia kuhusu “Namna ya kumwamini Mungu katika kipindi cha kusubiri” kutoka Toleo la New King James (NKJV)
- Zaburi 27:14
“Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.”
Maelezo: Mwandishi wa Zaburi anatuhakikishia kwamba tunapomngoja Mungu, atakuja na kuimarisha mioyo yetu.
- Isaya 40:31
“bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”
Maelezo: Tunapomnngoja Mungu katika wakati wake kamilifu, anaahidi kutuimarisha katika safari.
- Maombolezo 3:25-26
“BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo, Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANA Na kumngojea kwa utulivu. ”
Maelezo: Hata katika nyakati ngumu, ni vyema kumngoja Mungu afungue njia kwa ajili yako badala ya kujaribu kutatua mambo peke yako. Aya hii inatuhamasisha kusubiri kwa utulivu kwa Mungu atuokoe kwa sababu Mungu daima ni mwema kwa wale wanaomngojea.
- Zaburi 37:7
“Ukae kimya mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanye hila.”
Maelezo: Aya hii inatoa wito wa kuwa na subira tunapomngoja Mungu atuokoe. Hatupaswi kuwa na wasiwasi tunapoona wengine wakichagua njia za mkato, bali tuamini kwamba Mungu ana mpango bora kwetu.
- Mika 7:7
“Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia.”
Maelezo: Kama Nabii Mika, tunaweza kuamini kwamba Mungu anasikia maombi yetu tunapomngojea, na kwamba atatujibu.
- Zaburi 62:5-6
“Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake.Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,Ngome yangu, sitatikisika sana.”
Maelezo: Tunapomngoja Bwana, tunaweza kuimarisha imani yetu Kwake tukikumbuka kwamba Yeye ndiye pekee anayetujua kweli kweli na kuelewa kilicho bora kwetu.
- Habakuki 2:3
“Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”
Maelezo: Wakati tunasubiri, hatupaswi kupoteza mtazamo wa maono na malengo yetu kwa sababu mwishoni, yatatimia.
Mada na aya hukusanywa kutoka nyenzo mbalimbali na kupitiwa na timu yetu. Ikiwa aya au mada haifai au haipo, tafadhali wasiliana nasi. Maandiko yamechukuliwa kutoka Toleo la New King James®. Hakimiliki © 1982 na Thomas Nelson. Limetumika kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa.
Je una swali?
Usikae nalo! Timu yetu itafurahia kusaidia kujibu chochote kinacho kushangaza. Jaza fomu hapa chini kuuliza.
Zungumza na wengine!
Acha swali au maoni kwa ajili ya wengine kufikiria na kujadili pamoja nawe!
Majadiliano yanaratibiwa. Tafadhali soma Sera Yetu ya Maoni.